Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mapya yaibuka wasichana wawili waliotoweka Arusha

Wasichana Kareen Didas (kulia, aliyevalia gauni jeusi) na Nakivona Toroka (kushoto, aliyevalia gauni jekundu) wakiwa katika picha ya pamoja kabla ya kutoweka kwao.

Muktasari:

  • Kwa mujibu wa taarifa za familia, wasichana hao waliondoka Juni 20, 2025 kwenda kwenye sherehe ya kuhitimu mtihani wa mwaka wa kwanza chuo, lakini hawakurudi



Arusha. Taarifa mpya zimeibuka kuhusu sakata la kutoweka katika mazingira ya kutatanisha Kareen Marc Didas (23) na Nakivona Toroka maarufu kama Rahma (22), Juni 20, 2025, wilayani Arumeru mkoani Arusha, huku mtu anayetajwa kuwa wa mwisho kuwaona akikanusha tuhuma zinazomkabili.

Akizungumza na Mwananchi jana Jumanne Mei 5, 2026 , mfanyabiashara wa utalii jijini Arusha, Godwin Ndossi, amekanusha madai ya kuwa na uhusiano wa kimapenzi na Kareen au kuhusika kwa namna yoyote na kupotea kwa wasichana hao.

Amesema walikuwa marafiki wa kawaida na kwamba taarifa za kumtuhumu zimekuwa zikisambazwa mitandaoni bila ushahidi.

Ndossi ameeleza kuwa, siku ya tukio, wasichana hao walifika katika hoteli yake kwa ajili ya burudani ya kawaida ya chakula na vinywaji inayofanyika kila Ijumaa, baadaye waliondoka kama ilivyo kwa wateja wengine.

“Nilijaribu kumpigia Kareen simu asubuhi yake ili kujua kama alifika salama lakini hakupokea. Nilipowasiliana na dada yake, nilijulishwa naye pia hampati,” amesema.

Ameongeza kuwa baadaye Kareen alimtumia ujumbe mfupi akieleza kuwa alikuwa anaelekea Namanga kumsindikiza rafiki yake, Nakivona, lakini baada ya hapo mawasiliano yalikatika kabisa.

Kutokana na hali hiyo, Ndossi amesema alichukua hatua ya kuwasiliana na familia ya Kareen pamoja na polisi, ingawa awali alidai kukumbana na changamoto ya kupokewa taarifa zake kwa kuwa hakuwa ndugu wa karibu.

Aidha, amesema alitoa fedha kwa familia ya Kareen ili kusaidia gharama za usafiri kwa ajili ya kufuatilia tukio hilo Arusha, lakini juhudi hizo hazikuzaa matunda baada ya ndugu kushindwa kufika kwa sababu mbalimbali, ikiwamo dharura na matatizo ya kiafya.

Baada ya siku kadhaa, Ndossi amesema aliripoti tena polisi na jalada lilifunguliwa na upelelezi kuanza.

 Hata hivyo, anashangaa kuona anahusishwa na tukio hilo, akidai hata wafanyakazi wake walishikiliwa na polisi bila maelezo ya kina.

“Mimi si mtuhumiwa. Kama kuna jambo wanahitaji kutoka kwangu, wangeniita rasmi badala ya kufanya mambo kwa mshtuko,” amesema.

Dada wa Kareen, Elizabeth Didas amethibitisha kupokea fedha kutoka kwa Ndossi kwa ajili ya kumwezesha mama yao kusafiri Arusha kufuatilia tukio hilo.

Hata hivyo, amesema safari hiyo haikuwezekana baada ya baba yao kupata ajali njiani wakati akimsindikiza kwenda kituo cha basi.

Elizabeth amesema licha ya changamoto hizo, familia imeendelea kufuatilia suala hilo bila mafanikio makubwa, na sasa wameitwa na mkuu wa Wilaya ya Arumeru kwa ajili ya maelezo zaidi.

“Tulishawahi kutoa taarifa kwa vyombo vya usalama na hata kufika ofisi za wilaya, lakini bado hatujapata majibu ya kuridhisha kuhusu alipo mdogo wangu,” amesema.

Awali, taarifa za kupotea kwa wasichana hao zilianza kusambaa mitandaoni Mei 2, 2026, zikimuhusisha Ndossi kuwa ndiye aliyewaalika kwenye sherehe ya usiku kabla ya kutoweka kwao, madai ambayo ameyakanusha.

Kwa mujibu wa familia, Kareen alikuwa akiishi Shangarai, Arumeru, akijishughulisha na biashara ndogo ndogo huku akisoma uhasibu kwa njia ya mtandao.

Siku ya tukio, aliondoka nyumbani kwenda kumchukua rafiki yake Nakivona na kuelekea kwenye sherehe aliyodai ameandaliwa kumpongeza baada ya kumaliza mitihani.

Tangu walipoondoka usiku huo wa Juni 20, 2025, hawajawahi kuonekana tena.

Ndugu wa Nakivona, Kakai Daudi amesema waliripoti tukio hilo polisi lakini hadi sasa hakuna maendeleo yanayoonekana, hali inayozidi kuongeza majonzi kwa familia.

Kamanda wa Mkoa wa Arusha, Justine Masejo amesema uchunguzi wa tukio hilo unaendelea na taarifa kamili zitatolewa pindi uchunguzi utakapokamilika.

Wakati uchunguzi ukiendelea, familia za wasichana hao zimeendelea kuomba msaada wa Serikali na vyombo vya dola kuhakikisha ukweli unajulikana na haki inapatikana.