Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Polisi wazuia ndoa ya mwanafunzi

Muktasari:

  • Mwanafunzi wa kidato cha pili (15) katika Shule ya Sekondari Chamazi amenusurika kuolewa baada ya Serikali kuingilia kati huku mumewe mtarajiwa, Maulid Athuman, mshenga na Sheikh wakikamatwa na Polisi.


Dar es Salaam. Mwanafunzi wa kidato cha pili (15) katika Shule ya Sekondari Chamazi amenusurika kuolewa baada ya Serikali kuingilia kati huku mumewe mtarajiwa, Maulid Athuman, mshenga na Sheikh wakikamatwa na Polisi.

Binti huyo anasema alikubali kuolewa ili kuepuka kero ya migogoro ya ndoa ya wazazi wake ambayo amekuwa akiishuhudia kwa muda mrefu, ingawa bado alikuwa akitamani kuendelea kusoma.

Wakati hilo likitokea, Serikali imesema itaanzisha mfumo wa kufuatilia ushughulikiaji wa matukio ya ukatili wa kijinsia yanayopokelewa ili wahusika wachukuliwe hatua haraka.

Akizungumza jana na waandishi wa habari mbele ya Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maaalumu, Dk Dorothy Gwajima, Ofisa Ustawi Manispaa ya Temeke, Lilian Mafole alisema Aprili 14, 2022 mchana walipigiwa simu na msamaria mwema ikiwataarifu kuna mwanafunzi anatarajiwa kufunga ndoa Aprili 15, 2022 saa 2:00 usiku.

“Baada ya kupokea taarifa hiyo niliwasiliana na vitengo tofauti, tukafanya uchunguzi kujiridhisha na kuyafahamu vizuri mazingira ya tukio na tukafanikiwa. Siku ya tukio saa mbili usiku tulifika tukiwa na timu nzima akiwamo mkuu wa shule na polisi.

“Tulifanikiwa kuzuia ndoa hiyo kufungwa na watuhumiwa watatu wamekamatwa na kupelekwa kituo cha polisi kwa hatua za kisheria,” alisema Mafole.

Alisema mwanafunzi huyo alichukuliwa na kupelekwa kwenye nyumba maalumu sehemu ambako anapatiwa huduma za ushauri wa kisaikolojia na kuangalia namna ya kumrudisha shuleni.

“Baadaye tunatakiwa kufanya utaratibu asirudi katika shule aliyokuwa anasoma kwa ajili ya maendeleo yake,” alisema Mafole.

Katika tukio hilo, baba wa bibi harusi anadaiwa kukimbilia kusikojulikana huku mama anadaiwa alizimia na kupelekwa hospitali kupatiwa matibabu.

Binti huyo ambaye pia kiumbo ni mdogo, alisema anatamani kuwa daktari pindi atakapomaliza kusoma.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Temeke, Elihuruma Mabelya alisema chanzo cha binti huyo kukubali kuolewa ni migogoro ndani ya familia yake.

“Migogoro ya kifamilia ilimfanya aone yuko tayari kuolewa, licha ya kuwa anasema moyoni hakuwa tayari kuolewa ila alitaka kuondokana na ugumu wa maisha na migogoro hiyo. “Niwaombe wazazi, familia zetu ziwe na umoja, ili kuboresha ustawi wa maisha ya watoto wa kike,” alisema Mabelya. Alisema manispaa walijipanga kupitia kamati na hatimaye kuzuia ndoa hiyo isifungwe.

“Nikiwa mwenyekiti wa ulinzi wa mwanamke wa kamati, siko nyuma kuhakikisha haki za wanawake na watoto zinalindwa ipasavyo, ustawi wa jamii ni pamoja na kuhakikisha haki zao zinalindwa,” alisema.

Waziri Gwajima

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Dk Dorothy Gwajima aliagiza watu wote waliohusika wakamatwe, kwani kilichofanyika ni kosa kisheria kwa sababu inakatazwa kumuachisha mtoto shule kwa ajili ya kumuozesha.

“Wazazi, washenga, viongozi wa imani mbalimbali, mashuhuda waliokuwa wamevaa suti wameenda kwenye shughuli, wote wamekiuka sheria ya mtoto na sheria ya elimu ambayo inamtaka mtoto apate nafasi ya kuendelea na masomo,” alisema Dk Gwajima.

Alisema kutokujua sheria si sababu ya kutotii sheria, kwa kuwa hakuzuii hatua za kisheria kuchukuliwa dhidi yao.

Mfumo kutumika kudhibiti

Waziri Gwajima alisema ili kuhakikisha matukio ya ukatili yanashughulikiwa haraka, Serikali itaanzisha mfumo wa kitaifa utakaokuwa ukifuatilia kesi tangu siku zinazalishwa, kusajiliwa na zinashughulikiwaje hadi kufika mahakamani.

“Mhimili wa mahakama unajitegemea na mambo yake, ila huku kwenye jamii lazima tuzione kesi zinatembea, haiwezekani kesi izalishwe leo ikae miaka mitatu ndiyo ianze kushugulikiwa.

“Lazima kila mtu awajibike tuone kesi zinavyotembea na hili litawezesha wahusika wa upelelezi kuongea wanakabiliwa na changamoto gani,” alisema Waziri huyo.

Alisema ili kufanikisha hilo, wizara yake itazungumza na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, ili kujua changamoto zao na namna ya kuwawezesha kushughulikia kesi hizo kwa sababu wanashirikiana nao kwenye kila hatua ya kutokomeza ukatili nchini.

Hata hivyo, alitumia nafasi hiyo kueleza kuwa hivi sasa kutakuwa hakuna nafasi ya familia kutaka matukio ya ukatili yakamalizwe kifamilia, kwani kunaendelea kuchochea matukio hayo.

Mtoto mwingine alawitiwa

Wakati waziri alipomtembelea nyumba hiyo ambayo binti aliyenusurika kuolewa, alikumbana na tukio lingine la mtoto wa miaka minne aliyelawitiwa na baba yake mzazi na anaishi katika nyumba hiyo kwa mwezi mmoja sasa.

Mtoto huyo anatunzwa kwenye nyumba hiyo baada ya kuchukuliwa kutoka kwa baba yake baada ya wasamaria wema kuripoti tukio hilo.

Binti huyo alikuwa akiishi na baba yake baada ya mama yake kutengana na mumewe huyo.

“Hili nalo ni la kuangalia, mtoto huyu ni mdogo, alitakiwa kuwa mikononi kwa mama hadi afikie umri unaotakiwa, nani aliyekosea jukumu hapa hadi mtoto huyu akajikuta mikononi mwa baba,” alihoji Waziri Gwajima.

Alisema licha ya kesi hiyo kufikishwa mahakamani, ni vema wazazi wajue dunia haiko salama kwa kuwa ukatili hivi sasa hasa wa kingono unafanywa zaidi na watu wa familia.