Ngoma bado ngumu mgomo Kariakoo

Baadhi ya wafanyabiashara wadogo wakiendelea na biashara kama kawaida nyuma yao maduka yakiwa yamefungwa mtaa wa kongo Kariakoo jijini Dar es Salaam mchana huu, kutokana na mgomo waliyouweka wa kufunga maduka. Picha na Sunday George

Muktasari:

  • Licha ya mkuu wa mkoa kutumia zaidi ya dakika 17 kuwasihi kuendelea na shughuli zao kama kawaida, baadhi wameendelea kushikilia msimamo wao wa kutofungua maduka.

Dar es Salaam. Unaweza kusema ngoma bado ngumu katika soko la Kariakoo, baada ya hotuba ya takribani dakika 17 iliyotolewa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila kuwashawishi wafanyabiashara kuendelea na shughuli zao kushindwa kufua dafu.

Hiyo ni baada ya saa mbili tangu kuondoka sokoni hapo saa 6 mchana, lakini mpaka sasa 8 mchana baadhi ya wafanyabiashara wameendelea kushikilia msimamo wao wa kutofungua maduka.

Chalamila alifika sokoni hapo saa 5:09 asubuhi na kufanya kikao na wafanyabiashara, lakini mpaka anamaliza baadhi walionekana kutoridhishwa na kile alichozungumza.

Wafanyabiashara hao wamefunga maduka kwa madai ya kuchoshwa na vitendo wanavyofanyiwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Alipofika eneo hilo aliwasihi wafanyabiashara ndogondogo ‘machinga’ kuendelea na shughuli zao, huku akizungumzia namna wamiliki wa maduka wanavyolalamikia uwepo wao na kutaka waondoke, huku akieleza kuwa msimamo wake ni kutowaondoa.

Chalamila pia alizungumzia malalamiko ya uwepo wa wafanyabiashara kutoka China wanaofanya shughuli ndogondogo  ambao wamekuwa wakilalamikiwa na wafanyabiashara.

“Mkuu wewe umekuja huku kuongea na wafanyabiashara siyo machinga, machinga hawajagoma wanaendelea na shughuli zao, sisi ndiyo tumegoma,” alisikika mmoja wa wafanyabiashara aliyekuwa juu ya ghorofa.

Hata hivyo, Chalamila alimjibu na kusema machinga nao ni wafanyabiashara wakubwa wa kesho.

Akiwa katika mkutano huo, Chalamila amesema anafahamu mgomo huo uko nyuma ya baadhi ya vyama vya siasa ambavyo vinatamani kuwapo kwa maandamano, huku akiwataka kufanya biashara bila kudanganyika.

“Fanyeni biashara msidanganyike, msiichafue Dar es Salaam ndugu zangu, mkiichafua hamna sehemu ya kukimbilia, hakuna mkoa wowote utakaofanya biashara, ilindeni Dar es Salaam kuliko chochote kile. Mkikimbilia Iringa, Mbeya hakuna Kariakoo,” amesema Chalamila.

Amesema mwaka jana ulitokea mgomo kama huo ambao ulimfanya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kwenda kusikiliza, baadhi ya wafanyabiashara walitoa malalamiko yao kwa matusi kwa Serikali, lakini matatizo yote yalibebwa na yanaendelea kushughulikiwa.

Miongoni mwa yanayoshughulikiwa ni yale yanayohusu sheria na utawala ambayo yanahitaji muda.

Chalamila amesema baada ya kufungwa kwa maduka jioni yatakuwa ni majuto baada ya watu kukosa fedha, huku akieleza kitu ambacho anahitaji ni mazungumzo, lakini yanapotishiwa na kushinikizwa huwa hawafanyi kile kinachohitajika.

“Huwa natamani tukae mezani tuelewane, ukiigeuza biashara kuwa siasa siwezi kukusikiliza, mimi si kiongozi wa chama cha siasa, mimi nalea wafanyabiashara wote bila kujali wanatoka wapi wanakwenda wapi,” amesema Chalamila.

Amesema miaka michache nyuma wapo wafanyabiashara waliokuwa wakijifanya wakubwa, lakini Serikali ilipounguruma walihama nchi, huku akieleza hakuna kitu Serikali inashindwa kufanya zaidi ya kukaa kufanya mazungumza kwa pamoja.

“Wapo wafanyabiashara wanawatishia wengine, nimekuja kuwaambia endelea na biashara yako, mimi nitashughulika naye, nitakuja kumpa adabu hapahapa mbele yenu wala siendi mahali popote, hatuwezi kuendesha Serikali kwa migomo,” amesema Chalamila.

Amesema migomo si suluhisho, bali kukaa mezani na kuzungumza ndiyo jambo linaloweza kujenga Dar es Salaam.

Kuhusu wachina kujaa Kariakoo, amesema yanahitajika mazungumzo ya kidiplomasia, ili kujua sehemu ambazo Wachina wanapaswa kusimama na wazawa.

Kuhusu kodi, amesema kiwango cha ukwepaji bado kikubwa, huku akieleza baadhi ya wafanyabiashara wamekuwa wakitishia kugoma pindi Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) inapojaribu kufuatilia utoaji wa risiti.

Amesema kabla ya kuwapo kwa biashara, sheria zilikuwepo hivyo kama mtu alizisoma na kuzielewa, kuzikubali na watu kuanzisha maduka inakuwaje sasa wanalia.

“Sasa kuanza kunishinikiza leoleo, nibadilishe dunia leoleo haiwezekani, mimi nimeahidi kulinda biashara zote, ikiwezekana baadaye kama itahijika kuweka vyombo vya dola nitaweka, ili pote pafungwa halafu tusubiri hadi tusuluhishe, kama itachukua miezi miwili sisi tutalinda kwa miezi miwili hakuna mtu atainama kufungua kufuri,”

“Serikali haishindwi jambo, kama imetuma vikosi Congo kwenda kupigana vinashindwa kuja kupigana Kariakoo, kama Serikali inatuma vikosi kwenda kupigana Sudan (Darful) inashindwa vikosi kuja Kariakoo? Lakini je itakuwa ni biashara? Kama unapata Sh200 leo faida Sh100, basi endelea mazingira yakiwa mazuri kesho utapata Sh400. Ukifunga unapata nini,” amesema Chalamila.

Baada ya Chalamila kuzungumza na baadhi ya wafanyabiashara, wachache walirejea katika shughuli zao za kila siku.

Hata hivyo, wakati maduka mengine yakiwa yamefungwa, wauzaji wa dawa za asili wameendelea na biashara kwa madai kuwa wanatoa huduma za hospitali kunusuru uhai wa binadamu.

"Sisi ni kama madaktari, hivyo tunatoa huduma, ingawa tupo pamoja na wenzetu kwa sababu madai yanayotolewa hata sisi yanatugusa kwenye suala la kodi," amesema Asma Mcheche.

Amesema hata wafanyabiashara wenzao wanawaelewa, kwani wanafanya hivyo kwa ajili ya kunusuru wagonjwa waliopo majumbani na wengine hospitalini.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara wa Karikaoo, Martin Mbwana akizungumza na Mwananchi Juni 22, 2024 alikiri kuona vipeperushi vya kuhamaisha mgomo, akieleza hiyo ni hasira za kuchoshwa na wanayofanyiwa na TRA.