Mwanamke adaiwa kujiua kwa sumu kisa madeni

Unguja. Veronika Peter (46) Mkazi wa Zanzibar, anadaiwa kujiua kwa kunywa kitu kinachodhaniwa ni sumu kutokana na kuelemewa na madeni mengi yatokananyo na mkopo kadhaa aliyochukua huku akishindwa kuilipa.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi Richard Mchonvu amesema hayo leo Julai 12, 2023 wakati akitoa taarifa ya matukio yaliyojiri ndani ya kipindi cha kuanzia Julai Mosi hadi leo.
“Veronika alikuwa akiishi Mpendae anadaiwa kujiua baada ya kuona ameelemewa na mzigo mkubwa wa madeni. Nitoe wito kwa akina mama tuache tamaa wengi wanakopa mikopo wananunua nguo nzuri huwezi kurudisha mkopo kwa nguo ulizozivaa mwilini,” amesema bila kufafanua taasisi alizokopa na kiasi kilichokpwa.
Katika hatua nyingine jeshi la polisi linawashikilia vijana wawili Omar Abeid (22) na Eradius Katoto (26) kwa tuhuma za kuiba betri nane zinazotumika katika mifumo ya umeme jua ambao huwasha taa za barabarani, tukio lililotokea Julai 10 eneo la Migombani majira ya usiku.
Kamanda Mchonvu amesema katika tukio hilo walikamata gari aina ya Suzuki Carry likiwa limeegeshwa eneo inapotengenezwa barabara ya Mnazi Mmoja - Uwanja wa ndege na ilipokaguliwa ndani walikuta betri nne na walipohojiwa vijana hao walikiri kuiba betri hizo na zingine nne na kuziuza kwa Sh120, 000 kwa Asha Riziki.
Pia wamemkamata Mohamed Mkubwa (42) kwa tuhuma za wizi wa pikipiki mbili na mwingine Hafidh Salum kwa wizi wa unyang’anyi kwa kutumia nguvu ambao walikutwa na simu ya aina ya Huawei ambayo ilikwapuliwa na tayari mmiliki wake ameitambua.
Kamanda Mchonvu amesema jeshi hilo litaendelea kuhakikisha ulinzi na usalama huku likiwataka wananchi kujitokeza kutoa ushahidi pindi wanapokamatwa watuhumiwa kwa kuwa kukataa kutoa ushahidi mahakamani, kunarudisha nyuma jitihada za kuzuia uharifu.