Mwanafunzi afariki akidaiwa kuchwapwa, kukanyagwa kichwani na mwalimu

Muktasari:
- Mwanafunzi wa kike wa kidato cha pili katika Shule ya Sekondari Mwasamba Wilaya ya Busega Mkoa wa Simiyu, Mhoja Maduhu (18) amefariki dunia baada ya kudaiwa kuchapwa viboko 10 na kukanyagwa kichwani na mwalimu wake.
Simiyu. Mwanafunzi wa kike wa kidato cha pili katika Shule ya Sekondari Mwasamba iliyopo wilayani Busega Mkoa wa Simiyu, Mhoja Maduhu (18) amefariki dunia baada ya kudaiwa kuchapwa viboko 10 na kukanyagwa kichwani na mwalimu wake.
Tukio hilo limetokea Februari 26,2025 baada ya mwalimu huyo kutoa kazi ya vikundi kwa wanafunzi wa darasa hilo, ambapo baadhi yao hawakuifanya akiwemo marehemu.
Emanuel Mapengo ni mwanafunzi wa kidato cha pili shuleni hapo amesema kuwa wanafunzi ambao hawakufanya kazi hiyo walitolewa nje ya darasa na kupewa adhabu ya kupiga magoti kabla ya kuanza kuchapwa viboko 10 kila mmoja.
“Tulipotoka nje tukapiga magoti walianza wanafunzi wasichana kisha na sisi wanafunzi wa kiume tukapiga magoti, halafu mwalimu akaanza kutuchapa viboko 10 kila mmoja.”
“Alipofika kwa mwanafunzi Mhoja Maduhu akampiga hizo fimbo kichwani na mgongoni na baadaye mwanafunzi mwenzetu alianguka chini na mwalimu akaagiza wanafunzi wamwigize darasani na kumlaza sakafuni,”amesema.
Naye Paul Ndiana ambaye ni mwanafunzi wa darasa hilo ameeleza kuwa mara baada ya mwalimu huyo kumkuta mwanafunzi huyo akiwa anaendelea kulia huku amelala sakafuni na kumsihi anyamaze lakini alimkanyaga kwa mguu.
“Mwalimu aliingia darasani na kumkuta Mhoja anaendelea kulia akamwambia anyamaze lakini aliendelea kulia tu ndipo alipomkanyaga kichwani kwa kutumia mguu,”amesema.
Mara baada ya tukio hilo hali ya mwanafunzi huyo ilikuwa mbaya na walimu wa shule hiyo walimkimbiza katika Hospitali ya Mkula kwa ajili ya kupata matibabu, lakini walipomfikisha ilibainika ya kuwa amefariki dunia.
Wazazi wa Mwanafunzi huyo walifika katika hospitali hiyo baada ya kupata taarifa ya kuwa mtoto wao amefariki.
“Mtoto baada ya kuadhibiwa kwa adhabu kali na hali yake kuwa mbaya alikimbizwa katika Hospitali ya Mkula lakini alipofikishwa ilibainika ya kuwa amefariki dunia na walimu hao walielekezwa wampeleke chumba cha kuhifadhia maiti na kisha kuondoka,”amesema
Samwel Maduhu ambaye ni baba mdogo wa mwanafunzi huyo.
Mama mzazi wa mwanafunzi huyo, Luli Dotto amesema baada ya kupata taarifa ya kuwa mwanaye yuko katika Hospitali ya Mkula baada ya kupewa adhabu na mwalimu wake na muda si mrefu akaelezwa ya kuwa amefariki dunia.
“Kabla sijakwenda hospitali zikaja taarifa nyingine kuwa mwanangu amefariki kwa ugonjwa wakati hakuwa na ugonjwa wowote,”amesema.
Willison Maduhu ni baba wa marehemu ameeleza hawakukubaliana na chanzo cha kifo cha mtoto wao na kuomba uchunguzi ufanyike katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Ziwa Bugando.
“Uchunguzi wa kifo cha mwanangu kweli ulifanyika katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Ziwa Bugando na kubainika kuwa kifo hicho kimetokana na kuvia kwa damu kichwani kwenye ubongo na hii inaonyesha kuwa mwanafunzi alipata adhabu kali baada ya kukanyagwa kichwani na mwalimu wake.”
“Niiombe Serikali ichukue hatua kwa walimu wote waliohusika na tukio hili ili kukomesha matukio hayo ambayo yamekuwa yakijitokeza kwa walimu kutofuata utaratibu wa utoaji wa adhabu ya viboko na kusababisha mauaji na ulemavu kwa baadhi ya wanafunzi,”amesema.
Mwenyekiti wa kijiji cha Lutubiga, Dwasi Machai amekiri kuwa tukio hilo si la mara ya kwanza kwenye shule hiyo, kwani walishawaonya walimu juu ya utoaji adhabu ambazo hazifuati utaratibu uliowekwa wa utoaji wa adhabu hasa ya viboko.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Simiyu, Kamishina Msaidizi wa Polisi (ACP) Sunday Songwe amesema kuwa tayari wameshamshikilia mwalimu huyo kwa hatua zaidi za kisheria.