Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ponografia za watoto mtandaoni zaongezeka, wadau wataka udhibiti

Muktasari:

  • Matukio ya uchapishaji wa ponografia za watoto mitandaoni umeongezeka hadi kufikia matukio 38 yaliyorekodiwa mwaka 2024 kutoka tukio moja mwaka 2023 huku picha za ngono za watu wazima zikipungua kutoka matukio 45 hadi 33 mtawaliwa.

Dar es Salaam. Wadau wametaka sheria kali zichukuliwe kwa watu wanaosambaza ponographia za watoto katika mitandao ya kijamii ili iwe fundisho kwa wengine wanaotamani kufanya hivyo.

Hilo liende sambamba na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kuimarisha ushirikiano na kampuni kubwa zinazomiliki mitandao ya kijamii kama Meta, ili kusaidia kudhibiti maudhui hayo moja kwa moja ikiwa matumizi ya akaunti binafsi yatashindikana.

Hayo yanasemwa kufuatia ongezeko la uchapishaji wa ponografia za watoto hadi kufikia matukio 38 yaliyorekodiwa mwaka 2024 kutoka tukio 1 mwaka 2023.

Ripoti ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) inaonyesha wakati ponografia za watoto zikiongezeka kuchapishwa, picha za ngono za watu wazima zinapungua.

Akizungumza na Mwananchi, mwanaharakati wa haki za binadamu, Carol Ndosi amesema ni vyema suala la mitandao salama liingizwe katika mitalaa ili watoto wajifunze namna ya kujilinda tangu wakiwa wadogo.

Amesema suala hilo ni la muhimu hasa kabla ya kuwafundisha watoto namna ya kutumia kompyuta, ili wajue usalama na haki zao za kidijitali, anachopaswa kufanya na asichotakiwa kufanya.

“Elimu ni muhimu sana kwa taasisu za umma na hata sekta binafsi kuna kazi kubwa, tuwafikie wazazi kwa sababu kinachoonekana ni wazazi wameshindwa kuendana na matumizi ya kidijitali na wengine wamepitwa na watoto,” amesema.

Amesema jambo hilo limefanya baadhi yao kushindwa kudhibti maudhui ambayo watoto wanatumia akishika simu zao.

“Na siku hizi tumegundua kwenye games wanazocheza watu, wanaweza kutumiana ujumbe mfupi wa maandishi na hili linaanza kushika hatamu, hivyo ni vyema wazazi waingizwe kwenye mfumo wa kutoa elimu ili wajue madhara haya,” amesema.

Amesema hilo liende sambamba na elimu kwa walezi wa watoto ambao wako nyumbani au shuleni.


Wazazi watia neno

Wakati Ndosi akiyasema hayo, Beatrice Beatus mkazi wa Ubungo na mzazi amesema mabadiliko ya kasi ya sayansi na taknolojia yamewaacha wazazi wengi nyuma.

Hali hiyo inafanya baadhi ya watoto kujua mambo mengi zaidi ya wazazi wao jambo ambalo linawafanya kuingia sehemu ambazo si salama kwao.

“Pia watoto wengi wako katika kile kipindi cha kutaka kujaribu vitu vingi, bila kuangalia itakuwa na athari gani baadaye, hivyo ni vyema mzazi ukahakikisha unafuatilia mienendo ya mtoto wako ili kisaidia kudhibiti mambo yasiyofaa yasiende ulimwengu wa mitandao ya kijamii ambayo haisahau,” amesema.

Kwa upande wake Lawrence Kituo, amesema hali hii inachangiwa na baadhi ya wazazi kusahau majukumu yao ya malezi na kuacha watoto kuamua kila kitu wanachofanya wenyewe.

“Unakuta mtoto mdogo hana kazi ya kumwingizia kipato, anamiliki simu kubwa kuliko wewe baba au mama lakini hauhoji imetoka wapi, unaona ni sawa. Anatumia vitu vya gharama hujali, anashushwa na gari ambayo hujawahi kumiliki hujali, mwisho wa siku ukikutana na picha zake za utupu mtandaoni usimkaripie kwa sababu ulishindwa kuzuia hilo,” amesema Kituo.

Amesema ni vyema wazazi warudi kusimamia majukumu yao kikamilifu na kuacha tabia ya kuwategemea wasaidizi wao wa nyumbani katika kila kitu.

Wakati haya yakielezwa, Jeshi la Polisi linataja sababu za kuwepo kwa matukio haya kuwa ni hali duni ya kiuchumi, kukosa maadili, utandawazi na tamaa ya kujipatia kipato au mali.


Nini Kifanyike

Ndosi ambaye pia ni moja ya watu wanaohamasisha matumizi salama ya mitandao, amesema ili kukomesha hali hii ni vyema kuhakikisha wanaovunja sheria na kuchapisha picha hizi mitandaoni wanawajibishwa.

“Kwa mfano katika takwimu hizi zilizotolewa jamhuri ingekuwa inatwambia imeshtaki wangapi, kesi ilikuwaje, hukumu iliyotolewa hii hapa hii ingechagiza watu wasirudie kosa hilo,” amesema.

Hiyo ingefanya watu kujua kuwa endapo watakutwa na kosa la kusambaza video hizo, watahukumiwa kwa sheria gani na adhabu gani wataipata.

“Pia nadhani ni wakati sasa wa kujenga mahusiano mazuri na kampuni kubwa za teknolojia ili ziweze kusaidia pindi video inapochapishwa ishushwe haraka, licha ya kutumia akaunti binafsi lakini kampuni hizi kama Instagram zinaweza kusaidia,” amesema Carol.

Suala la udhibiti wa sheria liliungwa mkono na Mwanasaikolojia Charles Kalungu ambaye amesema sheria kali zinaweza kusaidia kudhibiti vitendo hivi.

“Adhabu za mfano zitolewe kwa wanaochapisha picha hizi mitandaoni, ili wengine waogope kuendelea kusambaza wanapozipata,” amesema Kalungu.

Katika hilo, jeshi la polisi linasema linashirikiana na taasisi mbalimbali katika kuzuia makosa ya uhalifu wa kimtandao.

“Pia tunaelimisha watumiaji wa mitandao juu ya usiri na umuhimu wa kutomwamini mtu kuhusu nywila, sambamba na kuendelea kutoa elimu ya sheria ya Makosa ya Mtandao Na. 14 ya Mwaka, 2015,” limesema Jeshi la Polisi.


Namna ya kumsaidia muathirika

Wakati video hizo zikisambazwa huku na kule, mwanasaikolojia anasema ni vyema kuhakikisha wahusika wanasaidiwa na jamii inayowazunguka kukabiliana na hali hiyo badala ya kulaumiwa.

Hilo lifanyike kwa kuhakikisha wanapatiwa msaada endelevu wa kisaikolojia ili waweze kukubaliana na hali iliyotokea kuwa haiwezi kubadilika.

Bila kufanya hivyo watoto wanaweza kukabiliwa na hali ya mfadhaiko unaoweza kuathiri maisha yao ya baadaye, hivyo ni vyema jamii inayowazunguka isiwe chanzo cha hali hiyo.

“Kama mazingira yanayomzunguka ni yale ya kulaumiwa kila wakati, ni ngumu kwao kukabiliana na hali hii kwa urahisi lakini kama ni jamii inayomtia moyo na kumwambia lililotokea limetokea, ni rahisi kuepukana na madhara ya hali hii,” amesema Kalungu.