Mwili wa mtalii aliyefia Ngorongoro wasafirishwa

Muktasari:
- Inbar, aliyefunga ndoa mwaka jana na Or Geisler, alikuwa binti wa mfanyabiashara mkubwa nchini Israel, Greidinger.
Arusha. Mwili wa mtalii, Inbar Greidinger-Geisler (30), aliyefariki dunia kwa ajali ya gari ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro, umesafirishwa kwenda nyumbani kwao mji wa Tel Aviv, nchini Israel kwa ajili ya taratibu za mazishi.
Mtalii huyo alifariki dunia kwa ajali Jumamosi ya Januari 4, 2025, baada ya gari inayomilikiwa na kampuni ya Wakali Safaris kupinduka na kujeruhi watalii wengine watano kutoka Israel na Mtanzania mmoja aliyekuwa dereva.
Akizungumza kwa simu leo Jumatatu, Januari 6, 2025, Balozi wa Israeli nchini Kenya na kanda ya Afrika Mashariki, Michael Lotem, amethibitisha kuwa mwili wa mwanamke huyo umesafirishwa jana Jumapili hadi nyumbani kwao Tel Aviv, nchini Israel kwa ndege kwa ajili ya taratibu za mazishi.
“Mwili wa marehemu Inbar Greidinger-Geisler umesafirishwa pamoja na mumewe na wanafamilia wote waliojeruhiwa kwenda Tel Aviv kwa ajili ya matibabu zaidi,” amesema Balozi Lotem na kuongeza;
“Tunashukuru mamlaka za Tanzania waliosaidia kuwawahisha hospitali majeruhi na kuwapatia huduma za haraka, lakini pia tunapongeza uongozi wa hospitali husika kwa kuwahudumia vema,” amesema.
Inbar, aliyefunga ndoa mwaka jana na Or Geisler, alikuwa binti wa mfanyabiashara mkubwa nchini Israel, Naomi Greidinger ambaye pia ni mkurugenzi wa maktaba ya Chuo Kikuu cha Haifa.
Awali, taarifa iliyotolewa na Kaimu Meneja wa Uhusiano wa Umma wa NCAA, Hamis Dambaya ilieleza ajali hiyo ilitokea kati ya kituo cha kutazama kreta na lango kuu la Loduare na gari hilo lilikuwa na watu saba.
Alisema majeruhi walipelekwa katika hospitali za Lutherani na Fame zilizopo wilayani Karatu kwa huduma ya kwanza na baadaye kusafirishwa kwenda Hospitali ya Arusha Lutheran Medical Center (ALMC) maarufu Selian kwa matibabu zaidi kabla ya kwenda kuchukuliwa.