Polisi yataja sababu ya kumkamata Niffer
Dar es Salaam. Wakati taarifa zikisambaa mitandaoni zikidai kutekwa na watu wasiojulikana mfanyabiashara, Jenifer Jovin maarufu Niffer katika eneo la Sinza jijini Dar es Salaam, Jeshi la Polisi limethibitisha kumshikilia kwa tuhuma za kuhamasisha vurugu.
Taarifa iliyotolewa leo Jumatatu Oktoba 27,2025 na Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro amethibitisha jeshi hilo kumkamata Niffer na linamuhoji.
"Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam Oktoba 27,2025 majira ya saa 9 mchana eneo la Sinza Kumekucha, limemkamata na linamuhoji Jenifer Bilikwiza Jovin miaka 26 mkazi wa Masaki Peninsula Kinondoni," taarifa ya polisi imeeleza.
Niffer anashikiliwa kwa tuhuma za kuhamasisha vurugu na kuharibu miundombinu katika maeneo mbalimbali jijini kuelekea Uchaguzi Mkuu 2025.
Kamanda Muliro katika taarifa hiyo ameeleza kuwa hatua zaidi za kisheria zinaendelea kuzingatiwa dhidi ya mtuhumiwa.
Endelea kufuatilia Mwananchi