Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mwamposa: Sikuja kwenye huduma kutafuta pesa

Mtume Boniface Mwamposa 'Buldoza'. Picha na Mtandao

Muktasari:

  • Azungumzia maisha yake na picha iliyowahi kusambaa kwenye mitandao ya kijamii ikimuonyesha alivyokuwa zamani

Dar es Salaam. Mtume Boniface Mwamposa 'Buldoza' wa Kanisa la Inuka Uangaze amesema hakuingia kwenye huduma hiyo ili kutafuta pesa.

Amesema kuna watu wengi wanafikiri furaha yake ni pesa na magari, lakini hata vikiondoka bado moyo wake upo kwa Mungu.

Ametoa kauli hiyo leo Julai 21, 2024 katika ibada ya Jumapili iliyoambatana na kongamano lenye jina la ‘Maisha ya kuingia kwenye furaha isiyo na kikomo.’

Takribani wiki mbili zilizopita Mwananchi ilichapisha ripoti maalumu ikieleza namna baadhi ya manabii na mitume wanavyojitengenezea ukwasi kupitia waumini wakiwauzia maji, mafuta, chumvi na vitambaa.

Mbali ya ripoti hiyo ya Mwananchi, kwenye mitandao ya kijamii kumekuwa na mijadala ikihusisha huduma zinazotolewa na mitume na manabii hao.

Akizungumza katika kongamano hilo lililofanyika Kawe, jijini Dar es Salaam, Mwamposa amesema furaha yake si pesa kama wengi wanavyodhani.

"Kuna watu wanatafuta hela wakifikiri furaha yao inatokana na pesa, sina maana msifanye kazi, nataka nibadilishe chanzo cha furaha yako,” amesema akizungumza na waumini.

"Nataka nikupe mbinu ambayo sisi watu wa Mungu tunawashinda watu wa kidunia, Yesu alisema tafuteni kwanza ufalme wa Mungu, hakuwaambia wasifanye kazi bali alikuwa anabadilisha chanzo wanachodhani kinawapa furaha," amesema Mwamposa ambaye pia alizungumzia maisha yake na picha iliyowahi kusambaa kwenye mitandao ya kijamii ikimuonyesha alivyokuwa zamani.

"Niliona watu siku moja wamerusha picha yangu, wakasema hivi ndivyo Mwamposa alivyoingia mjini. Niwaambie waache stori za mitandao, ukiangalia pale (hiyo picha) nilikuwa tayari nilishaanza huduma,” amesema.

Amesema watu wanalinganisha alivyokuwa, lakini hawajui wakati huo alikuwa wapi na aliacha vyote ndipo Mungu akaanza kumuinua.

"Sikuingia kwenye huduma hii kutafuta hela, ningekuja kutafuta hela hata leo hii nisingekuwa hapa,” amesisitiza.

Amesema Mungu alipomuita kwenye huduma ya utume, wengi walihoji kwa nini Buldoza anafanikiwa, wakizungumzia pesa na magari ambavyo amesema hata vikichukuliwa chanzo chake cha furaha ni kwa Mungu.

"Ukikutana na watu wanasema Buldoza amefanikiwa magari yamejaa, waambie hayo (magari) unayoona ni tone tu yapo mengi yatakuja," amesema.

Mwamposa aliwaita waumini kushuhudia baraka walizopata baada ya mkesha uliofanyika wiki iliyopita akisisitiza hakuna anayepangwa kushuhudia kama ambavyo wengi huwa wanafikiri.

Kuhusu umati kwenye ibada zake, amesema hakuna mtu alitumwa kwa mtutu wa bunduki aende kwa Mwamposa, akisisitiza wanaofika kanisani hapo si kwa nguvu yake (Mwamposa) ni kwa nguvu ya Mungu.

Amesema amewahi kuwashushua waandishi wa habari ambao siku moja walimuuliza alivyoweza kuujaza Uwanja wa Taifa wakimlinganisha na watu wengine, akawataka wasimlinganishe na kanisa, mtumishi au timu fulani.

"Wanaonilinganisha wanafanya makosa, sifanyi kazi hii kushindana na mtumishi fulani au timu yoyote bali kwa neema niliyopewa,” amesema.