NBS kutoa matokeo ya sensa kwa baadhi ya maswali

Kamisaa wa Sensa Tanzania Bara, Anna Makinda
Muktasari:
- Serikali imesema matokeo ya Sensa ya watu na makazi yanayozinduliwa leo ni matokeo ya chambuzi katika maswali machache kati ya 100 yaliyokuwapo katika dodoso na kwamba matokeo mengine yataendelea kutangazwa kadri uchambuzi unapokamilika kwa mujibu wa kalenda.
Dar es Salaam. Kamisaa wa Sensa Tanzania Bara, Anna Makinda amesema matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi yanayozinduliwa leo ni matokeo ya mwanzo yanayotokana na uchambuzi wa maswali machache kati ya 100 yaliyokuwapo katika dodoso.
Ameyasena hayo leo Oktoba 31 wakati hafla ya uzinduzi wa Matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi iliyofanyika Agosti mwaka huu nchini kote.
Makinda amesema kadri uchambuzi utakavyokuwa unakamilika ndivyo matokeo yatakavyoendelea kutolewa kwa mujibu wa kalenda ya kuchapisha matokeo ya Sensa.
"Kwa hiyo haya leo ni matokeo ya mwanzo, mengine yatakavyozidi kuchambuliwa yataendelea kutolewa, kuna mambo ya ustawi wa jamii, hali halisi, mazingira, yataendelea kutolewa kwa mujibu wa kalenda," amesema Makinda.
Amesema awamu hiyo ni muhimu kwani walipokuwa wakielimisha na kuhamasisha watu kushiriki sensa walizungumzia umuhimu wa kujenga mustakabali wa maendeleo ya nchi.
Amesema suala hilo lilileta matumaini kwa wananchi huku akieleza kuwa elimu hiyo ilileta mwamko wa watu kushiriki Sensa.
"Tunayo kazi ya kukidhi matumaini ya wananchi na yatafikiwa ikiwa tutazitumia ipasavyo takwimu za Sensa, bahati nzuri Serikali imeandaa mwongozo maalumu wa matumizi ya takwimu za sensa na ndiyo utakaowezesha Serikali zote kukidhi matarajio ya wananchi," amesema Makinda.