Padri Soka apangua kesi ya ubakaji, mahakama yamwachia huru

Muktasari:
- Padri Sosthenes Bahati Soka (42) aliyekuwa padri wa Kanisa Katoliki la Mt. Dionisi Aropagita, Kawawa, Wilaya ya Moshi amepangua kesi mbili kati ya tatu za ubakaji zilizokuwa zikimkabili katika mahakama ya hakimu mkazi Moshi na kuachiwa huru baada ya upande wa mashitaka kushindwa kudhibitisha mashtaka yaliyokuwa yakimkabili.
Moshi. Padri Sosthenes Bahati Soka (42) aliyekuwa padri wa Kanisa Katoliki la Mt. Dionisi Aropagita, Kawawa, Wilaya ya Moshi amepangua kesi mbili kati ya tatu za ubakaji zilizokuwa zikimkabili katika Mahakama ya Hakimu mkazi Moshi na kuachiwa huru, baada ya upande wa mashitaka kushindwa kudhibitisha mashitaka yaliyokuwa yakimkabili.
Padri Soka ameachiwa huru leo Septemba 25, 2023 na mahakama hiyo katika kesi namba 45 ya mwaka 2022 ya ubakaji wa mtoto wa miaka 12, mbele ya hakimu mkazi Mwandamizi wa mahakama hiyo, Herieth Mhenga ambaye alikuwa akisikiliza kesi hiyo.
Katika kesi ya kwanza namba 44 ya mwaka 2022 aliyoachiliwa nayo huru, Septemba 22, mwaka huu akikabiliwa na kosa la ubakaji na ulawiti wa mtoto wa miaka 12 upande wa mashitaka ulishindwa kudhibitisha shitaka hilo na kuachiwa huru.
Kesi ya pili aliyoachiwa nayo huru leo upande wa mashitaka umeshindwa kuthibitisha shitaka dhidi ya mtuhumiwa huyo na kumwachia huru ambapo Agosti 12, 2022 inadaiwa kuwa akiwa katika kanisa hilo alifanya mapenzi na mtoto wa miaka 12 bila ruhusa yake.
Padri Soka alikamatwa Septemba 20, 2022 na kufikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza Septemba 26 na kufunguliwa kesi tatu tofauti za kubaka watoto watatu.
Akitoa hukumu hiyo leo, Hakimu Mhenga ameeleza kuwa upande wa mashtaka umeshindwa kuthibitisha shtaka dhidi ya mtuhumiwa na kwamba kumekuwa na mashaka mengi kwa ushahidi wa upande wa mashitaka ambao umeshindwa kutolewa majibu na kutofautiana kwa maelezo ya mashahidi hivyo kupelekea ushahidi wao kutotiwa maanani na mahakama hiyo.
"Mshtakiwa aliieleza mahakama wakati tukio linatendeka hakuwepo eneo la tukio na upande wa mashtaka umeshindwa kupinga utetezi wa padri na kupelekea upande wa mahakama kuamini kuwa mshitakiwa hakuwepo eneo la tukio kama inavyodaiwa na upande wa mashtaka," amesema.
Hivyo kutokana na ushahidi huo mahakama imefikia uamuzi huo kwa kuona mshitakiwa hana hatia na kumwachia huru.
Hata hivyo, Hakimu Mhenga ameeleza kuwa kulikuwepo na mashahidi muhimu ambao upande wa mashtaka walitakiwa kuwaleta mahakamani lakini walishindwa kufanya hivyo na hawakueleza chochote mahakamani hapo ni kwanini mashahidi hao hawakwenda kutoa ushahidi.