Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ngono ‘muwawana’ kiini maambukizi mapya kwa vijana

Muktasari:

Zikiwa zimesalia siku nne kabla ya kilele cha maadhimisho ya siku ya ukimwi duniani, inaelezwa kuwa uhusiano wa kimapenzi usio wa ndoa, wala wa kibiashara unaochochewa na dhana ya wazi kwamba ngono itabadilishwa kwa usaidizi wa mali au manufaa mengine almaarufu ngono muwawana, unazidi kujengeka miongoni mwa vijana.

  

Dar es Salaam. Zikiwa zimesalia siku nne kabla ya kilele cha maadhimisho ya siku ya ukimwi duniani, inaelezwa kuwa uhusiano wa kimapenzi usio wa ndoa, wala wa kibiashara unaochochewa na dhana ya wazi kwamba ngono itabadilishwa kwa usaidizi wa mali au manufaa mengine almaarufu ngono muwawana, unazidi kujengeka miongoni mwa vijana.

Ngono muwawana ‘transactional sex’ imekuwa miongoni mwa maisha ya vijana wengi, hasa wa kike ambao wamejitofautisha na wale wanaofanya tendo hilo kama biashara.

Utofauti wao, hawa wamekuwa na wapenzi zaidi ya mmoja kwa ajili ya kujikimu kimaisha, kimasomo na kifedha ikilinganishwa na wale waliojipambanua kama wafanyabiashara za ngono wanaojiuza maeneo mbalimbali.

Selina (21) msichana anayesoma mojawapo ya chuo kikuu jijini Dar es Salaam ni miongoni mwa wasichana wadogo walio hatarini kupata maambukizi ya virusi vya Ukimwi (VVU) kutokana na kujihusisha kimapenzi na wanaume watatu tofauti.

Alipohojiwa na Mwananchi, Selina alisema ni maisha ya kawaida, kwani wasichana wenzake wengi wanafanya hivyo.

“Nipo mwaka wa pili chuoni. Mwanamume wangu wa kwanza alikuwa ni rafiki wa kiume ambaye tumekutana hapa, yeye tuna malengo ya kimaisha. Lakini baadaye nikapata mmoja wa wakufunzi ambaye niliona ni heri nimkubali ili niweze kupata ahueni kimasomo, chuoni kuna mambo mengi, usipokuwa makini unafeli kila siku.

“Katika zunguka zunguka yangu na wenzangu nikapata mpenzi mwingine, yeye ananiwezesha mno kiuchumi, hivyo naona naye siwezi kumuacha, maisha chuoni ni magumu,” Selina alisimulia namna alivyonasa katika mtego wa ngono muwawana.

Huyu anawakilisha mabinti wengi ambao wanapambana namna gani wataweza kutoka katika mtego huo, lakini wengi hawajui kama wapo katika aina hiyo ya mahusiano.

“Nina mpenzi anayenilipia kodi ya nyumba, lakini yeye yupo bize na familia yake, mwingine amenifungulia biashara, naye ni hivyo hivyo, mwingine mahusiano yanaanza na kuvunjika kila siku, lakini kiukweli nilimpata mwanaume ambaye ninakuwa naye huru muda wote ninaomhitaji, nashindwa nifanyeje, inabidi tu niwe nao wote,” alisema Lyidia Aloyce (33) mkazi wa Kinondoni jijini Dar es Salaam.

Hata hivyo si wasichana pekee, bali hata wanaume baadhi yao wameangukia katika hatari hiyo kwa kuwa na mahusiano na mtu zaidi ya mmoja kwa malengo ya kupata vitu mbalimbali, huku wengine ikiwa ni tamaa ya mwili.

Hata hivyo tafiti za sayansi ya jamii zimeendelea kusisitiza kuwa mahusiano ya ngono ya kibiashara kwa kiasi kikubwa ni tofauti na kazi ya ngono.

Hatari yake

Akielezea hatari yake, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la ushirikishwaji wa jamii kuhusu virusi vya Ukimwi na Ukimwi (Dare), Dk Lilian Mwakyosi alisema ngono muwawana hii ni hali ya kijana au mtu kulazimika kuwa katika mahusiano ya kingono na mtu kwa sababu ya kupata vitu vitakavyomsaidia kujikidhi kimaisha.

Alisema inaweza kuwa mahitaji ya lazima kama chakula, mavazi, malazi, wakati mwingine ada za shule na mahitaji mengine, hasa vitu ambavyo vinaendana na maisha ya siku hizi kama vile kupata simu za mkononi, viatu, aina ya nguo fulani au vifaa vya kidijitaji.

“Vitu hivyo vinamfanya awe katika mazingira ambayo yanamweka katika mahusiano ya kingono na kwa sababu kuna kitu unapata kama matokeo ya kuwa katika hayo mahusiano kama mbadilishano na ngono, inakuwa inapunguza nguvu ya kufanya maamuzi, hasa katika kutumia kondomu kwa mwendelezo na kwa usahihi pia,” alisema Dk Mwakyosi.

Dk Mwakyosi ambaye pia ni mraghabishi na miongoni mwa watafiti wa ugonjwa huo Afrika, alisema ukijaribu kuangalia kwa ukaribu nadharia ya ngono muwawana ni rahisi kuhisi kwamba haina uhatari wowote.

“Watu wengi wanaoshiriki ngono hii, wanajihisi wapo katika uhatari mdogo wa kupata maambukizi ya VVU, kitu ambacho si kweli. Ukitofautisha na wanaofanya biashara ya ngono, wale tayari wanafahamu kwamba mimi mazingira yangu ya kazi yananiweka katika uhatari wa kupata maambukizi ya vvu, wanajua kutumia kinga kwa usahihi na uendelevu,” alisema.

Alifafanua kuwa ngono muwawana katika jamii imekuwa kama ni sehemu ya kawaida na tamaduni kwenye mahusiano.

“Kwamba ukiwa katika mahusiano lazima mtu uliyenaye akuhudumie baadhi ya vitu ambavyo inapunguza nguvu ya kufanya maamuzi na kwa kuwa ni mahusiano yanayojulikana baina ya wenza, ile hali ya kuona umuhimu wa kutumia kinga inakuwa chini zaidi na mtu anajiona hayupo kwenye uhatari ya kupata maambukizi,” alisema Dk Mwakyosi.


Tafiti

Katika tafiti mbalimbali, watafiti wameeleza ngono muwawana huwa na matokeo hasi kwa washiriki wengi.

Imeelezwa baada ya muda mahusiano hayo huzaa chuki, kwani hakuna mtu anapenda kujisikia kutumika. Watu ambao wanahisi hasira au kukuchukia hawana hamu ya kujibu maombi yako ya mara kwa mara.

Katika utafiti uliofanywa mwaka 2019 katika nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara na kukusanya takwimu kwa wanawake vijana 160 wenye umri wa miaka 14-24 na wanaume wenye umri wa miaka 18-35 nchini Uganda na Tanzania ulibaini vijana wengi hawana ufahamu kuhusu mahusiano yaliyopo kati ya ngono muwawana na biashara ya ngono.

Utafiti huo ulioongozwa na Dk Wamoyi Joyce ulipendekeza hatua zaidi zichukuliwe ili kusaidia kupunguza kuenea kwa ngono muwawana miongoni mwa vijana ambao huathirika zaidi na maambukizi mapya.

Kwa nini vijana waelimishwe

Dk Mwakyosi alisema takwimu zinaonyesha vijana wanachukua theluthi moja au zaidi jumla ya watu wanaoishi na VVU nchini, hii inamaanisha kuwa nchi inapopanga mipango yote isiwasahau vijana kwa kuwa wao ndio nguvu kazi ya taifa.

“Katika kuzuia maambukizi tuangalie wao inaonyesha asilimia kubwa miaka 15 hadi 24 ndio wanaoongoza na ukiangalia namba ya watu wanaopata maambukizi mapya kwa mwaka vijana wanachukua asilimia 40 ya maambukizi tunayoyapata nchini, sababu zinaweza kuwa tofauti.

“Kisababishi cha ongezeko kwa kundi hili, hasa wasichana walio katika umri balehe na wanawake vijana imekuwa ni changamoto ya kuichumi na vijana wengi umasikini umechangia kuingia katika mazingira yanayowaweka katika hatari ya kupata maambukizi ya VVU,” alisema.

Dk Mwakyosi alisema mwenendo wa takwimu unaonyesha kundi hilo, wasichana balehe wana uhatari zaidi wa kupata VVU kwa zaidi ya mara tatu ikilinganishwa na wavulana wa umri huohuo.

“Wasichana hawana nguvu ya kufanya maamuzi, hasa wanapokuwa katika mahusiano yanayohusisha ngono na kushindwa kukubaliana matumizi sahihi na endelevu ya kondomu, kuna vitu vingine vingi au tabia nyingi zinazowafanya wawe katika hatari ya kupata maambukizi,” alisema.

Hata hivyo, alisema kinga zipo, lakini kumekuwa na changamoto kwa namna ambavyo huduma zinawafikia vijana na pia hata wao wanakuwa wazito kujitokeza, licha ya huduma kuandaliwa kwa ajili yao.