Prime
Hatima ya Chadema kutoshiriki uchaguzi

Dar/Mikoani. Suala linalogonga vichwa na kutawala mijadala ya kisiasa kwa sasa ni tangazo la Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) kuwa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) hakitashiriki Uchaguzi Mkuu wa Oktoba na nyingine ndogo zitakazofanyika ndani ya miaka mitano, baada ya kutosaini Kanuni za Maadili ya Uchaguzi.
Kati ya vyama 19 vyenye usajili wa kudumu nchini, Chadema pekee haijasaini kanuni hizo huku vingine 18, INEC na Serikali vikizisaini, fursa ambayo tume hiyo ilieleza ilikuwa inapatikana jana pekee na kuwa waliosaini ndio watashiriki uchaguzi mkuu wa Rais, wabunge na madiwani wa baadaye mwaka huu.
Hata hivyo, kumekuwa na mitazamo tofauti juu ya fursa hiyo kupatikana kwa upekee jana, ikielezwa miaka ya nyuma, chama kingeweza kusaini wakati wowote kabla ya uteuzi wa wagombea.
Aprili 4, 2025 INEC ilituma mialiko kwa makatibu wakuu wa vyama vya siasa na Serikali kukutana jijini Dodoma jana kujadiliana na kusaini kanuni hizo za maadili.
Vyama vilivyoitika wito na makatibu wakuu wake kusaini ni ADC, Demokrasia Makini, DP, NRA, NLD, SAU, UDPD, ADA-Tadea, AAFP, CCM, CUF, ACT-Wazalendo, Chaumma, UMD, TLP, NCCR-Mageuzi, CCK na UDP.
Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika mapema jana alieleza kwamba asingeenda na hajatuma mwakilishi kwenda kusaini kanuni hizo.
Mnyika kupitia mtandao wa kijamii wa X na baadaye katika mazungumzo kwa simu na Mwananchi, alieleza msimamo huo:
“Ni vema mkaandika kwamba sijakwenda wala sijateua mtu. Habari kubwa sasa hivi ni katibu mkuu sitakwenda kusaini wala sijateua mtu."
Msimamo huo, ulisisitizwa na Makamu Mwenyekiti wa Chadema (Bara), John Heche ambaye pia aliandika ujumbe kupitia mtandao wa X kuwa chama hicho hakitasaini kanuni za maadili ya uchaguzi.
Msimamo wa viongozi hao unaendana na ajenda ya Chadema ya No reforms, no election ambayo chama hicho kimeshaweka wazi kwamba, kama hakutakuwa na mabadiliko ya mifumo na sheria za uchaguzi, hakutakuwa na uchaguzi.
Kupitia operesheni zake, Chadema imekuwa ikienda kwa wananchi kufikisha ujumbe huo wa kuishinikiza Serikali kufanya mabadiliko ya mfumo wa uchaguzi nchini.
Operesheni ya kunadi ajenda ya No reforms ilianza Machi 23, 2025 katika mikoa ya Iringa, Njombe, Mbeya, Songwe na Rukwa, kabla ya kuhamia Lindi, Mtwara na Ruvuma.
Chama hicho kikiwa mkoani Ruvuma Aprili 10, ili kuhitimisha mikutano yake, Jeshi la Polisi lilimtia mbaroni Mwenyekiti wa chama hicho, Tundu Lissu kutokana na kauli alizozitoa kwenye operesheni hiyo, kisha likasitisha kibali cha kuendelea kwa mikutano mkoani Ruvuma, na sasa Chadema inapitia upya ratiba kabla ya kuendelea.
Kwa mujibu wa INEC, kanuni za maadili zimeandaliwa kwa mujibu wa kifungu cha 162 (1), (2) na (3) cha Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani Na. 1 ya Mwaka 2024, ambacho kinaitaka Tume baada ya kushauriana na vyama vyote vya siasa na Serikali, kuandaa na kuchapisha katika Gazeti la Serikali Kanuni za Maadili ya Uchaguzi zitakazoainisha maadili ya vyama vya siasa, Serikali na Tume wakati wa kampeni za uchaguzi na uchaguzi na utaratibu wa utekelezaji wake.
Kifungu hicho kinaelekeza kanuni za maadili zitasainiwa na kila chama cha siasa, kila mgombea kabla hajawasilisha fomu ya uteuzi, Serikali na Tume na zitapaswa kuzingatiwa na wahusika wote waliosaini.
Baada ya shughuli hiyo, Mkurugenzi wa Uchaguzi wa INEC, Ramadhani Kailima alisema: “Chama cha Chadema ambacho hakikusaini kanuni za maadili ya uchaguzi wa Rais, wabunge na madiwani za mwaka 2025, hakitashiri uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba mwaka huu na chaguzi zote ndogo zitakazofuata kwa muda wa miaka mitano.”
"Utaratibu wa kusaini kanuni hizi ni leo tu, hakutakuwa na siku nyingine. Kwa maana hiyo chama ambacho hakijasaini hakitaweza kushiriki uchaguzi na chaguzi nyingine ndogo zitakazofuata katika kipindi cha miaka mitano, kwa sababu kanuni hizi uhai wake ni ndani ya miaka mitano kuanzia uchaguzi mkuu huu," alisema.
Wakati Kailima akisema hivyo, mwanasheria John Mallya ambaye pia ni kada wa Chadema alisema anavyojua yeye kanuni hizo si lazima zisainiwe mara moja, labda kama kuna mabadiliko.
"Ninavyokumbuka fomu hizo zinatakiwa chama kisaini kabla ya uteuzi wa wagombea haujatangazwa. Mwaka 2015 Chadema ilichelewa kusaini, baadaye ikazisaini.
"Huenda utaratibu wa kuzisaini umewekwa mwaka huu, ninachojua daftari lilikuwa linawekwa wazi na muda wowote unasaini," alisema.
Maoni ya Mallya yanarandana na ya mwanasheria Jebra Kambole, aliyesema sheria haikuweka ukomo wa muda wa kusaini kanuni za maadili ya uchaguzi na hivyo wakati wowote chama au mgombea anaweza kusaini.
“Hakuna ukomo wa kusaini kanuni za maadili. Chama au mgombea atasaini muda wowote,” alisema na kufafanua kuwa, uchaguzi unasimamiwa na Katiba na siyo kanuni, hivyo hakuna uwezekano wa chama au mgombea kukosa haki ya kushiriki mchakato huo kwa sababu za kikanuni.
Msimamo utawagharimu
Mchambuzi wa siasa, Dk Onesmo Kyauke alisema uamuzi wa Chadema kususia uchaguzi utawagharimu katika siku za usoni na hivyo hakioni chama hicho kikiendelea kuwa kikuu cha upinzani.
Alisema INEC haina makosa kwa sababu ilitangaza na kuviita vyama vyote kusaini nyaraka, lakini Chadema imekacha.
Dk Kyauke ambaye pia ni mwanasheria, alisema kitakachotokea siku zijazo ni wagombea wa chama hicho kuhamia vyama vingine ili kutimiza ndoto za kuwania udiwani au ubunge.
“Chadema kitakosa ushawishi, ruzuku na kitakufa, wasiposhiriki watasahaulika, hawatakuwa na jukwaa. Watu wengi ndani ya Chadema walishajiandaa na ubunge, hawatakubali kukaa nyuma, bali watatafuta jukwaa mbadala.
“Nilidhani Chadema wangeshiriki huku wakiendelea kupiga kelele kuhusu ajenda yao, lakini si kususia uchaguzi. Chadema wamefanya uamuzi mbovu wa kususia uchaguzi,” alisema.
Kada wa Chadema, Julius Mwita alisema amesikitishwa na taarifa ya INEC kwamba chama hicho kikuu cha upinzani hakitashiriki uchaguzi mkuu utakaofanyika baadaye mwaka huu.
“Watanzania wanaiunga mkono Chadema kwa sababu ndiyo jukwaa la matumaini la kusemea kero zinazowakabili, lakini kwa sasa itawazilazimu kuhamia vyama vingine ili kupeleka changamoto zao.
“Nimeumia kusikia taarifa ya INEC inayohusu chama changu, naamini uamuzi wa Chadema kutokwenda kusaini kanuni haujafanywa na kamati kuu au mkutano mkuu,” alisema.
Hata hivyo, Makamu Mwenyekiti mstaafu wa Chadema (Zanzibar), Said Issa Mohamed licha ya kusema chama hicho kimepokea taarifa hizo, alisema huenda kikakaa kutafakari ili kuchukua hatua mahususi ama kuingia katika uchaguzi au kutoingia.
“Matamshi kama hayo yanakuja na hizo sheria zipo, wakati mwingine sheria zinakwenda na kubadilika kwa mazungumzo au maridhiano. Lakini tamko la moja kwa moja kwamba Chadema haishiriki si rahisi hivyo.
“Chadema tumeipata taarifa hiyo kwa mshtuko kwa sababu tu chama hakijaenda kusaini,” alisema.