Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Neno la mwisho la Mafuru kwa mdogo wake

Mdogo wa Marehemu, Lawrence Mafuru, Maira Mafuru

Muktasari:

  • Hadi mauti yanamkuta, Mafuru alikuwa Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango, aliyehudumu nafasi hiyo kwa mwaka mmoja na miezi mitatu. Ameacha mjane na watoto wawili.

Dar es Salaam. Wakati mwili wa aliyekuwa Katibu Mtendaji wa Tume ya mipango, Lawrence Mafuru ukitarajiwa kuwasili Tanzania kesho Jumanne Novemba 12, 2024, mdogo wa marehemu, Maira Mafuru amezungumza kauli ya mwisho ya kaka yake.

Amesema, alizungumza na Mafuru Ijumaa iliyopita, siku moja kabla ya kifo chake kilichotokea Jumamosi ya Novemba 9, 2024 wakati akipatiwa matibabu Hospitali ya Apollo nchini India.

Akizungumza na Mwananchi leo Jumatatu, Novemba 11, 2024 nyumbani kwa marehemu Bunju A, jijini Dar es Salaam, Maira amesema walizungumza kwa simu na kumwambia waendelee kumuombea, kwani matibabu yake yakikamilika atarudi kuungana nao tena.

"Tulizungumza kwa simu, akasema atarudi salama matibabu yake yakikamilika, ilikuwa Ijumaa iliyopita," amesema.

Maira amesema kifo chake kimewashtua, kwani alikwenda akiwa katika hali ya kawaida.

"Kama nilivyosema, aliondoka katika hali ya kawaida, anatembea mwenyewe, alituaga anakwenda kwenye matibabu ya kawaida, tuliamini ni matibabu ya kawaida, hata Ijumaa nilipozungumza naye alisema tumuombee atarudi salama matibabu yakikamilika," amesema Maira kwa huzuni.

Akizungumzia makuzi ya Mafuru, amesema kaka yao huyo aliyekuwa wa kwanza kuzaliwa kati ya watoto wanne, alikuwa ni kiungo muhimu kwenye familia.

"Akiwa kaka mkubwa alitaka kila mtu akue kwenye misingi mizuri ambayo yeye amekuwa nayo, alikuwa akifuatilia kwa karibu sisi wadogo zake nini tunafanya,” amesema.

Amesema hata alipowashika mkono kama wadogo zake alimpa kila mmoja uhuru wa kufanya anachokitaka.

"Alikuwa ni kaka ambaye hakai na kitu moyoni, hata tukimkwaza anaongea na dakika hizo hizo ukikiri makosa yanakwisha, ni kaka ambaye alikuwa akishirikiana na kila mmoja," amesema Maira.

Maira anasema wao ni Wajita wenyeji wa Musoma, wazazi wao baba na mama walihamia Shinyanga ambako ndipo mji wao upo na wazee hao wapo mkoani humo.

Kwa upande wake, msemaji wa familia, Epharaim Mafuru amesema mwili wa ndugu yao utazikwa Ijumaa, Novemba 15 katika makaburi ya Kondo, Tegeta, jijini Dar es Salaam.

Mafuru aliyekuwa mtaalamu wa fedha na uchumi maarufu hapa nchini akihudumu katika sekta binafsi na sekta ya umma, mwili wake utawasili nchini kesho Jumanne, Novemba 12 saa 7:45 mchana katika uwanja vya ndege vya Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere ukitokea New Delhi, India na utakwenda kuhifadhiwa hospitali ya Lugalo.

Ephraim amesema Jumatano itakua ni maombolezo nyumbani kwa marehemu Bunju A na Alhamisi Novemba 14, mwili wa Mafuru utaagwa katika ukumbi wa Karimjee kuanzia saa 3:00 asubuhi hadi saa 8:00 mchana, kisha utapelekwa nyumbani kwake utakapolala kabla ya shughuli za maziko yatakayofanyika Ijumaa kuanzia saa 9:00 alasiri.

Ephraim amesema Mafuru aliyeacha mke na mabinti wawili, alikaa nchini India mwezi mmoja kwa matibabu hadi mauti ilipomkuta, Novemba 9, 2024.

Nyumbani kwa marehemu, leo waombolezaji mbalimbali walifika kutoa pole, akiwamo Msajili wa Hazina, Nehemia Mchechu na aliyekuwa mwenyekiti wa Bodi ya Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL), Leonard Mususa.

Mmoja wa marafiki wa marehemu, Mchungaji wa AICT Chang'ombe, Joseph Mayala amesema enzi za uhai wake Mafuru alikuwa mpole, mcheshi, msema kweli na mpambanaji.

"Alikuwa rafiki yangu tangu 1997 nikiwa Benki ya Standard Charter, tukawa marafiki hadi sasa.

"Agosti 8, 2024 nilikuwa naye kwenye Nanenane Dodoma na mara nyingi suala la kumcha Mungu na hata kuombea kazi zetu kwake ilikuwa ni kawaida.

"Aliipenda sana nchi yetu, alikuwa na hamasa na kazi ambayo Rais alimpatia, pia alikuwa ni mnyenyekevu na aliyejali watu," amesema.

Mafuru amefariki akiwa Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango, ambaye amehudumu nafasi hiyo kwa mwaka mmoja na miezi mitatu.