Mwenge waanza na kuteketeza lita 100 za gongo

Wakimbiza Mwenge kitaifa wakiongozwa na Kiongozi wa Mbio za Mwenge kitaifa Abdallah Shaib Kaim wakiteketeza pombe aina ya gongo Lita 100 iliyotengenezwa kwakutumia bibo katika manispaa ya Mtwara mikindani.
Muktasari:
- Zaidi ya lita 100 za pombe ya moshi zimeteketezwa Mtwara mjini baada ya kesi kumalizika katika mahakama mbalimbali mkoani hapa, huku Halmashauri ya Mji Nanyamba ya Mkoani Mtwara na pamoja na Kijiji cha Luokwe cha mkoani Lindi zikitajwa kuwa kinara wa kutengeza pombe haramu ya gongo inayotengenezwa kwa kutuma tunda la bibo.
Mtwara. Zaidi lita 100 za pombe haramu ya gongo zimeteketezwa na wakimbiza mwenge kitaifa baada ya kesi kumalizika katika mahakama mbalimbali mkoani Mtwara.
Akitoa taarifa hiyo mbele ya kiongozi wa mbio za Mwenge kitaifa Abdallah Shaib Kaim wakati wa zoezi la kuteketeza gongo hizo, Koplo Lameck Mwita kutoka Jeshi la Polisi Mkoa wa Mtwara Kitengo cha Upelelezi wa Makosa ya Jinai wa Madawa ya Kulevya, alisema kuwa Luokwe na Nanyamba ni kinara kwa kutengeneza pombe hiyo haramu ya gongo.
“Leo tumetekekeza pombe haramu lita 100 ambazo kesi zake zimeisha na watu wameshakututwa na hatia ndiyo maana inateketezwa. Tunatoa wito kwa wananchi wanaofanya biashara hii ama kutengeneza pombe aina hii wajue kabisa kuwa ni kinyume cha sharia,” amesema.
“Zipo kesi 25 zinazotokana na pombe ya moshi kesi 10 zimeisha na kesi sita wametiwa hatiani moja wapo ni hizi ambazo zinateketezwa leo,” amesema Koplo Mwita.
Naye Hassan Juma mkazi wa Mtwara amesema kuwa pombe hiyo ni hatari kwa afya elimu itolewe zaidi vijijini ili kunusuru afya za Watanzania wanaotumia.
Unajua licha ya kuwa ni haramu lakini namna inavyotengenezwa pia sio salama kwa afya hivyo tunapaswa kushirikiana na vyombo husika ili kuweza kupunguza matumizi na utengenezaji wa pombe hiyo,” amesema Juma.
Naye Ashura Iddi Mkazi wa Mtwara mjini amesema kuwa licha ya hii pombe kuwa haramu lakini watu wanaotengeneza na kuuza wengine wanakunywa kwanini haidhibitiwi.
"Wengi wanaotumia pombe hizi tuko nao mitaani nao wachukuliwe hatua ikikosa wateja hata watengenezaji hawatatengeneza alafu ukitaka kujua kuwa haifai angalia wanaokunywa Yaani muda wote wamelewa hata hawafanyi kazi wala hawana maendeleo," amesema Idd.