Profesa Mkenda: Tumeanza maandalizi shule za mafunzo ya amali

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Adolf Mkenda akisisitiza jambo wakati alipotembelea eneo la ujenzi wa Chuo Kikuu cha Ardhi kampasi ya Mwanza katika kijiji cha Karumo wilayani Sengerema. Picha na Saada Amir
Muktasari:
Kwa mujibu wa Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Adolf Mkenda, jukumu la kutambua shule za sekondari zitakazoongezewa shule za msingi linatekelezwa na wizara hiyo kwa kushirikiana na Tamisemi.
Sengerema. Serikali imeanza kutekeleza mpango wa elimu ya msingi kuanzia darasa la awali hadi kidato cha nne kwa kutambua shule za sekondari zitakazoongezewa wigo wa shule za msingi.
Kwa mujibu wa Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Adolf Mkenda, jukumu la kutambua shule za sekondari zitakazoongezewa shule za msingi linatekelezwa na wizara hiyo kwa kushirikiana na Tamisemi.
“Kwa kushirikiana na Tamisemi tumeanza kazi ya kuzitambua shule za sekondari nchi nzima ambazo tutajenga shule za msingi,”amesema Profesa Mkenda
Waziri huyo ambaye yuko kwenye ziara ya kukagua miundombinu ya elimu katika mikoa ya Mwanza na Mara amesema shule zitakazoingia kwenye mpango huo zitakuwa za mafunzo kwa vitendo (mafunzo ya amali) kulingana na shughuli za kiuchumi katika maeneo husika.
‘’Wanafunzi watakaomaliza masomo yao ya kidato za nne katika shule hizo watapewa na cheti cha kuhitimu elimu ya sekondari na cha kumaliza mafunzo ya amali,’’ amesema
Amesema mpango huo utakaoanza baada ya kupatikana kwa kibali cha sera na mtaala mpya wa elimu utahusisha elimu ya msingi utakaoishia darasa la sita kabla ya wanafunzi kufanya mitihani na kuendelea hadi kidato cha nne.
Profesa Mkenda amesema Serikali inakusudia kuongeza madarasa ya kidato cha kwanza hadi cha nne katika shule za msingi ambazo nyngi kwa sasa hazina shule za sekondari.
Akikagua maeneo ya ujenzi wa miundombinu ya elimu wilayani Sengerema Juni 5, 2023, Profesa Mkenda aliwapongeza wakazi wa wilaya hiyo kwa kujitolea nguvu na mali kujenga zaidi ya shule mpya 17 na kuwasihi wananchi wa maeneo mengine nchini kuiga mfano huo.
“Kwa sera ya elimu bila malipo hadi kidato cha sita, wananchi hawalazimishwi kutoa michango ya kujenga miundombinu ya elimu. Lakini hiyo haimaanishi wazazi wasijipange kuchangia kwa hiari kwenye miundombinu ya shule, kwenye chakula (cha mchana) cha wanafunzi (kwa shule za kutwa)….elimu bila ada ni kwamba hakuna mwanafunzi mtoto atarudishwa nyumbani kwa kukosa ada au michango,’’ amesema
Waziri huyo mwenye dhamana ya elimu ameahidi kuwa Serikali itakamilisha ujenzi wa miundombinu ya elimu iliyojengwa kwa nguvu za wananchi wilayani Sengerema.
Katika hatua nyingine, Profesa Mkenda ametembelea na kukagua mradi wa ujenzi wa tawi la Chuo Kikuu cha Ardhi kampasa ya Mwanza kinachojengwa eneo la Kijiji cha Karumo wilayani Sengerema.
Akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi huo, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Cha Ardhi, Profesa Evaristo Liwa amesema zaidi ya Sh17.8 bilioni zitatumika kujenga majengo matano ya kampasi ya Mwanza, mradi unaotarajiwa unaotarajiwa kukamilika ndani ya kipindi cha miezi 15 ijayo kuanzia Septemba, mwaka huu.
Amesema asilimia 70 ya gharama hiyo itatumika kujenga majengo ya studio, utawala, ofisi za walimu, maktaba, bweni na zahanati huku asilimia 30 iliyosalia itatumika kununulia samani na uandaaji wa mitaala kwa awamu ya kwanza ya mradi.
Profesa Mkenda pia ametembelea na kukagua maandalizi ya ujenzi wa Chuo cha Ufundi Veta Halmashauri ya Buchosa kitakachojengwa kwa gharama ya zaidi ya Sh3 bilioni.