Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

NHIF yajibu wadau, yakaribisha maoni

Dar es Salaam. Wakati maboresho ya kitita cha mafao cha Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) yakitarajia kuanza Januari mwakani, mfuko huo umesema wadau wote walishirikishwa na bado milango ipo wazi ya kupokea maoni, ushauri ili kuboresha utoaji huduma kwa wananchi.

Kufuatia wito huo, Rais wa Chama cha Madaktari (MAT), Dk Deusdedit Ndilanha alisema tayari juzi walifanya mazungumzo na NHIF na leo watarudi pia kufanya mazungumzo kuhusu maboresho hayo.

"Juzi tulikwenda kukafanya nao mazungumzo na tutarudi tena leo (jana), lengo ni kuboresha huduma," alisema Dk Ndilanha. Awali, MAT walisema hawakuwa wameshirikishwa kwenye maboresho hayo.

MAT na Chama cha Watoa Huduma za Afya Binafsi Tanzania (Aphta) walilalamika kushushwa kwa ada ya ushauri wa daktari na kupunguzwa kwa bei ya baadhi ya dawa wakidai hawakushirikishwa.

Jumatatu ya wiki hii watendaji wa NHIF walikutana na wadau mbalimbali, wakiwamo wahariri na waandishi wa habari na kubainisha maboresho hayo ambayo yaliwaibua MAT na Aphta kutoa mitazamo hiyo.

 

Ufafanuzi wa NHIF

Juzi, Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Bernard Konga alifanya mahojiano maalumu na gazeti hili kuhusu masuala mbalimbali, ukiwamo ushirikishwaji wa wadau, akisema maboresho yaliyofanyika yanalenga kuongeza na kupunguza gharama katika baadhi ya huduma ili kuendana na soko na kwamba maboresho yalianza tangu 2020 huku wadau wote wakishirikishwa.

“Tulifanya tathmini maeneo yenye uhitaji wa maboresho, sasa yale ambayo tulitaka kufanyia mabadiliko yanagusa watu, hivyo tuliita wataalamu, wakiwemo wamiliki wa vituo vya afya sekta binafsi, vyama vya kitaaluma, pia tumekaa na hospitali za Serikali na waganga wafawidhi wote tuliwashirikisha,” alisema.

Konga alisema baada ushirikishwaji kukamilika, walianza kutoa taarifa Agosti mwaka jana, hivyo tangu wakati huo waliingia kwenye majadiliano na wadau hao hadi mwaka huu walipotangaza kuanza utekelezaji.

Mkurugenzi mkuu huyo alisema mabadiliko yaliyofanyika yatakwenda kuimarisha utoaji wa huduma nchini, hasa huduma ya afya ya msingi na za kibingwa.
Kuhusu mabadiliko ya kitita cha mafao, alisema yalifanyika mwaka 2016, huku mwaka 2019 yakifanyika mabadiliko kidogo, hivyo ilikuwa lazima 2023 wafanye mabadiliko mengine.

“Miaka saba ya kutofanya mabadiliko kwenye kitita cha mafao, kumetufanya kugundua mengi hivyo tutakuwa tunafanya mabadiliko mara kwa mara,” alisema.
Aliwaondoa hofu wadau kuhusu mabadiliko hayo, akiahidi kufanya kazi maeneo ya upungufu yatakayobainika.

Alisisitiza mabadiliko yaliyofanyika hayatadumaza sekta ya afya:
“Tunakwenda kuboresha sekta ya dawa na watoa huduma watanunua na kuuza dawa, tumeangalia uhitaji, bei ya soko na miongozo, huenda kilichopo sasa ndicho kinadumaza,’’ alieleza.

Ufafanuzi huo ulitokana na kile kilichokuwa kimeelezwa na Mwenyekiti wa Aphta, Dk Egina Makwabe kuwa mabadiliko hayo hayachochei ukuaji wa vituo vya afya binafsi.

“Itakuwa ni vigumu kuendesha kituo cha afya na vigumu kituo cha afya kukua kwa bei hizo za NHIF, tumekaa vikao vingi lakini hatujakubaliana,” alisema Makwabe.
 

Mjadala wa dawa

Kwenye huduma za dawa, Konga alisema mwaka 2021 kulitolewa mwongozo na NHIF kuchelewa kufanyia maboresho, hivyo kujikuta ndani ya mwongozo kuna dawa ambazo hazipo kwenye kitita. “Dawa 124 tumezijumuisha kwenye kitita cha mafao ili zikatoe ahueni na kuongeza ukubwa wa kitita katika utoaji wa huduma, tumezihuisha bidhaa za dawa 374 ambazo zimeongezewa bei kwa wastani wa asilimia 10 hadi 20,” alisema.

Konga alisema kuna maeneo dawa walikuwa wakilipa kwa gharama ndogo, lakini sasa watalipa kulingana na bei ya soko.
Alisema zipo dawa wamepunguza bei, kwani kadiri wanasayansi wanavyovumbua dawa bei inashuka.

Pia alisema kwa kadiri watu wanavyotengeneza dawa nyingi, ndivyo bei inavyozidi kushuka.

 

Ada ya daktari kupungua

Kuhusu eneo linalolalamikiwa na MAT la viwango vya kumuona daktari, Konga alisema kwenye eneo hilo walipokea malalamiko ya viwango vinavyolipwa kutokuwa na taswira nzuri kwa daktari.

“Kulikuwa na tofauti za malipo kati ya daktari anayefanya kazi hospitali ngazi ya taifa hadi mkoa, jambo lililoibua malalamiko ya muda mrefu.

“Mapendekezo yalikuwa ni kuweka kima sawa cha fedha hizo, jambo ambalo tulilizingatia kwa kuweka mzani sawa kwa aliye juu kushuka chini na aliye chini sana kupanda,” alisema.

Alisisitiza fedha wanazolipa kama ada ya ushauri kutoka kwa daktari yasitafsiriwa kama ndio thamani ya daktari, bali shukrani kwa mtaalamu huyo kumuona mwanachama wa NHIF.

Alisema thamani ya daktari haiwezi kufananishwa kwa Sh20,000 au Sh15,000 zinazolipwa, akirejea ugumu wa masomo ya fani hiyo ambao alisema huwezi kuulinganisha na malipo hayo.

“Kwa hali ya mfuko sasa, ndio tumeona ndicho tunaweza kulipa. Kadiri siku zinavyokwenda na sasa tunapoingia kwenye mfumo wa Bima ya Afya kwa Wote, tutazidi kuboresha viwango hivi zaidi,” alisema.

Katika mabadiliko ya ada ya usajili na ushauri wa daktari, viwango vya mgonjwa kumuona daktari Hospitali ya Taifa vimeshushwa hadi Sh25,000 kutoka Sh35,000 kwa daktari bingwa mbobezi, na Sh20,000 kutoka Sh 25,000 kwa daktari bingwa.

Mabadiliko mengine ni kwenye hospitali ya rufaa ya kanda ambapo kumuona daktari bingwa mbobezi ni Sh25,000 kutoka Sh35,000 na kumuona daktari bingwa ni Sh20,000 kutoka Sh25,000

Hospitali ya mkoa, gharama zimepanda ambapo kumuona daktari bingwa mbobezi ni Sh25,000 kutoka Sh15,000 na kwa daktari bingwa ni Sh20,000 kutoka Sh15,000.