NBS kuja na mpango kazi yaliyobaikia kwenye sensa

Kamisaa wa Sensa, Anne Makinda
Muktasari:
Wakati Shirika la Umoja wa Kimataifa la Idadi ya Watu (UNPFA) likiahidi kuendelea kusaidia Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), kufanya kuchakata takwimu za sensa ya watu na makazi, Kamisaa wa Sensa ya Watu na Makazi, Anne Makinda amesisitiza umuhimu wa matumizi ya takwimu hizo.
Dodoma. Kamisaa wa Sensa, Anne Makinda amesema kazi inayofanywa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) ni kutengeneza mpango kazi (roadmap) kwa ajili ya utekelezaji wa mambo yaliyobakia ya sensa ya watu na wakazi.
Hatua hiyo inakuja baada ya Oktoba 31, 2022 Rais Samia Suluhu Hassan kutangaza kuwa idadi ya watu waliohesabiwa katika sensa ya watu na makazi iliyofanyika Agosti 23 mwaka huu ilikuwa ni milioni 61.7.
Makinda ameyasema hayo leo Jumatano Novemba 16,2022 baada ya hafla fupi ya kumwaga Naibu Mwakilishi Mkaazi wa Shirika la Kimataifa la Idadi ya Watu (UNPFA), Wilfredy Ochan iliyonyika katika Ofisi za NBS.
“Kuna kazi nyingi sana kuweza kuzitengeneza zile takwimu za sensa ziweze kutumika kwa matumizi mbalimbali,”amesema.
Amesema UNPFA imeahidi kuendelea kuisaidia Tanzania ili watu waweze kufahamu matumizi ya takwimu walizozipa katika sensa.
Amesema ingawa watanzania hawana utamaduni wa kutumia takwimu lakini kwa sensa iliyofanyika mwaka huu wanataka matumizi yaweze kuonekana.
Makinda amesema Ochan ameahidi UNPFA itaendelea kuisaidia NBS na kwamba hadi sasa imeahidi kuwasaidia Euro 200,000 na kusisitiza takwimu zitumike sio zifungiwe makabatini.
Aidha, amesema UNPFA ilikuwa ni miongoni mwa mashirika yaliyosaidia kwa kiasi kikubwa katika kufanikisha sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 ambapo walisaidia kwenye masuala ya ufundi, utaalam unaostahili na vifaa.
Makinda ambaye pia ni spika wa Bunge la 10, amesema UNPFA iliwasaidia katika kuwashirikisha na mashirika mengine ambayo yaliwawezesha kupata vishkwambi zaidi ya 800 kwa ajili ya sensa.
Kwa upande wake, Ochan amesema mbali na kuteuliwa kuwa mwakilishi wa UNPFA nchini Ghana, shirika hilo litaendelea kuangalia na kuhamasisha raslimali za kuisaidia NBS kwenye kuchakata takwimu za sensa ya watu na makazi.
“Natumaini mtahamasisha wanasiasa na watu wengine kutumia takwimu hasa katika utengenezaji wa mipango ya maendeleo na bajeti,”amesema.