Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ngono zembe tishio kwa ustawi wa vijana nchini

Muktasari:

Tangu akiwa na miaka 15, kijana huyo anasema alianza kushiriki ngono isiyo salama.

“Nimewahi kuwa na uhusiano wa kimapenzi na wasichana watatu, mmoja nilikuwa nasoma naye na wawili wa mtaani kwetu. Sijawahi kutumia kondom hata siku moja nilipofanya nao ngono kwa sababu niliwaamini.”

Ndivyo mtoto mwenye umri wa miaka 17 (jina linahifadhiwa) mwanafunzi wa Kidato cha Tatu katika moja ya shule za sekondari za jijini Dar es Salaam alivyoanza kuzungumza na Mwananchi kuhusu maambukizi mapya ya Virusi vya Ukimwi na Ukimwi na namna anavyojilinda.

Kijana huyo anasema imani yake kwa wasichana hao kwamba hawatakuwa na maambukizi ndiyo iliyomfanya awaamini na kufanya nao mapenzi.

Tangu akiwa na miaka 15, kijana huyo anasema alianza kushiriki ngono isiyo salama.

“Ilitokea tu amekuja kusoma kwenye chumba changu, basi hakurudi kwao nikajikuta nipo nao. Sikupanga kufanya nao mapenzi, ilitokea tu,”anasema.

Anasema hajawahi kupewa elimu ya kutosha kuhusu ukimwi japo anajua unaambukizwa zaidi kwa kushiriki ngono isiyo salama.

Zaidi ya kusoma mbao za matangazo, vipeperushi na kusikiliza vyombo vya habari hajawahi kupata mahali pengine elimu hiyo, hii ni kwa mujibu wake.

Msichana (jina linahifadhiwa), anayeishi na VVU anasema kwa sababu wenzake hawajui kama ameambukizwa au laa, mara kadhaa amepata usumbufu kutoka kwa wavulana, wengi wakimtaka afanye nao mapenzi bila kutumia kondom. “Huwa nawakatalia lakini wananilazimisha. Binafsi sijawahi kukubali najijali na ninawajali wao, lakini kama nikikubali wengi nitawaambukiza kwa kuwa afya yangu ni njema hakuna anayejua hali yangu,” anasema.

Sio hao tu. Vijana rika wengi wanafanya ngono bila kinga wakiamini wako salama.

Wapo walioambukizwa VVU baada ya kufanyiwa ukatili ikiwamo ubakaji na ulawiti, wengine kutoka kwa wazazi wao kabla au baada ya kuzaliwa na wapo walioambukizana wao kwa wao kwa kufanya ngono zembe.

Takwimu zinaonyesha vijana wa chini ya miaka 24 na watoto wadogo ndiyo wanaoongoza kwa kupata maambukizi ya virusi vya Ukimwi (VVU), duniani.

Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia masuala ya ukimwi (Unaids) hivi karibuni lilitoa takwimu zinazoonyesha asilimia 40 ya maambukizi mapya ya VVU na Ukwimwi duniani yanatokana na vijana wenye miaka 15 hadi 24.

Pia, zinaonyesha asilimia mbili ya maambukizi mapya ya virusi hivyo kwa hapa nchini yapo miongoni mwa vijana hao.

Anasema pia idadi kubwa ya vijana wamepata maambukizi hayo kwa wazazi wao tangu wakiwa tumboni na hivyo wanapozaliwa wanakuwa tayari na maambukizi.

Mtaalamu wa masuala ya kuzuia maambukizi ya Virusi vya Ukimwi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto kutoka Shirika la Afya Duniani (Unicef), Hafsa Khalfani anasema takwimu za kidunia zinaonyesha asilimia tano ya vijana rika wanaoishi na VVU duniani wapo Tanzania.

Katika mafunzo ya uandishi wa habari za watoto yaliyoendeshwa na Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) na kwa ufadhili wa Unicef, Khalfan alisema upo umuhimu wa kuendelea kutoa elimu kwa watoto na vijana kuhusu ukimwi.

Kijana Ephrahim Joseph (21), mkazi wa Mabibo Dar es Salaam, anasema alienda kupima baada ya kupata mafunzo kuhusu maambukizi hayo, jambo lililomfanya awe makini tangu hapo.

“Nilipita kwenye njia nyingi hivyo nilipopewa mafunzo nikaamua kwenda kupima. Niliogopa sana wakati wa kupokea majibu kwa sababu nimepita njia nyingi, nashukuru ni mzima hivyo nimejifunza,” anasema.

Kijana huyo anasema kitakachoweza kuepusha maambukizi mapya ni elimu ya ukimwi kwa vijana na watoto hasa wanaoanza kuingia kwenye umri wa kukua.

Wazazi wazungumza

“Hatukuwahi kumwambia kama anaishi na VVU, siku zote tulimpa dawa tukimwambia anaumwa ‘tonses’ aliamini hivyo hadi alipomaliza darasa la saba,” anasema mzazi ambaye binti yake anaishi na VVU.

Kilicho mfanya asimwambia anasema ni hofu, alidhani huenda angeshtuka na kushindwa kuendelea na masomo.

Anasema muda wa kwenda kusoma sekondari ulipofika huku akitakiwa kwenda kukaa bweni nje ya Dar es Salaam, walilazimika kumueleza kusudi afahamu hali ya afya yake.

“Ilikuwa kazi kubwa kumwambia ukweli, kabla sijasema naye, nililia kwanza kwa sababu nilijihukumu kwa kumkosesha furaha,” anasema mama yake.

Cha ajabu alipoanza kumwambia, binti yake alimjibu kwamba anafahamu jambo hilo, japo naye hakutaka kumwambia mama yake kwa kuwa alijua anamdanganya.

“Kumbe akiwa kliniki, alimuuliza muuguzi ambaye alikaa naye chemba akamweleza kuhusu afya yake. Alielewa na hakupata shida. Niliumia zaidi. Ilibidi nimuombe msamaha,” anaeleza mama huyo.

Hata hivyo, anasema kuna haja ya wazazi kuvunja ukimya na kuwaeleza watoto wao kuhusu afya ya ukimwi na uzazi kwa sababu, ni rahisi kuambukizana wasipojijua.

“Najuta kutozungumza na mwanangu kumueleza ukweli, wazazi lazima tuvunje ukimya,” anasisitiza mama huyo.

Mzazi mwingine, Jackline Joseph anasema wanawe wanaelewa kuhusu ukiwmi kwa sababu mara nyingi huzungumza nao kuhusu athari ya maradhi hayo.

Nini kinafanyike

Ripoti ya Unicef iliyotolewa mwishoni mwa 2016, inapendekeza kuongeza mikakati ya kuzuia VVU miongoni mwa vijana na kutibu wale ambao tayari wameanza kuugua.

Ripoti hiyo inasema ipo haja ya kuwekeza katika kuimarisha ukusanyaji wa takwimu, kutokomeza ubaguzi na unyanyasaji wa kijinsia sambamba na elimu kwa vijana

Mkuu wa Wilaya ya Mafia, Shaibu Anunduma anasema moja ya jitihada za wilaya hiyo ni kutoa elimu kwa makundi yote, huku vijana wakipewa kipaumbele.

“Tumejitahidi kupambana na maambukizi mapya ya VVU kwa kutoa elimu kwa jamii ili kuhakikisha wanaacha tabia zinazochangia maambuizi hasa vijana,” anasema mkuu huyo wa wilaya.

Matokeo ya elimu hiyo yamekuwa mazuri kwani mwaka 2015, maambukizi yalikuwa asilimia 3.2 lakini mwaka jana yalipungua hadi asilimia mbili.

Mkuu wa Wilaya ya Kilolo, Asia Abdalah anasema mkakati wa wilaya hiyo ni kuhakikisha kila linapokutana kundi lolote kwa sababu yoyote, suala la ukimwi na namna ya kujilinda lazima lizungumzwe.

“Ukatili wa kijinsia ni hatari kwenye masuala ya ukimwi, kwa hiyo wilayani kwangu nimetoa wito kwa wasichana wote wenye umri wa kwenda shule wapelekwe. Hawatakuwa na muda wa kujiingiza kwenye ngono, watawekeza kwenye elimu,” anasema Abdalah.

Katika hotuba yake ya Bajeti ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa mwaka wa fedha 2017/2018, Waziri wa wizara hiyo, Ummy Mwalimu alisema wanaendelea kudhibiti Ukimwi kwa kutoa ushauri, kupima na kutoa dawa za kufubaza virusi (ARV) kwa wale wenye maambukizi.

Kuanzia Januari hadi Desemba mwaka jana, zaidi ya wateja wapya milioni 7.4 walipata ushauri na kupima VVU.

Anasema Oktoba mwaka jana, Serikali ilianza kutoa dawa za ARV kwa watu wenye maambukizi ya Virusi vya Ukimwi bila kujali kiwango cha CD4.

Anasema watu wanaotumia dawa hizo hadi sasa ni ni 849,594 sawa na asilimia 60 ya watu million 1.4 wanaokadiriwa kuwa na maambukizi ya VVU nchini.

Waziri Ummy katika hotuba hiyo alisema kati ya hao, watoto 55,670 wako kwenye matibabu ya ARV.

Hata hivyo anasema Serikali inaendelea kutekeleza afua ya tohara kwa wanaume kama mojawapo ya njia za kupambana na maambukizi ya VVU.