Polisi yajitenga kukamatwa Wakili Mwabukusi na wenzake

Kamanda wa Polisi Mkoa (RPC) Morogoro Alex Mkama
Muktasari:
- Wakati taarifa za kukamatwa na kushikiliwa kwa Wakili Boniface Mwabukusi na wanzake wawili, katika Kituo cha Polisi cha Mikumi, mkoani wa Morogoro zikisambaa, Kamanda wa Polisi Mkoa huo (RPC) Alex Mkama, amesema hana taarifa za kukamatwa kwa watu hao.
Dar/Morogoro. Wakati taarifa za kukamatwa na kushikiliwa kwa Wakili Boniface Mwabukusi na wanzake wawili, katika Kituo cha Polisi cha Mikumi, mkoani wa Morogoro zikisambaa, Kamanda wa Polisi Mkoa huo (RPC) Alex Mkama, amesema hana taarifa za kukamatwa kwa watu hao.
Taarifa hizo zilianza kusambaa alfajiri ya leo Jumamosi Agosti 12, 2023 katika mitandao ya kijamii zikieleza Wakili Mwabukusi, Katibu wa Chadema Kanda ya Kati Emmanuel Masonga na Mdude Nyagali, wamekamatwa wakiwa katika gari moja ambapo walizuiwa katika kizuizi cha Mikumi na watu waliojitambulisha kuwa ni Polisi.
"Sijapata taarifa ya kukamatwa kwa hao watu, kuna mwandishi mwenzako amenipigia pia kuniuliza hilo jambo, na nimefuatilia Kituo cha Mikumi ili kujua kama ni kweli, lakini wamesema hakuna mtu aliyekamtwa, nikipata lolote nitawapa taarifa," amesema RPC Mkama.
Inadaiwa kuwa Wakili Mwabukusi na wenzake, walizuiwa katika kizuizi cha Mikumi na watu waliojitambulisha kuwa ni Polisi na kwamba kwa sasa wanashikiliwa Kituo cha Polisi Mikumi kutokana na kwa maelekezo ya Kamanda Mkama, ambaye amedai kutokuwa na taarifa yeyote ya tukio hilo.
Akizungumza na Mwananchi Digital, Katibu wa Chadema Mkoa wa Morogoro, Barnabas Okola, amesistiza juu ya kukamatwa kwa watu hao maeneo ya Mikumi na kwamba wao kama viongozi wa mkoa, wanalifuatilia sual hilo.
Okola ameiambia Mwananchi Digital kuwa wamefika Kituo Kikuu cha Polisi Morogoro ili kujua kama watu hao wamefikishwa hapo, hata hivyo walijibiwa kuwa hawapo, na kwamba labda wafuatilie kwingine.
"Ni kweli wamekamatwa Mikumi na kuna kiongozi wetu pale Mikumi tunawasiliana nae yuko Kituo cha Polisi Mikumi, amemuona Wakili Mwabukusi na amemkabidhi ufunguo wa gari yake na kumwambia ameambiwa anapelekwa chumba cha upelelezi kituoni hapo hivyo anasubiri," amesema Okola.
Amesema anaamini kuwa, kama Wakili Mwabukusi yuko kituoni hapo basi na wenzake watakuwa hapo.
Wakili Mwabukusi ni miongoni mwa mawakili wa walalamikaji katika kesi ya kupinga mkataba wa ushirikiano wa kiuchumi na kijamii kati ya Serikali ya Tanzania na Dubai (IGA), iliyokuwa imefunguliwa Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya.
Kesi hiyo ya kikatiba namba 5 ya mwaka 2023 ilifunguliwa na mawakili wanne kutoka mikoa tofautofauti ambao ni Alphonce Lusako, Emmanuel Chengula, Raphael Ngonde na Frank Nyalus dhidi ya Serikali.
Hata hivyo Agosti 10, mwaka huu, Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya ilitoa uamuzi wa kesi hiyo ikisema mkataba huo hauna tatizo hivyo pingamizi lililowekwa na walalamikaji halina mashiko.