Mwanafunzi aliyepotea Mbeya apatikana kwa muuza mkaa

Mwanafunzi, Esther Noah (katikati) akiwa na mama yake mzazi Isalia Iyobu (aliyekaa kulia) wakiwa ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya baada ya kupatikana Juni 23, 2023
Dar es Salaam. Mwanafunzi wa kidato cha tano, wa shule ya Sekondari ya Panda Hill aliyetoweka shuleni Mei 18, 2023, Esther Mwanyilu amepatikana akiwa hai katika chumba cha muuza mkaa eneo la Ifisi mji mdogo wa Mbalizi mkoani Mbeya.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Juni 23, mkoani hapo, Mkuu wa Mkoa huo, Juma Homera amesema chumba hicho kinamilikiwa na Azurati Mohamed ambapo baada ya mahojiano alidai binti huyo alikabidhiwa na mmoja wa mteja wake.
“Amepatikana akiwa hai maeneo ya Isisi mji mdogo wa Mbalizi akiwa katika chumba cha mwanamke mmoja ambaye ni muuza mkaa kwenye nyumba ya kupanga ya Azurati Mohamed, alikabidhiwa na mtu mmoja ambaye ni mteja wake wa mkaa,”amesema
Amesema mteja huyo anajulikana kwa jina la Baba Geofrey na kwamba baada ya makabidhiano hayo alisema amemwaribu mwanafunzi huyo hivyo akae naye siku mbili akimtafutia sehemu ya kumpangia.
Hata hivyo Jeshi la Polisi mkoani humo kwa kushirikiana na kamati ya ulinzi lilipomuuliza binti huyo iwapo anahitaji kwenda shule, alidai yupo tayari isipokuwa apelekwe shule nyingine.
“Nikipelekwa shule nyingine nitakuwa tayari kuingia darasani kusoma ila siyo shule niliyokuwa nasoma na naomba walimu wabadilike” amesema
Hata hivyo mkuu wa mkoa huo ameahidi kumpeleka kwenye shule yeyote aendelee kusoma.
Homela ameeleza kuwa katika vipimo vya awali walivyofanya havijaonesha kama anaujauzito, na wanatarajia kufanya vipimo vingine.
“Ikibainika kwamba anaujauzito itatakiwa abaki nyumbani hadi ajifungue kisha arudi shuleni kuendelea na masomo,”amesema
Homela amesema Jeshi la Polisi linaendelea na uchungu ikiwamo kumtafuta Baba Geofrey.
Mwanafunzi huyo amepatikana ikiwa ni siku moja tangu Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kutoa maagizo kwa mkuu wa mkoa huo kufanya uchunguzi wa tukio hilo.