Nyara za Serikali zampeleka jela miaka 20

Muktasari:
Hakimu Mkazi Mfawidhi, Chiganga Ntengwa alitoa hukumu hiyo baada ya Mahakama kuridhishwa na ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka uliokuwa na mashahidi saba.
Mahakama ya Wilaya ya Mpanda mkoani Katavi imemhukumu kifungo cha miaka 20 jela, mkazi wa Kijiji cha Kanoge, Robert Nakie (44) kwa kosa la kupatikana na meno ya tembo yenye thamani ya Sh120 milioni.
Hakimu Mkazi Mfawidhi, Chiganga Ntengwa alitoa hukumu hiyo baada ya Mahakama kuridhishwa na ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka uliokuwa na mashahidi saba.
Awali, Wakili wa Serikali, Jamira Mziray alidai mshtakiwa alitenda kosa hilo Oktoba 21, 2016 katika Kijiji cha Kanoge.
Mziray alidai siku ya tukio mshtakiwa alikamatwa na askari wa Hifadhi ya Taifa Katavi akiwa na vipande 11 vya meno ya tembo yenye thamani ya Sh120 milioni alivyokuwa amevipakia kwenye pikipiki kwa lengo la kwenda kuviuza.
Alidai, awali askari wa hifadhi hiyo walipata taarifa za siri kuwa mshtakiwa Nakie anamiliki nyara hizo za Serikali kinyume na sheria ndipo walipoandaa mtego na kumtia mbaroni. Kabla ya kutoa adhabu, Hakimu Ntengwa alisema ushahidi uliotolewa mahakamani, upande wa mashtaka ulikuwa na mashahidi watano na upande wa utetezi haukuwa na shahidi zaidi ya mshtakiwa.
Akijitetea kabla ya hukumu ili kuishaiwshi Mahakama impunguzie adhabu, mshtakiwa alidai ana familia inayomtegemea.
Hata hivyo, Wakili Mziray alidai kama anajua ana familia inayomtegemea asingejihusisha na nyara za Serikali bila kibali.
Aliiomba Mahakama itoe adhabu kali kwa mshtakiwa.