Prime
Nyuma ya pazia mbio za wajawazito Korogwe

Mkuu wa Wilaya ya Korogwe, Jokate Mwegelo akizungumza wakati wa mahojiano maalumu na waandishi wa kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) ofisini kwake. Picha na Elizabeth Edward
Korogwe. Mkuu wa Wilaya ya Korogwe, Jokate Mwegelo amefichua kilichomsukuma kuanzisha mbio na matembezi ya wajawazito.
Pia amesema baada ya kupata mwitikio chanya katika mbio hizo zilizofanyika wilayani humo, upo mpango wa programu hiyo kufanyika kitaifa.
Waswahili husema aisifuye mvua imemnyea, na hivi ndivyo ilivyokuwa kwa Jokate, aliyesema alifikia uamuzi wa kuandaa mbio na matembezi hayo, baada ya yale aliyopitia akiwa mjamzito.
“Nilipopata ujauzito ndiyo niligundua kuwa wanawake wanapitia vitu vingi, mtu hadi kuitwa mama kuna mengi anayapitia. Nikagundua umuhimu wa kuwa na taarifa sahihi kuhusu uzazi, kufuatilia ujauzito na kujifungua.

“Naamini ukipitia kitu fulani kama unaweza kuwa na mchango wa kubadilisha basi tumia fursa hiyo kusaidia wengine. “Nikashauriana na watu wangu wa karibu tukaona ni jambo zuri la kufanya.”
Alisema alifurahi kufanikisha jambo hilo kwa sababu ni mara ya kwanza kufanyika Tanzania na ataangalia jinsi ya kufanya ili lifike katika maeneo mengine.
“Ni programu ninayotarajia kuindeleza na haitaishia Korogwe, mpango ni kuifanya kitaifa,” alisema Jokate.
Mkuu huyo wa wilaya ambaye kwa sasa ni mama akizungumza katika mahojiano maalumu aliyofanya na gazeti hili ofisini kwake, alisema amebaini kuwa wakati mwingine wanawake wa pembezoni hawafikiwi na elimu ya uzazi salama, na kujikuta wakiweka maisha yao hatarini pale wanapokuwa wajawazito.
Alisema: “Hili suala la uzazi salama bado lina changamoto, kuna wengine hawapati taarifa kabisa, hawaendi kliniki hivyo hawapati elimu sahihi.
“Hata kwa watoa huduma nako kuna changamoto, inawezekana anahitaji kumsaidia mjamzito lakini hana vifaa, ndiyo maana naona kuna haja ya kuweka nguvu katika eneo hilo kuhakikisha mama ana uhakika wa vifaa vya kujifungulia.
Mbio hizo za wajawazito zilifanyika Mei 28, mwaka huu zikilenga kuhamasisha elimu ya uzazi kwa wajawazito kwa kuwawezesha kujifungua salama na hatimaye kupunguza vifo vinavyotokana na uzazi.
Zaidi ya wanawake 2,000 walishiriki kwenye matembezi na mbio hizo zilizowezesha wajawazito zaidi ya 1,000 kupata vifaa vya kujifungulia na elimu ya lishe na uzazi, ambayo ni nadra kuipata hasa kwa wanawake waishio pembezoni.
Jokate alieleza kipindi cha ujauzito mama anatakiwa kuzingatia lishe bora na mazoezi kama kichocheo cha kujifungua salama, na kuwezesha mpango wa Serikali wa kupunguza vifo vya wajawazito na watoto wachanga.
Kwa sasa Tanzania inatekeleza Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa 2021/2022 – 2025/2026 wa kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi kutoka vifo 321 kwa kila vizazi hai 100,000 hadi kufikia vifo 220.
Julai 2022 akizindua jengo la huduma ya afya ya mama na mtoto katika Hospitali ya CCBRT, Rais Samia Suluhu Hassan alisema Serikali itaendelea kuwekeza zaidi katika kutoa huduma za dharura na kupunguza vifo vinavyotokana na uzazi kwa kina mama na watoto wachanga. Alisema ni muhimu kwa mjamzito kupatiwa huduma bora ya uzazi tangu ujauzito, kujifungua na baadaye uangalizi kwa mzazi na mtoto mchanga.
Naye Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake CCM (UWT), Mary Chatanda ambaye alikuwa mgeni rasmi kwenye mbio hizo alipongeza ubunifu huo unaolenga kugusa afya ya wajawazito na watoto wachanga.
Endelea kufuatilia mahojiano maalumu na Mkuu wa Wilaya ya Korogwe kupitia mitandao yetu ya kijamii na tovuti yetu.