Mvua kubwa mikoa 14 kuanza Aprili 12

Wakazi wa Kata ya Kihonda na Lukobe Manispaa ya Morogoro wakishika kamba, ili wavushwe na Askari wa Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji baada ya Barabara ya Mazimbu, eneo la 'Kwa bwanajela' kujaa maji kutokana na mvua iliyonyesha Jumanne, Januari 30, 2024 . Picha na Maktaba
Muktasari:
Mikoa 14 ya Tanzania bara na visiwani kuanzia Aprili 12 kutakuwa na mvua kubwa kwa mujibu wa utabiri wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA)
Dar es Salaam.Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetabiri uwepo wa mvua kubwa katika mikoa 14 ya Tanzania bara na visiwani kuanzia Aprili 12 mwaka huu.
Utabiri huo umetolewa leo Aprili 10,2024 na TMA, mvua zinategemewa kunyesha kwenye maeneo ya Mkoa wa Dar es salaam, Tanga, Morogoro, Pwani Lindi, Mtwara, Rukwa, Iringa, Mbeya, Songwe, Njombe, Ruvuma na visiwa vya Unguja na Pemba.
“Athari zinazotegemewa ni mafuriko na kuathirika kwa shughuli za kiuchumi katika maeneo hayo,” meandikwa kwenye taarifa hiyo.
Aprili 13, TMA imesema mikoa ya Dar es Salaam, Tanga, Morogoro, Pwani, Lindi na Mtwara pamoja na Unguja na Pemba zitashuhudia mvua kubwa.
Baadhi ya maeneo ya Mkoa wa Iringa, Njombe na Ruvuma yanapaswa kuchukua tahadhari kwani mvua kubwa inatarajiwa kunyesha.
Siku ya Aprili 14, Mkoa wa Dar es Salaam, Tanga, Morogoro, Pwani Lindi na Mtwara na visiwa vya Unguja na Pemba zitakuwa na mvua kubwa huku athari zitakazotokea zikitajwa kuwa ni mafuriko na shughuli za kiuchumi kuathirika.