Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Polisi yadaiwa kumshikilia mmoja tukio la mabinti wawili kutoweka Arusha

Wasichana Kareen Didas (kulia, aliyevalia gauni jeusi) na Nakivona Toroka (kushoto, aliyevalia gauni jekundu) wakiwa katika picha ya pamoja kabla ya kutoweka kwao.

Muktasari:

  • Inadaiwa kuwa wasichana hao walitoweka katika mazingira ya kutatanisha Juni 20, 2025, mkoani Arusha, baada ya kuhudhuria sherehe ya kupongezana kufuatia kumaliza mitihani ya mwaka wa kwanza wa chuo.



Arusha. Mfanyabiashara, Godwin Ndossi mkazi wa Shangarai mkoani Arusha anadaiwa kushikiliwa na Jeshi la Polisi kwa mahojiano kuhusiana na tukio la kupotea kwa Kareen Marc Didas (23) na Nakivona Toroka maarufu kwa jina la ‘Rahma’ (22).

Inadaiwa kuwa wasichana hao walitoweka katika mazingira ya kutatanisha Juni 20, 2025, mkoani Arusha, baada ya kuhudhuria sherehe ya kupongezana kufuatia kumaliza mitihani ya mwaka wa kwanza wa chuo.

Wakili wa Ndossi, Liberia Mosoi amesema mteja wake alijisalimisha jana katika Kituo cha Polisi Kati na baada ya kutoa maelezo aliendelea kubaki kituoni hapo kwa ajili ya taratibu zaidi za kipolisi.

 “Mteja wangu alifika polisi kutoa maelezo baada ya kuona anatuhumiwa mitandaoni. Hata hivyo, baada ya maelezo yake kuchukuliwa, ameendelea kushikiliwa kwa taratibu nyingine za kipolisi.”

Mosoi amesema wanaendelea kufuatilia uwezekano wa kupata dhamana na iwapo kutakuwa na hatua nyingine za kisheria, watachukua hatua stahiki.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, SACP Justine Masejo amesema uchunguzi wa tukio hilo bado unaendelea.

“Kama nilivyokueleza awali, upelelezi unaendelea na tutatoa taarifa zaidi baadaye,” amesema alipozungumza na Mwananchi kwa simu.

Leo Jumatano Mei 6, 2026 alipoulizwa kuhusu idadi ya watu wanaoshikiliwa kuhusiana na tukio hilo mpaka sasa, alikata simu.

Hata hivyo, kabla ya kushikiliwa, Ndossi alidai kuwa meneja wake pamoja na dereva wake tayari walikuwa wanashikiliwa na Jeshi la Polisi kuhusiana na tukio hilo.


Awali tukio lilivyokuwa

Taarifa za kupotea kwa wasichana hao zilianza kusambaa mitandaoni Mei 2, 2026, huku mfanyabiashara huyo akituhumiwa kuwaalika katika sherehe ya usiku.

Inadaiwa kuwa Kareen na Nakivona (Rahma) walihudhuria sherehe hiyo iliyofanyika Juni 20, 2025 katika eneo la Shangarai, wilayani Arumeru na tangu siku hiyo hawajaonekana.

Tukio hilo liliripotiwa katika Kituo cha Polisi Tengeru na kuandikishwa kwa jalada namba TEG/RB/342/2025.

Akizungumza kwa njia ya simu, dada wa Kareen, Elizabeth Didas amesema mdogo wake alikuwa akiishi Shangarai, wilayani Arumeru, akijishughulisha na biashara ndogondogo pamoja na masomo ya uhasibu kupitia Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT) kwa njia ya mtandao.

Amesema baada ya kupotea kwa mdogo wake, walitoa taarifa polisi ili uchunguzi ufanyike, lakini hadi sasa ni zaidi ya siku 320 zimepita hakuna majibu yoyote yaliyotolewa.

 “Hata mchumba wake ambaye inadaiwa alikuwa naye, alipofuatiliwa hakuwa akitoa ushirikiano.”

Elizabeth amesema wanafarijika kuona kuwa baada ya taarifa kusambaa mitandaoni na kuripotiwa na vyombo vya habari, hatua za uchunguzi zimeanza kuchukuliwa.