Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Profesa Assad aeleza mchango wa Rais Mkapa Chuo Kikuu cha Waislamu Morogoro

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Waislamu Morogoro, Profesa Mussa Hassad akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, kuhusu maadhimisho ya miaka 20 ya chuo hicho. Picha na Michael Matemanga

Muktasari:

  • Mchakato wa kukabidhiwa  chuo hicho ulifanyika mwaka 2004 na Rais Benjamin Mkapa, kabla ya kuzinduliwa mwaka mmoja baadaye.

Dar es Salaam. Wakati Chuo Kikuu cha Waislamu cha Morogoro (MUM) kikielekea kutimiza miaka 20 Juni 2025, makamu mkuu wa hicho, Profesa Mussa Assad ameelezea mchango wa Rais mstaafu wa Tanzania, hayati Benjamin Mkapa hadi kuzinduliwa na kuanza kwa chuo hicho.

Amesema chuo hicho kimetokana na mchango wa Rais huyo ambaye alitaka kuboresha elimu kwa Waislamu nchini.

Akigusia sababu za Rais Mkapa kuwakabidhi chuo hicho, Profesa Assad huku akinukuu maneno ya Rais huyo aliyefariki dunia Julai 2020, amesema:"Nakumbuka mazungumzo ya mzee Mkapa, alisema Waislamu wamerudi nyuma katika elimu, chuo hiki ni mchango wangu katika kuchangia elimu yao."

Amesema Rais Mkapa alipowakabidhiwa chuo hicho mwaka 2004, mwaka mmoja baadaye kilizinduliwa na kuanza kutoa elimu kikiwa na idadi ndogo ya wanafunzi.

"Kilipoanza kilikuwa na wanafunzi 260 pekee, sasa kina wanafunzi 4,760, tumepiga hatua kubwa kama ilivyotarajiwa na jamii ya Kiislamu," amesema profesa Assad leo Aprili 28, 2025 wakati akitangaza maadhimisho ya miaka 20 ya Chuo hicho.

Maadhimisho hayo yataanza Juni 11 na kilele chake kitakuwa Juni 20, 2025, katika kitivo cha chuo hicho mjini Morogoro yakitarajiwa kuongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan.

Siku hiyo pia, kutakuwa na utoaji tuzo kwa waasisi wa chuo hicho, hafla itakayokwenda  sanjari matukio mbalimbali ya kitaaluma na kijamii na kuwa na makala maalumu ambayo itaonesha miaka 20 ya chuo kilipotoka na mipango yake ijayo.

"MUM kama taasisi nyingine, nayo imepitia changamoto kadha wa kadha ambazo zitaelezwa katika makala maalumu ya miaka 20 katika maadhimisho hayo huku pia chuo kikitoa tuzo kwa waasisi wake na baadhi ya watu waliotoa mchango katika mafanikio ya chuo hicho," amesema profesa Assad.

Amesema katika maadhimisho hayo pia, kutakuwa na dua maalumu mbili zitakazoongozwa na Mufti wa Tanzania, Sheikh Mkuu, Abubakar Zuber.

Akizungumza kwa niaba ya Mufti, mwakilishi kutoka Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata), Mwenda Said Mwenda amesema MUM ni ufunguo maendeleo kwa jamii.

Amesema kupitia ushirikiano wa jamii, wameweza kuendeleza mafanikio ya chuo hicho.

"Kwa niaba ya Bakwata, tunawaalika wananchi kusherehekea miaka hii 20 ambayo si jambo dogo," amesema.

Wakielezea namna chuo hicho kilivyoanzishwa, baadhi ya wanazuoni wamesema kililenga kutoa fursa kwa Waislamu na hata wale wasio Waislamu kupata elimu.

"Wakati Rais Mkapa anatukabidhi majengo haya nilikuwa mbunge wa Morogoro mjini," amesema Shamim Khan.

"Ilikuwa ni fursa kubwa kwa Waislamu, MUM tangu wakati huo kimekuwa  ni chuo cha Kitanzania, ambacho katika miaka 20 kimepiga hatua na kuwalea vijana kitaaluma na kimaadili," amesema.

Mwanazuoni mwingine, Sheikh Amir Mussa Kundecha alianza kwa kueleza moja ya misemo ya wanazuoni akibainisha ni vigumu kumtofautisha binadamu na mnyama isipokuwa kwa elimu.

"Chuo chetu ni kigezo cha tafsiri ya maneno ya wanazuoni, kwani kuna elimu dunia na elimu akhera, na zote zinapatikana duniani," amesema.

Sheikh Kundecha amesema katika miaka 20 ya MUM ni ya kuangalia kipindi kijacho ili kiwe bora zaidi ya kilichopita.