Kisa wivu amuua mwanaye, naye ajinyonga hadi kufa

Muktasari:
- Mkazi wa kijiji cha Uria Wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro, Elifuraha Mlay (23) amemuua mwanaye mwenye umri wa miezi tisa na kisha mwenyewe kujinyonga hadi kufa.
Moshi. Mkazi wa kijiji cha Uria Wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro, Elifuraha Mlay (23) amemuua mwanaye mwenye umri wa miezi tisa na kisha mwenyewe kujinyonga hadi kufa.
Akizungumza leo Alhamisi Aprili 29, 2021 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Amon Kakwale amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kuongeza kuwa marehemu alikuwa na mpenzi wake waliyekuwa wakiishi pamoja, Loveless Msemwa (19).
“Tukio hili limetokea usiku wa kuamkia jana marehemu alimuua mtoto wake Elikarimu na baada ya kumuua mwanaye na yeye alijiua kwa kujinyonga kwa kutumia chandarua aliyoifunga kwenye mti nje ya nyumba aliyokuwa akiishi.”
"Chanzo cha tukio hili bado kinachunguzwa lakini inasemekana ni wivu wa mapenzi baina ya marehemu na Loveness waliyekuwa wakiishi pamoja,” amesema kamanda huyo.