Ndoto ya madaktari mikoani kuhusu matibabu ya saratani

Dar es Salaam. Kila amuonapo mgonjwa wa saratani kutoka Mkoa wa Mbeya akipewa rufaa kwenda Dar es Salaam kwa matibabu ya kibingwa, Dk Godlove Mbwanji anatamani kungekuwa na kituo cha kutibu ugonjwa huo katika mikoa ya Nyanda za Juu Kusini ili kuwasaidia wagonjwa wasisafiri umbali mrefu kufuata matibabu.
Ni wastani wa kilomita 800 kutoka Mbeya hadi Dar es Salaam.
“Hapa tunaweza kutoa matibabu ya msingi tu ya saratani kama dawa za kawaida, lakini hatuna huduma zingine ikiwamo mionzi,” anasema Dk Mbwanji, ambaye ni Mkurugenzi Mkuu wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Mbeya.
Katika hali kama hiyo, kunakuwa hakuna chaguo jingine zaidi ya kuwapa rufaa wagonjwa wa saratani kwenda Kituo cha Saratani cha Ocean Road (ORCI), anasema Dk Mbwanji wakati wa mahojiano maalumu na Mwananchi.
Anasema hali hiyo inasababisha uchelewaji wa matibabu kwa wagonjwa ambao mara nyingi huhitaji kupatiwa tiba ya haraka.
Kama hiyo haitoshi, wagonjwa wengi wanaosumbuliwa na saratani wanaolazimika kwenda Dar es Salaam kwa matibabu zaidi, hujikuta wakiingia gharama kubwa za usafiri na malazi wakiwa katika jiji hilo.
Miongoni mwao ni Christina Lusambo (40), mkazi wa Mbeya, aliyepitia safari ndefu na changamoto za kupata rufaa.
Hii pia ni sababu kwa nini ugonjwa wa saratani unaweza kuwa hatari zaidi kabla ya wataalamu wa ORCI kuingilia kati.
Lusambo alijigundua kuwa na uvimbe katika moja ya matiti yake ambao mwanzo uligundulika kuwa ni ‘jipu’ alipokuwa katika kituo kimoja cha afya karibu na nyumbani kwake.
Hiyo ilikuwa ni mwaka 2014. Hata hivyo, ilimchukua takriban mwaka mmoja mpaka kuja kugundulika kuwa amepata saratani ya titi.
Hata pale alipofahamu, ilimchukua miezi kadhaa kabla ya kuanza kupatiwa matibabu sahihi. Kwa bahati nzuri, alipatiwa rufaa ya kwenda Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) na baadaye ORCI.
Analazimika kurudi Mbeya
Wakati muda wa kupata matibabu sahihi ulipowadia, tatizo jingine jipya lilijitokeza. Lusambo hakuwa na nyaraka sahihi ambazo zingemwezesha kupata matibabu chini ya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF).
“Nililazimika kurudi Mbeya ili kuchukua cheti changu cha ndoa. Ilikuwa ni safari ndefu. Nakumbuka nilikaa nyumbani takriban miezi minne kabla ya kurudi Ocean Road, kinyume na nilivyokuwa nimeelekezwa na madaktari,” anasema Lusambo.
Anasema ilimchukua muda mrefu kujiunga na bima ya afya akiwa mnufaika wa kadi ya mume wake ambaye ni mwalimu.
“Madaktari walinigombeza niliporudi Dar es Salaam miezi minne baadaye. Waliniambia kansa yangu imeenea kwa kiasi kikubwa mwilini mwangu.”
Hivi sasa anasema tayari ameshafanya matibabu kwa hatua ya sita ya tiba ya dawa ambayo kitaalamu inaitwa chemotherapy. “Namshukuru Mungu naendelea vizuri,” alisema huku akionyesha matumaini kwamba atapona na hivyo kuendeleza shughuli zake za kilimo.
Hata hivyo, tatizo kama hili la Lusambo huwakumba wagonjwa wengi wa saratani nchini.
Muuguzi aliyemhudumia, Chausiku Chapuchapu anasema, “Tunakabiliwa na changamoto kadhaa zinazohusiana na wagonjwa wa aina hii wanaotoka maeneo ya mbali. Huko wanakotoka inachukua muda mrefu kugundua ugonjwa wao.
“Hata muda wa kuchukua kipimo (biopsy) kutoka kwenye sehemu ya nyama iliyoathirika ukifika, mara nyingi huwa imeshachelewa sana,” anasema Chapuchapu na kuongeza:
“Kwa wagonjwa kutoka Mwanza, kuna afadhali kwa sababu wengi wao wanabainika kuugua saratani katika Hospitali ya Bugando, lakini kwa wanaotoka mikoa kama ya Kigoma na maeneo mengine ya mbali, bado kuna changamoto nyingi.”
Kwa Mkoa wa Mbeya, Dk Mbwanji na mamlaka zingine za afya mkoani humo waliohojiwa wanaamini kwamba ni muda muafaka sasa kwa vituo kama ORCI vikajengwa katika kanda, lakini pia kuweka miundombinu ya uchunguzi wa awali katika ngazi za chini.
Kutofahamu taratibu za rufaa
Anitha Chula (40) amesafiri takribani kilomita 255 kutoka Mafinga, Iringa hadi Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Mbeya kwa ajili ya kupima saratani ya mlango wa kizazi.
Anasema haziamini hospitali za chini. Amepita vituo kadhaa vya afya ambavyo vingeweza kutoa huduma hiyo.
Hata hivyo, kwa mujibu wa Mganga Mkuu wa Mbeya (RMO), Yahaya Msuya huduma za ‘screening’ kwa saratani ya mlango wa kizazi zinatolewa na hospitali za wilaya ambazo Chula amezipita.
Wagonjwa kama Chula husababisha changamoto katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Mbeya kwa sababu ya ukosefu wa mwamko wa jinsi mfumo wa rufaa unavyofanya kazi nchini.
Alipoulizwa kama anajua kuwa huduma aliyoifuata Hospitali ya Rufaa ya Kanda inapatikana kwenye vituo vya afya alivyovipita, Chula alijibu: “Sikujua.”
Muuguzi ambaye alimfanyia uchunguzi wa awali, Ruth Fungo anasema wamekuwa wakipokea watu wenye mtazamo kama wa Chula.
“Ni changamoto kwa sababu inafanya utoaji wa huduma kuwa mgumu. Tunachoweza kukitoa hapa ni kwa wale waliopitia mfumo wa rufaa,” anasema.
Hatuwezi kuwarudisha
Licha ya ukweli kwamba baadhi ya wagonjwa wanafika hospitalini hapo bila kufuata utaratibu, hospitali haiwanyimi huduma.
“Inabidi tuwasaidie lakini wakati huohuo tukiwaelimisha kwamba huduma waliyoifuata hapo inapatikana karibu na nyumbani anakotoka,” anasema Fungo.
Lakini kwa mujibu wa Dk Mbwanji, mfumo wa taifa wa rufaa, licha ya mafanikio kadhaa yaliyopatikana kwa siku za hivi karibuni, bado unahitaji kuboreshwa.
Dk Mbwanji anasema dhana iliyojengeka miongoni mwa watu kwamba huduma bora za afya zinapatikana katika hospitali kubwa na za rufaa pekee, inaweza kuondoshwa kwa kuimarisha utoaji wa huduma za afya katika ngazi za awali.
Wazo la Dk Mbwanji linaendana na utafiti uliofanywa mwaka 2008 uliopewa jina la ‘Taratibu za rufaa za wagonjwa waliopokewa katika hospitali ya rufaa ya Taifa.
“Changamoto katika nchi zenye kipato cha chini’ uliochapishwa katika Jarida la Afya ya Jamii la Afrika Mashariki.
“Juhudi za kuimarisha mfumo wa rufaa katika nchi zenye kipato cha chini zinahitaji kwenda sambamba na uboreshwaji wa huduma katika ngazi za awali ili kuweza kuzuia matumizi yasiyo ya lazima ya hospitali za rufaa,” unapendekeza utafiti huo.
Kuhusu saratani, Dk Mbwanji anapendekeza kuwe na juhudi za kuwajengea uwezo wataalamu wanaofanya kazi katika hospitali za ngazi za chini na uwekaji wa vifaa tiba stahiki kwa ugunduzi wa saratani na utabibu.
Takwimu zilizopatikana katika ofisi ya Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, zinaonyesha asilimia 16 ya kata 178 zimeunganishwa na vituo vya afya.
Sensa ya mwaka 2012 inaonyesha asilimia 44 ya vijiji vya mkoa huo, ambao una takriban watu milioni mbili, ndio vina zahanati.
Hii kwa mujibu wa Dk Msuya. Anasema hali hiyo inazifanya Hospitali za Rufaa za Mkoa wa Mbeya na ya Rufaa ya Kanda ya Mbeya kuelemewa na mzigo wa huduma ambazo haziwezi kutolewa katika ngazi za chini.