Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Necta yaonya udanganyifu mtihani darasa la nne

Dar es Salaam. Wakati wanafunzi milioni 1.62 wa darasa la nne wakianza kufanya mitihani yao ya upimaji (SFNA) leo, Baraza la Mitihani la Taifa (Necta) limekemea udanganyifu kwa wanafunzi.

Wakati wakimaliza mtihani huo kesho, Jumatatu ya Oktoba 30 hadi Novemba 9 mwaka huu wanafunzi 759,573 kutoka shule za sekondari 5,546 Tanzania Bara wanatarajia kuanza mitihani yao ya upimaji kidato cha pili (FTNA).

Akizungumza na wanahabari, Dk Said Mohamed, ambaye ni Katibu Mtendaji wa Necta alisema kati ya wanaofanya mtihani wa darasa la nne wavulana ni 828,591, sawa na asilimia 48.95 na wasichana ni asilimia 51.05.

“Pia kati ya wanafunzi milioni 1.692 waliosajiliwa kufanya upimaji wa kitaifa wa darasa la Nne mwaka 2023, asilimia 94.84 watafanya kwa lugha ya Kiswahili, asilimia 5.16 watatumia lugha ya Kiingereza ambayo wamekuwa wakiitumia katika kujifunzia,” alisema Dk Mohamed.

Idadi ya wanaofanya mtihani huo wa upimaji ni pungufu kwa asilimia 5.26 ikilinganishwa na wanafunzi milioni 1.71 waliofanya mtihani huo mwaka uliopita.

Akiendelea kufanya uchambuzi wa wanafunzi wa darasa la nne, alisema wenye mahitaji maalumu wapo 6,402 na kati yao, 1,074 ni wenye uoni hafifu, 93 ni wasioona, 1,240 wenye ulemavu wa kusikia, 2,209 ni wenye mtindio wa akili na 1,786 ni wenye ulemavu wa viungo vya mwili.

Siku ya nne baada ya darasa la nne kumaliza mitihani yao, wavulana 353,807 na wasichana 405,766 kutoka sekondari 5,546 Tanzania Bara watafanya mitihani ya upimaji kidato cha pili.

Kati yao, wanafunzi wenye mahitaji maalumu ni 1,382, ambao 683 ni wenye uoni hafifu, 82 ni wasioona, 290 wenye ulemavu wa kusikia na 309 ni wenve ulemavu wa viungo vya mwili na 18 wenye ulemavu wa akili.

“Upimaji huu ni muhimu, kwani unatuwezesha kujua kiwango cha wanafunzi katika kumudu stadi za juu za kusoma, kuandika na kuhesabu. Kwa upande wa kidato cha pili hupima uwezo na uelewa wa wanafunzi katika yale yote waliyojifunza kwa kipindi cha miaka miwili ya masomo yao ya sekondari,” alisema Dk Mohamed.

Alitumia nafasi hiyo kuwataka wasimamizi wahakikishe wanafanya kazi ya usimamizi kwa weledi na kwa kuzingatia kanuni za mitihani na miongozo waliyopewa ili kila mwanafunzi husika apate haki yake.

“Baraza halitarajii kuona mwanafunzi yeyote kujihusisha na vitendo vya udanganyifu. Mwanafunzi yeyote atakayebainika kufanya udanganyifu, matokeo yake yatafutwa kwa mujibu wa Kanuni za Mitihani,” alisema Dk Mohamed.

Pia, Necta iliwataka wamiliki wa shule kutambua kuwa shule zao ni vituo maalumu vya mitihani, hivyo hawatakiwi kwa namna yoyote kuingilia majukumu ya wasimamizi wa mitihani katika kipindi chote cha ufanyikaji wa upimaji huo.