Polisi adaiwa kuua kwa risasi

Muktasari:
- Kijana ambaye jina lake halijatambulika mkazi wa kijiji cha Bwira Juu kata ya Selembara wilaya ya Morogoro anadaiwa kuuawa kwa kupigwa risasi na polisi wa kituo cha polisi Dala.
Morogoro. Kijana ambaye jina lake halijatambulika mkazi wa kijiji cha Bwira Juu kata ya Selembara wilaya ya Morogoro anadaiwa kuuawa kwa kupigwa risasi na polisi wa kituo cha polisi Dala.
Inaelezwa kuwa askari huyo alikuwa amekwenda kumkamata kijana huyo nyumbani kwake baada ya mkewe kumshtaki polisi kuwa anataka kumdhulumu mazao ya ufuta waliyolima pamoja akitaka akamatwe ili wasuruhishwe.
Rehema Jango mkazi wa kata ya Mvuka akizungumza kwa njia ya simu na Mwananchi Digital amesema mwanamke huyo alilima ufuta na mumewe baada ya kuvuna kijana huyo alionyesha dalili za kutaka kumdhulumu mkewe na ulianza ugomvi.
Amesema alipoona hapati haki alikwenda kituo cha polisi Dala na kutoa taarifa, ndipo alipoondoka na askari kituoni hapo wakiwa na pikipiki.
“Polisi huyo alimfuata yule kijana nyumbani kwake akiwa na silaha na pikipiki na kumtaka waondoke wote lakini kijana aligoma baada ya mabishano ya muda mrefu polisi alimpiga risasi,”amesema Rehema.
Tukio hilo limetokea Mei 31, 2022 mchana lakini saa 11 jioni inadaiwa kijana huyo alikimbizwa hospitali kwa ajili ya kupatiwa matibabu na alifariki baadaye kutokana na kuvuja damu nyingi.
Akizungumzia tukio hilo mkuu wa Wilaya Morogoro, Albert Msando amesema, "ni kweli nimepata taarifa ya kuwepo kwa tukio hilo lakini naomba nipe muda ili nipate taarifa kamili kwani RCO na OCD wameenda huko wakirudi na kunipa taarifa nitakujulisha."