Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mvua yaua 15 ndani ya siku saba Tanzania

Muktasari:

  • Watu 15 wafariki dunia, huku watoto wakiwa 12 baada ya kusombwa na maji ya mvua zinazoendelea kunyesha maeneo mbalimbali nchini.

Dar es Salaam. Watu 15 wamefariki dunia kutokana na kusombwa na maji ya mvua zinazoendelea kunyesha maeneo mbalimbali nchini.Takwimu hizo zimetolewa na Jeshi la Polisi nchini ambalo limesema baadhi yao wamefariki wakiwa wanaogelea, wengine wakiwa wanavuka maeneo ambayo maji yanatiririka kwa kasi na wengine kutokana na kutumbukia kwenye mashimo au madimbwi yaliyojaa maji.

“Miongoni mwa watu hao watoto ni 12 na watu wazima ni watatu,” imeeleza taarifa ya jeshi hilo iliyotolewa leo Aprili 8, 2024, huku ikibainisha vifo hivyo vimetokea ndani ya siku saba pekee kuanzia Aprili mosi, 2024 hadi Aprili 7, 2024.

Taarifa hiyo imeyataka maeneo yalipotokea vifo hivyo kuwa ni wilaya ya Kalambo (Rukwa), wilaya ya Kilwa (Lindi), wilaya ya Ludewa (Njombe), wilaya ya Muheza (Tanga), wilaya ya Kibaha na Mkuranga (Pwani), wilaya ya Babati (Manyara), Wilaya ya Kyela (Mbeya) na mkoani Geita.Aidha, kutokana na vifo hivyo, Jeshi la Polisi limeendelea kutoa wito na tahadhari kwa watu wote, hususan wazazi na walezi kuwalinda watoto kwa karibu na kuwapa maelekezo sahihi kutokana na mvua hizi zinazoendelea kunyesha.

“Pia, viongozi wa Serikali za mitaa, walimu shuleni, viongozi wa dini tuendelee kuelimisha watoto wetu kujihadhari na maji yaliyotuama au yanayotembea na wala wasishindane na maji ya mvua yanayotiririka, kwani ni hatari kwa maisha yao,” limetahadharisha Jeshi la Polisi.