Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Pombe inavyogharimu maisha ya watu Rukwa

Muktasari:

  • Watu zaidi ya 30 wamepoteza maisha kwa nyakati tofauti kati ya mwaka 2024 hadi Aprili 2025 kutokana na unywaji wa pombe usiozingatia afya. Kutokana na hali hiyo, Jeshi la Polisi limekuja na kampeni maalumu ya unywaji salama kwa kuwa hawawezi kuzuia watu wasinywe pombe.

Rukwa. Jeshi la Polisi Mkoa wa Rukwa limeanzisha kampeni maalumu ya unywaji pombe salama ili kuepuka madhara yatokanayo na unywaji usiozingatia afya.

Akizungumza leo Ijumaa, Aprili 25, 2025 katika mkutano wa hadhara ulioandaliwa na jeshi hilo katika Kata ya Chanji, Manispaa ya Sumbawanga, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa, Shadrack Masija amesema watu 32 wamepoteza maisha kutokana na unywaji wa pombe usiozingatia afya.

Amesema moja ya sababu kubwa kutokula chakula na kutochagua aina ya pombe kulingana na afya aliyonayo mnywaji.

Amesema kuwa idadi hiyo ya watu 32 imethibitishwa na daktari, akifafanua kuwa vifo hivyo vimetokana na pombe kuzidi mwilini.

Akizungumzia kuhusu madhara ya unywaji wa pombe, Kamanda Masija amesema kumekuwa na wimbi la watoto wa mitaani kwa sababu wazazi/walezi wamewatelekeza.

Pia amesema ukosefu wa malezi bora kwa watoto na lishe bora kunakotokana na kukosa chakula cha kutosha kunasababisha udumavu.

“Unywaji holela wa pombe unasababisha ngono zembe, ubakaji, ulawiti wa watoto na ukosefu wa maadili katika jamii,” amesema.

Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Zahanati ya Kizwite, Dk Simon Mjema amesema unywaji wa pombe kupitiliza umekuwa changamoto kwa afya ya familia, jamii na uchumi wa taifa kwa ujumla.

Amesema unywaji wa pombe unaweza kusababisha ugonjwa wa ini, shinikizo la damu, kiharusi na hatimaye kusababisha kifo.

Amesema pia unywaji wa pombe unaweza kusababisha matatizo ya afya ya akili kwa sababu pombe huathiri mfumo wa utendaji kazi wa ubongo.

Aidha, amewataka wananchi kufanya kazi kwa bidii ili kuwa na familia zenye afya njema.

Akizindua kampeni hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga, Nyakia Chirukile amewataka wananchi kuzingatia kanuni za afya na kuacha tabia ya kuwapa watoto wadogo pombe ili walale.

“Kuna tabia ya baadhi ya kinamama kuwapa watoto wadogo pombe ili walale na wao waendelee na shughuli zao, hali hiyo madhara makubwa ya kiafya ikiwemo udumavu na utapiamlo,” ameeleza Chirukile.

Amesisitiza kuwa ni muhimu watoto wakapewa lishe bora kwa kupewa chakula mchanganyiko na kuachana na tabia ya kuwapa pombe mara kwa mara.

Aidha, Chirukile amesema kuwa unywaji wa pombe kupindukia unarudisha nyuma maendeleo ya taifa na kuchochea umaskini kwa jamii.

Naye mraibu wa pombe kutoka katika Mtaa wa Soweto, Kata ya Chanji, Ezebio Senga amesema; “Siwezi kuacha pombe, kwa kuwa nikinywa siwazi chochote. Nakunywa, nalala, maisha yanaendelea.”

Aurelia Linguya, mke wa Senga, anasema mume wake alianza kunywa pombe hata kabla hawajaoana na ikafikia hatua ya kuwa mlevi kupindukia.

“Hafanyi kazi, ni mgomvi, hajui thamani ya maisha. Anachojua yeye ni kunywa pombe tu. Ameniachia mzigo mkubwa, ninalea watoto mwenyewe,” amesema Lunguya.

Sheikh Mohammed Abdallah amesema jamii inapaswa kumgeukia Mwenyezi Mungu na kuacha kufanya matendo mabaya.