Padri Kusekwa ‘awauma’ sikio viongozi wa kisiasa

Padri Albert Kusekwa wa Kanisa Katoliki Parokia ya Mtakatifu Theresia wa Mtoto Yesu akizungumza katika ibada ya jumapili ya matawi kanisani hapo.
Muktasari:
- Akihubiri katika Misa Takatifu ya Jumapili ya Matawi kanisani hapo leo Aprili 13, 2025, Padri Kusekwa amesema ipo haja kwa viongozi wa nyanja zote kuacha tabia ya kutafuta kumpendeza binadamu mmoja na kuwaacha wengi, badala yake wasimame kwenye misingi ya haki na uadilifu.
Geita. Padri Albert Kusekwa wa Kanisa Katoliki Parokia ya Mtakatifu Theresia wa Mtoto Yesu Jimbo Katoliki la Geita, amewataka viongozi wa kisiasa, kijamii na kidini kusimama imara katika kutetea ukweli bila kutaka kupendeza watu au kuogopa kupoteza umaarufu.
Akihubiri katika Misa Takatifu ya Jumapili ya Matawi kanisani hapo leo Aprili 13, 2025, Padri Kusekwa amesema ipo haja kwa viongozi wa nyanja zote kuacha tabia ya kutafuta kumpendeza binadamu mmoja na kuwaacha wengi, badala yake wasimame kwenye misingi ya haki na uadilifu.
“Hatupaswi kuogopa kusimamia ukweli kwa sababu ya kelele za watu. Misimamo ya kutetea ukweli hufifishwa kwa sababu ya nguvu za wengine, sio kila kinachosemwa na watu wengi kina kuwa cha kweli, tunapaswa kusimama kwenye ukweli bila kuogopa,”amesema Padri Kusekwa.
Amesema kuna wakati ukweli huzimwa ili kutetea waovu, huo ni wajibu wa viongozi au jamii kusimamia ukweli kwa kuwa hata kama dunia itajaa waongo, ipo siku ukweli utashinda.
“Hata kama waongo ni wengi anahitajika mtu mmoja wa kusema kweli, tukubali kubeba majukumu bila kusingizia wengine, tuwe wajumbe na watetezi wa kusimamia ukweli,”amesisitiza kiongozi huyo wa dini.

Aidha, ametolea mfano wa Yusufu katika Biblia aliyekataa kushiriki njama ya kumuua Yesu, akisisitiza kuwa ujasiri wa mtu mmoja unaweza kuokoa jamii nzima.
Misa hiyo Takatifu mbali na waumini, imehudhuriwa pia na viongozi wa Jeshi la Polisi waliokuwa wakitoa elimu ya polisi jamii ikiwa ni sehemu ya mafunzo ya ulinzi shirikishi yaliyoandaliwa na jeshi hilo kwa kushirikiana na mgodi wa dhahabu wa Geita (GGML) kwa lengo la kuimarisha usalama wa wananchi.
Akizungumza baada ya Misa hiyo, Mkuu wa Dawati la Jinsia na Watoto Mkoa wa Geita, Grace Kaijage, amewataka wazazi kuwa makini na mazingira wanayowaweka watoto wao.
"Utafiti na taarifa zetu zinaonesha kuwa matukio mengi ya ukatili dhidi ya watoto yanatokea majumbani na wahusika wakuu mara nyingi ni watu wa karibu kabisa wa familia," amesema Kaijage.
Kaijage amesema tafiti zinaonyesha kuwa baadhi ya matukio hayo hutekelezwa na watoto dhidi ya wenzao, hivyo ni wajibu wa kila mzazi kuhakikisha watoto wote wa kike na wa kiume wanalindwa na kulelewa katika mazingira salama.
Kwa upande wake, Dk Ezekiel Kyogo kutoka Kitengo cha Ushirikishwaji wa Jamii Makao Makuu ya Polisi, ametoa wito kwa wananchi kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama kwa manufaa ya jamii nzima.
"Polisi jamii inamaanisha ushirikiano wa karibu kati ya raia na polisi. Hakuna maendeleo yanayowezekana bila usalama. Hivyo basi, ni wajibu wetu wote kushiriki kulinda amani ya maeneo yetu," amesema Dk Kyogo
Charles Masanyiwa mkazi wa Ibolelo amesema elimu ya ulinzi shirikishi inayoptolewa na jeshi hilo inawasaidia kujua wapi pa kupeleka changamoto zao pindi wanapofanyiwa ukatili, lakini pia elimu hiyo inawasaidia wazazi kujua namna ya kuwalea watoto na kuwaepusha na vitendo vya ukatili kama ubakaji na ulawiti.