Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mwili wa mwanamke waokotwa Mwanza

Muktasari:

  • Mwili wa mwanamke ambaye hajatambulika umeokotwa katika mtaa wa Kuzenza kata ya Nyegezi jijini Mwanza huku ukiwa na majeraha maeneo mbalimbali ikiwamo shingoni na usoni.

Mwanza. Mwili wa mwanamke ambaye hajatambulika umeokotwa katika mtaa wa Kuzenza kata ya Nyegezi jijini Mwanza huku ukiwa na majeraha maeneo mbalimbali ikiwamo shingoni na usoni.

Mwili wa mwanamke huyo ambaye anakadiriwa kuwa na umri kati ya miaka 25 hadi 35 umekutwa leo Septemba 4, 2022 huku ukionekana kuchanwa shingoni na kitu chenye ncha.

Mbali na majeraha hayo, baadhi ya sehemu ya mwili wake zimeonekana kuvunjika ikiwemo mguu wa kulia na mkono wa kushoto.

Baada ya maofisa wa polisi kuwasili katika eneo hilo walifanya uchunguzi wa awali kwenye eneo ulipokuwa mwili huo na kukuta mkasi na chupa ya pombe aina ya Valeur ambayo ilikuwa na mabaki ya kinywaji hicho ndani yake.

Akizungumza na Mwananchi katika eneo hilo, Mkazi wa Mtaa wa Kuzenza kaya ya Nyegezi jijini hapa, Jeni Mwebesa amelaani tukio hilo huku akisema huo ni ukatili na kuomba mamlaka husika kuwatafuta na kuwakamata waliotekeleza tukio hilo.

Pia, amesema tangu ahamie katika eneo hilo ni mara ya kwanza kushuhudia tukio kama hilo.

“Nimekuja kushuhudia nikakuta mwili umetupwa hapo ukiwa na majeraha mwilini mwake na kitendo hiki sijakipenda nakemea kwa sababu mwanamke kama huyu kuuawa wamekatisha ndoto zake,” amesema Jeni ambaye baada ya kukuta mwili huo ukiwa wazi alichukua kitenge chake na kuufunika.

Hata hivyo, Mwenyekiti wa mtaa wa Kuzenza lilipotokea tukio hilo (jina lake halikutambuliwa baada ya kuchukuliwa na Polisi) na mtaa wa Igubinya, Ndonho Nzella kata ya Nyegezi jijini hapa walipoitwa na maofisa wa Jeshi la Polisi kuutambua mwili huo walidai hawamtambui mwanamke huyo.

Baada ya mwili huo kuwekwa kwenye gari ya polisi, askari aliyeongoza msafara huo alipotakiwa kuzungumzia walichobaini amekataa akidai mwenye mamlaka ya kulizungumzia ni Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Mwanza.

Akizungumza kwa njia ya simu kwa niaba ya Kamanda wa Polisi mkoa wa Mwanza, Ramadhani Ng’anzi, Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Gideone Msuya amethibitisha kutokea mauaji hayo huku akisema maofisa wa polisi wanaendelea na uchunguzi wa tukio hilo.

“Taarifa ndiyo imefikia muda huu, tunaifanyia kazi na mara uchunguzi ukikamilika tutatoa taarifa,” alisema Msuya