Profesa Shivji ataka mjadala wa kitaifa Dira ya Maendeleo

Profesa Issa Shivji akizungumza wakati wa kongamano lililoangazia uhuru wa wanataaluma jijini Dar es salaam. Picha na Elizabeth Edward
Muktasari:
- Profesa Issa Shivji ameitaka Serikali kutoishia kukusanya maoni ya wananchi kwa ujumbe wa simu na mitandao kisha kuwapa wataalamu wachache kuyachakata, bali wananchi wote wajadili kwa ujumla.
Dar es Salaam. Profesa wa Sheria, Issa Shivji amesema ili kufikia mwafaka wa Taifa kimaendeleo, kuna haja ya kuwa na mjadala wa kitaifa utakaohusisha wananchi kwa ujumla.
Profesa Shivji ameyasema hayo leo Juni 8, 2024 alipokuwa akitoa mada katika kongamano la Dira ya Taifa ya maendeleo ya mwaka 2050 lililofanyika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).
Ameitaka Serikali kutoishia kukusanya maoni ya wananchi kwa ujumbe wa simu na mitandao kisha kuwapa wataalamu wachache kuyachakata, bali wananchi wote wajadili kwa ujumla.
“Kwa maoni yangu, Dira haiwezekani bila kuwa na mjadala wa kitaifa ili kufikia mwafaka wa Taifa wa Tanzania tunayotaka.
“Tusifanye ile tunayozoea, wananchi wanatoa maoni sms, mtandao na kadhalika, halafu wataalamu ndio watachambua maoni yao, hapana. Tuwe na mjadala wa kitaifa.
“Popote pale walipo wananchi, vijijini, viwandani na penginepo, ili kujenga mwafaka wa kitaifa wa nchi tunayotaka. Hii ndio Dira yetu na mengine ya kupanga mipango ya muda mrefu na muda mfupi itafuata,” amesema.
Amesema kwa muda mrefu nchi za Afrika zimegeuzwa kuwa maabara ya majaribio ya mipango ya maendeleo na nchi zilizoendelea kwa kupanga program za marekebisho.
“Walikuja na masharti ambayo kwa pamoja tunayaita Structural Adjustment programs (SAPs), yaani kulegeza mashatrti ya biashara ya nje, kubinafsisha mashirika ya umma, kuondoa ruzuku kwenye vyakula vya watu wa kawaida, kutoa huduma kama afya na elimu kwa bei na kwa jumla kuondoa Dola kwenye uchumi,” amesema.
Amesema program hizo zilikuja baada ya nchi nyingi za Afrika kujikuta kwenye mkwamo wa madeni katika miaka 1970 na 1980.
“Tuliambiwa kwamba sio kazi ya Dola kuingia kwenye uchumi, Dola ni mlinzi wa njia za uchumi. Tukahubiriwa na kukubali uchumi huria, lakini kweli ni soko huria.
“Katika mashindano hayo, wale wenye nguvu za kifedha ndio wanapaa na wale wasio na nguvu ndio wanazama kwenye umasikini,” amesema.
Pamoja na program hizo, Profesa Shivi amesema nchi za Afrika ziliendelea kuwa masikini, kwani uchumi haukukua kama ilivyotabiriwa, watu wengi walipoteza ajira zao, wasio na ajira wakaongezeka, umasikini, maradhi, ujinga na vifo vya watoto wachanga pia vikaongezeka.
Kama hiyo haitoshi, Profesa Shivji amesema nchi zilizoendelea zikaja na miradi mingine, kama Mkukuta (Mkakati wa kupunguza umasikini na kukuza Uchumi) na Mkuratibu (Mpango wa kurasimisha mali na biashara Tanzania).
“Mali za wanyonge ni ardhi, hivyo ikawa ni kupima, kupanga ili iweze kuuzika, ndio njia ya kupoteza ardhi. Kwa ufupi, bara letu limekuwa maabara ya kufanyia majaribio, watu wetu wamegeuzwa kuwa viungo bandia kufanyiwa majaribio,” amesema.
Ameendelea kusema katika miongo miwili iliyopita baadhi ya nchi za Afrika zimeanza kuwa na dira za maendeleo ya miaka 25 na miaka 50.
“Safari hii tusikubali kufanyiwa majaribio. Majaribio yaliyofanyika miaka 60 yanatosha. Katika kuandaa Dira ya Taifa letu tuwashirikishe wananchi kikamilifu, popote pale walipo, kupata maoni yao ya nchi wanayotaka, Tanzania wanayotamani. Matamanio yao yapewe kipaumbele, matakwa yao yawe wito wetu,” amesema.
Awali akitoa mfano bora wa dira ya taifa, amelitaja Azimio la Arusha ambalo amesema katika hilo, wananchi walidhamiria kujenga nchi ya kijamaa, nchi ya usawa na isiyo na mataba ya wafanyakazi na wasio na wafanyakazi.
“Nchi isyo na unyonyaji, ukandamizwaji, uteswaji, nchi inayojitegemea, inayojitawala na kufanya maamuzi yake yenyewe. Mtazamo wa kifalsafa nyuma ya Azimio la Arusha ulizama kwenye msingi wa binadamu wote ni sawa,” amesema.