Ndege kutafiti madini Mirerani

Mkurugenzi mkuu wa taasisi ya jiolojia na utafiti wa madini Tanzania (GST) Dk Mussa Budeba (katikati) akielezea namna ndege nyuki zilivyotumika kufanya utafiti wa madini mji mdogo wa Mirerani wilayani Simanjiro mkoani Manyara. Picha na Joseph Lyimo
Muktasari:
- Imeelezwa kuwa, utafiti wa madini utawasaidia wachimbaji wadogo kuepukana na hasara na kupoteza muda wa kuchimba maeneo yasiyo na madini.
Mirerani. Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) imetumia ndege nyuki kufanya utafiti wa kubaini maeneo yenye Tanzanite, mji mdogo wa Mirerani wilayani Simanjiro Mkoa wa Manyara.
Imeelezwa kuwa utafiti huo utawasaidia wachimbaji wadogo kuepukana na hasara na kupoteza muda wa kuchimba maeneo yasiyo na madini.
Mkurugenzi Mkuu wa GST, Dk Mussa Budeba amesema leo Jumapili Juni 23, 2024 kuwa, baada ya kufanyika utafiti wa awali utasaidia urahisi wa upatikanaji wa madini ya Tanzanite.
Dk Budeba amesema utafiti huo utawaepusha wachimbaji na hasara ya kuchimba kwa mazoea kwenye maeneo yasiyo na madini na kwa utafiti huo, tayari kitalu C na D vimeshapimwa.
Amesema wanatarajia kufanya utafiti kwa asilimia 50 kwenye maeneo yote nchini ifikapo 2030.
“Hivi sasa tumeshafanya utafiti kwa asilimia 16, baadhi ya machimbo, Waziri wa Madini Anthony Mavunde amekuja na vision (maono) ya 2030 ya madini ni maisha na utajiri, kwa kufanya utafiti na tunamshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutuongezea bajeti,” amesema Dk Budeba.
Ofisa Madini Mkazi Mirerani, Nchagwa Marwa amesema utafiti huo wa awali uliofanywa na GST, umehusisha vitalu viwili vya C na D na utafiti ujao utahusisha maeneo yaliyosalia.
Marwa amesema GST watarejea tena kwa kuongeza wigo wa kufanya utafiti kwenye maeneo yote ya machimbo ya Tanzanite yaliyopo mji mdogo wa Mirerani.
Meneja Mkuu wa Kampuni ya Franone Mining Ltd, Vitus Ndakize amesema utafiti huo utatanua wigo wa uchimbaji madini kwa kuepuka uchimbaji wa kubahatisha.
Ndakize amesema utafiti utakuwa chachu kwa wachimbaji wa Tanzanite, kwa sababu utapunguza gharama kwa kuwa wachimbaji watafanya kazi hiyo kwa kufuata taarifa zinazotolewa na GST.
Akizungumzia hilo, mchimbaji mdogo wa madini ya Tanzanite eneo la kitalu D, Paulo Mwanache amesema utafiti huo utakuwa njia rahisi kwao ya kufanya uchimbaji usiokuwa na hasara tofauti na mwanzo.
“Utafiti umetuonyesha maeneo yenye miamba iliyolala na wapi penye madini mengi na wakatueleza sababu ya madini kuungua chini kabla ya uzalishaji wake,” amesema Mwanache.