Muuguzi auawa kwa kuchomwa kisu, muuaji adaiwa kujinyonga

Muktasari:
- Muuguzi wa Zahanati ya Kijiji cha Malembeka wilayani Bunda, Mkoa wa Mara amefariki dunia baada ya kuchomwa kisu na mtu anayesemekana kuwa ni mpenzi wake kisha naye muuaji kufariki dunia baada ya kujinyonga na kwa kutumia shuka.
Bunda. Muuguzi wa Zahanati ya Kijiji cha Malembeka kilichopo wilayani Bunda, Mkoa wa Mara, Zawadi Kazi (31) amefariki dunia baada ya kuchomwa na kisu sehemu mbalimbali za mwili wake na mtu anayedhaniwa kuwa ni mpenzi wake kwa kile kinachelezwa ni ugomvi wa kimapenzi.
Baada ya kufanya tukio hilo mtuhumiwa huyo alikimbilia kusikojulikana hata hivyo mwili wake kukutwa ukiwa unaning'inia kwenye mti akiwa amefariki dunia kwa kujinyonga.
Akizungumza kwa njia ya simu, Mwenyekiti wa Kijiji cha Malembeka, Ramadhani Sarima amesema muuguzi huyo aliuawa jana Mei Mosi 2025 saa 4 usiku kijijini hapo na kumtaja mtuhumiwa wa tukio hilo kuwa ni Ndege Makebe (31) mkazi wa kijiji hicho.

Muuguzi Zawadi Kazi akiwa kwenye maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani jana Mei mosi, 2025 muda mfupi kabla ya kuuawa.
"Nesi alichomwa zaidi ya visu kumi katika maeneo mbalimbali ikiwepo shingoni, tumboni, ubavuni upande wa kulia na kushoto na kwenye matiti yote mawili na kusababisha kuvuja damu nyingi sana," ameeleza
Akieleza namna tukio lilivyotokea, Sarima amesema mbali na kuwa ni muuguzi katika zahanati ya kijiji hicho, pia alikuwa akimiliki duka la dawa kijijini hapo ambapo alikuwa na utaratibu wa kwenda dukani kwake baada ya kumaliza majukumu yake katika zahanati.
Amesema jana baada ya kufunga duka, muuguzi huyo alipanda bodaboda kwa ajili ya kwenda nyumbani kwake na alipofika alimkuta mtuhumiwa akiwa amesimama nje karibu na mlango jambo ambalo lilimpa wasiwasi hivyo kumuamuru bodaboda waondoke katika eneo hilo.
"Wakati bodaboda anageuza pikipiki kwa ajili ya kuondoka, Ndege aliwahi kabla pikipiki haijawaka kisha akaanza kumchoma nesi kwa kisu sehemu mbambali za mwili wake na kusababisha majeraha kisha alianguka," ameeleza.
Amesema baada ya wananchi kupata taarifa, walifika eneo la tukio kwa ajili ya kutoa msaada lakini kutokana na majeraha na kuvuja damu, muuguzi huyo alifariki dunia papo hapo.
Sarima amesema mwili wa muuguzi huyo umehifadhiwa katika Kituo cha Afya Mugeta kwa ajili ya taratibu zingine.

Ndege Makebe enzi za uhai wake.
Ameeleza kuwa leo Ijumaa Mei 2, 2025 saa 1 asubuhi mwili wa mtuhumiwa umekutwa ukiwa unaning'inia kwenye mti kijijini hapo baada ya kujinyonga kwa kutumia shuka.
"Hivi tunavyoongea nipo eneo la tukio na mwili bado uko juu ya mti, tunawasubiri polisi waje waushushe kwani tayari tumetoa taarifa na wamesema wanakuja," amesema.
Sarima amesema katika enoe la tukio hilo wamekuta vitu kadhaa ikiwemo kofia ya muuguzi aliyokuwa amevaa jana kabla ya tukio, kisu chenye damu ambacho kinaaminika kilitumika kumjeruhi muuguzi pamoja na kofia ya marehemu Makebe.
Amesema wawili hao awali walikuwa na mahusiano ya kimapenzi lakini miezi mitano iliyopita walikuwa na ugomvi uliosababisha muuguzi huyo kuamua kuachana na mpenzi wake uamuzi ambao Makebe hakukubaliana nao.
Amesema katika kipindi hicho Makebe amekuwa akijribu kurudiana na mpenzi wake bila mafanikio hadi kufikia hatua ya kutishia kumuua.
"Nimeambiwa Makebe alifikia hatua ya kumtumia nesi ujumbe kuwa endapo hatarudiana naye basi atamuua mwisho wa siku ameamua kumuua kweli," amesema.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Pius Lutumo amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na amesema polisi wako njiani kuelekea katika eneo la tukio.
"Ni kweli kuna hayo matukio yametokea jana usiku, nesi aliuawa kwa kuchomwa na kitu chenye ncha kali na muda huu mwili wa mtuhumiwa umekutwa ukining'inia juu ya mti kwa sasa vijana wanaelekea eneo la tukio na uchunguzi umeanza," amesema Lutumo.