Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mvua yakata mawasiliano ya usafiri Kilimanjaro na Arusha

Haya ni baadhi ya mabasi yanayofanya safari zake mikoa mbalimbali ya Tanzania ambapo yameshindwa kuendelea na safari baada ya kukatika kwa mawasiliano ya barabara katika eneo la Kwa Msomali Wilaya ya Hai, mkoani Kilimanjaro kutokana na mto Biriri kujaa maji na kusababisha mafuriko katika eneo hilo ambapo huduma za usafirishaji zilisimama kwa muda.

Muktasari:

  • Mawasiliano kati ya Mkoa wa Kilimanjaro na Arusha yamekatika asubuhi ya leo Jumanne Aprili 25, 2023  baada ya maji kujaa barabarani katika eneo la Kwa Msomali wilayani Hai mkoani Kilimanjaro.

Hai. Mawasiliano kati ya Mkoa wa Kilimanjaro na Arusha yamekatika asubuhi ya leo Jumanne Aprili 25, 2023  baada ya maji kujaa barabarani katika eneo la Kwa Msomali wilayani Hai mkoani Kilimanjaro.

Mabasi na magari mbalimbali yaliyoathirika na adha hiyo ni yale yanayotokea Arusha kwenda Kilimanjaro kuelekea Mikoa ya Dar es salaam na yale yanayotokea Kilimanjaro kwenda Arusha na maeneo mengine

Tangu asubuhi magari yameshindwa kupita katika eneo hilo baada ya mto Biriri kujaa maji na kusababisha mafuriko na kupelekea kukatika kwa mawasiliano ya barabara.

Mkuu wa Kitengo cha Usalama Barabarani mkoani Kilimanjaro (RTO), Pili Misungwi amewatahadharisha madereva wanaopita katika maeneo hayo na kuwataka kuwa watulivu na wavumilivu kwa muda huu mpaka hali itakapokaa sawa.

"Tunawatahadharisha watumiaji wa barabara hii toka Hai kuja Moshi na wanaotoka Moshi kwenda Hai kuwa watulivu, pia wawe na subira, tukumbuke maji ni hatari na hayajaribiwi,"amesema

Hali ilivyo Arusha

Mvua zilizonyesha usiku kucha maeneo mbalimbali ya mikoa ya Arusha na Manyara zimesababisha mafuriko ya maji yaliyofunika barabara ya Arusha-Moshi na kusababisha magari kushindwa kupita.

Leo Aprili 25 kuanzia majira ya saa 12 asubuhi hadi kufikia saa nne asubuhi magari yalishindwa kupita katika meneo ya Palestina jirani la uwanja wa ndege wa kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), maeneo ya Hai na Siha, King'ori wilaya ya Arumeru, huku mengine yakipita kwa zamu chini ya uangalizi wa polisi.

Hata hivyo, baadhi ya wakazi wa maeneo hayo, wameitaka Serikali kujenga madaraja katika barabara hiyo kwani tangu mwaka 2019 imekuwa ikikubwa na mafuriko.

Akizungumza na Mwananchi, Peter Mtungi mkazi eneo la Mijohoroni Hai, ameomba serikali kuboresha barabara kwa kuongeza madaraja katika barabara ya Moshi-Arusha.

"Hii shida imekuwa ikitokea kila wakati wa mvua na mwaka 2019 magari yalianguka hapa, hivyo tunaomba Serikali kuongeza madaraja," amesema.

Naye Joseph Mombo mkazi wa Siha akiwa katika barabara hiyo, ameishauri Serikali kuongeza kalavati katika Maeneo ya barabara hiyo Ili kuondoa adha ya magari kukwama.

Baadhi ya magari yakiwa yamekwama barabara ya Moshi-Arusha leo. Picha na  Mussa Juma

Mombo amesema mvua hizo licha ya kuzuia magari pia makazi ya watu maeneo ya Rundugai, Relini na Stesheni yamezingirwa na maji.

"Kutokana na Maji kutofata mkono Sasa yameingia katika makazi ya watu, hivyo ni vyema barabara kuboresha Ili maji yarudi kwenye mkondo wake," amesema.

Kamanda Polisi mkoa Arusha, Justin Masejo amewataka wakazi wa Arusha wakiwepo madereva kuchukuwa tahadhari kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha.

Amesema uchunguzi wa athari za mvua bado unaendelea.

Mkuu wa Mkoa Arusha, John Mongella pia amewataka wakazi wa Arusha kuchukuwa tahadhari, kwani tayari Mamlaka ya hali ya hewa (TMA) ilitoka utabiri mwaka huu uwepo wa mvua kubwa lakini zitakuwa za muda mchache.