Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mwanamke jasiri anayetegemea uvuvi kuendesha maisha yake

Elelath Mbugi akiwa pamoja na mvuvi mwenzake wakitayarisha nyavu ambayo hutumika kwa ajili ya kuvua samaki Picha na Peter Saramba.

Muktasari:

  • Amevunja utamaduni uliojengeka kwa muda mrefu kuwa kazi na uwekezaji katika sekta ya uvuvi hufanywa na wanaume na hivi sasa amekuwa mfano katika shughuli za uvuvi

Mwanza. Penye nia pana njia! Huo ndiyo usemi unaofaa kueleza siri ya mafanikio ya Elelath Mbugi (43), mwanamke jasiri asiyeogopa mawimbi ndani ya Ziwa Victoria anayeendesha maisha yake kwa shughuli ya uvuvi wa samaki aina ya Sangara.

Elelath, mama wa watoto wanane siyo tu ni mvuvi, bali pia ni mmiliki wa kambi ya uvuvi wenye boti 20 za kuvua Sangara zinazotoa ajira kwa wavuvi 65.

Haikuwa njia rahisi kufikia mafanikio haya, kwani Elelath amelazimika kuruka viunzi kadhaa ikiwemo mila, desturi na imani potofu dhidi ya wanawake katika baadhi ya shughuli za kiuchumi, hasa zinazohusu sekta ya uvuvi na madini.

Akizungumza na Mwananchi katika mahojiano maalumu, Elelath anasema mafanikio yake yamekumbana vikwazo vingi ikiwemo vile vya kutengwa na wavuvi wenzake kwa madai kuwa wanawake hawatakiwi kuingia ziwani wanapokuwa kwenye siku za mzunguko wa hedhi kwa sababu wana mkosi unaowafukuza samaki.

Anasema wakati anaanza kazi hiyo, miaka 22 iliyopita, alikuwa anashirikiana na mume wake ambaye hata hivyo aliamua kuiacha na hivyo kufanya abaki mwenyewe; ndipo unyanyapaa dhidi yake kutoka kwa wavuvi wengine ulipoanza.

“Siyo tu nilikuwa natengwa na wenzangu, bali pia nilionekana mwanamke mwenye tabia ya ajabu kwa kuingilia shughuli ya uvuvi ambayo imezoeleka kufanywa na wanaume. Sikujali bali niliongeza bidii” anasema


Alifikaje kwenye uvuvi?

Anasema yeye na mume wake walikuwa wauza viatu vya mtumba katika Soko Kuu jijini Mwanza lakini waliona biashara ya samaki ina faida zaidi hivyo waliamua kuifanya baada ya kupata taarifa kutoka kwa watu tofauti.

Anasema mwanzoni wakati anaanza biashara ya samaki kipato cha mauzo kilikuwa kizuri kwani walikuwa wakiviuzia viwanda kwa bei ya Sh7,000 hadi Sh7,500, pia gharama ya kununua mafuta ya taa kwa ajili ya taa za karabai za uvuvi ilikuwa nafuu kwani lita moja iliuzwa kwa Sh800.

“Hivi sasa hali imekuwa ngumu maana wavuvi hatuna fursa ya kuuza viwandani moja kwa moja bali tunawauzia mawakala kwa Sh5,000 hadi Sh6,000 kwa kilo moja” anasema

Bila kutaka kutaja mtaji alioanza nao, Elelath anasema; “Kwa kutumia mtaji wetu wa mitumba na akiba kidogo tuliyokuwa nayo, tukaingia kwenye uvuvi na sasa tumefikia mafanikio haya ambayo kwa hakika ni jambo la kumshukuru Mungu,”


Changamoto

Penye mafanikio hapakosi changamoto na ndivyo anavyosema Elelath akitaja uvamizi na wizi wa mashine za uvuvi ziwani nyakati usiku kuwa miongoni mwa changamoto zinazomrejesha nyuma kimafanikio.

“Maharamia wamewahi kuvamia boti zangu na kuiba mashine sita za uvuvi. Pia kuna wizi wa mitego licha kuwepo doria,” anasema

Anaipongeza Serikali kupitia mamlaka mbalimbali kwa kuanzisha utaratibu wa kukagua stakabadhi za ununuzi wa vifaa vya uvuvi akisema imepunguza kwa kiasi kikubwa wizi wa vifaa ziwani na katika kambi za uvuvi.

Licha ya kupambana, Elelath anasema tatizo la unyanyapaa dhidi ya wanawake bado ni kubwa kwenye sekta ya uvuvi, hasa anapohamia maeneo mapya kulingana na upatikanaji wa samaki.

“Kambi zetu za uvuvi ni za kuhamahama kulingana na upatikanaji wa samaki, sasa ninapohamia maeneo mapya nakutana na tatizo la unyanyapaa kwa wavuvi ninaowakuta huku kuniangalia kama mwanamke. Msimamo na uimara wangu katika kusimamia kile ninachokiamini ndio silaha yangu kubwa inayoniwezesha kumudu hali hiyo,” anasema

Anasema hadi sasa, ameshahamia na kukaa katika visiwa zaidi ya sita za uvuvi ambako kote amefanikiwa kuvunja na kuruka kiunzi cha unyanyapaa dhidi ya wanawake kwenye sekta ya uvuvi huku akiwahimiza wanawake wengine kujitokeza kuwekeza na kushiriki shughuli za uvuvi kwa sababu ni kazi inayoweza kufanywa na wote, wake kwa waume.

Anasema rushwa ya ngono ni changamoto nyingine ambayo wanawake wavuvi, wafanyabiashara, walanguzi na wachuuzi wa bidhaa za samaki hukumbana nayo kwenye visiwa na mialo yote ya uvuvi lakini msimamo, kujitambua na nidhamu binafsi ndiyo silaha pekee.

“Ukionyesha kijiheshimu, kuwa na msimamo na kuzingatia kazi zako wanaume wenyewe wanarudi nyuma,” anasema