Mwanafunzi aliyepotea Arusha akutwa akiuza baa

Muktasari:
- Mwanafunzi wa kidato cha tatu katika shule ya sekondari Longido mkoani Arusha (jina limehifadhiwa) aliyetoweka kwa zaidi ya siku 30 amekutwa akiuza pombe kwenye moja ya bar maarufu mjini Moshi.
Moshi. Mwanafunzi wa kidato cha tatu katika shule ya sekondari Longido mkoani Arusha (jina limehifadhiwa) aliyetoweka kwa zaidi ya siku 30 amekutwa akiuza pombe kwenye moja ya bar maarufu mjini Moshi.
Mwanafunzi huyo wa kiume alitoweka nyumbani kwao Kwa Mromboo, Arusha tangu Septemba 19, mwaka huu na hakuonekana shuleni alikokuwa akienda kuripoti siku hiyo ambapo baadaye wazazi walipata taarifa kwamba mwanafunzi huyo hakuripoti shuleni.
Baada ya kubainika mwanafunzi huyo hajulikani alipo na hakuripoti shuleni wazazi wake walikwenda kutoa taarifa katika kituo cha polisi cha Muriet kilichopo Wilaya ya Arusha na kupewa namba ya kumbukumbu MRT/RB/4900/2023 kufuatilia mwanafunzi huyo alipo.
Alipotafutwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Justine Masejo kuhusiana na tukio la kutoweka kwa mwanafunzi huyo alisema apewe muda anafuatilia tukio hilo na kwamba atalitolea taarifa baadaye.
"Ngoja nifuatilie ili lifanyiwe kazi," amesema Kamanda Masejo.
Akielezea kutoweka kwa mwanafunzi huyo leo Oktoba 23, baba mkubwa wa mwanafunzi huyo, Philibert Mshanga amesema baada ya mwanafunzi huyo kuaga nyumbani kwao kwenda shuleni hakuonekana kwa zaidi ya mwenzi mmoja mpaka alipokutwa Oktoba 19 akifanya kazi baa.
"Novemba 18 mwaka huu ambapo ndio siku shule zilifunguliwa mtoto aliondoka nyumbani muda wa saa nne asubuhi kwenda shuleni Longido na ana desturi akifika shuleni anatoa taarifa kwa wazazi kwamba amefika, sasa zikawa zimepita siku kadhaa hajatoa taarifa.
"Wazazi wakajiuliza mbona hajatoa taarifa ya kufika shuleni? Wazazi wakapiga simu shuleni, wakaelezwa ana vipindi vitatu hajaonekana darasani, ikabidi wazazi wafike pale shuleni kupata taarifa zaidi, walipofika ni kweli hakuonekana ikabidi waende kituo cha polisi kwenda kutoa taarifa," amesema.
Amesema baada ya kupewa RB namba waliendelea kumtafuta mwanafunzi huyo pamoja na kutuma taarifa za kumtafuta mtoto huyo kwenye makundi mablimbali ya WhatsApp ambapo siku chache baadaye ulitumwa ujumbe kwenye simu ya mama yake uliosomeka, "Njoo nichukue nateseka."
"Baada ya mama yake kupata ujumbe huo, alipiga simu ambayo ilituma ule ujumbe na ikapokelewa na mwanamke mmoja, akamuuliza wewe ni nani akamwambia kuna ujumbe umetuma kwenye simu yangu,” amesema.
Amesema baadaye polisi walifuatilia mawasiliano ya namba iliyotuma ujumbe kwenye simu ya mama wa mwanafunzi huyo ambayo ilifanikisha kumpata mwanafunzi huyo akiwa kwenye moja ya baa iliyopo Soweto Manispaa ya Moshi.