Mume mbaroni tuhuma za kumchinja mkewe Mbeya

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Benjamin Kuzaga
Muktasari:
- RPC Kuzaga amesema taarifa za awali zimeeleza kabla ya umauti kumkuta Happyness uliibuka ugomvi kati ya wanandoa hao waliokuwa wakiishi kitongoji cha Masista Kijiji cha Lusese wilayani Mbarali.
Mbeya. Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linamshikilia Ombeni Kilawa (43) mkazi wa Kijiji cha Lusese kata ya Igurusi wilayani Mbarali kwa tuhuma za mauaji ya mkewe Happyness Mwinuka(40) kwa kumkata na kisu shingoni .
Kamanda wa polisi mkoani Mbeya, Benjamin Kuzaga ameyasema hayo leo Alhamisi Machi 14, 2024 na kwamba tukio hilo limetokea Machi 13 mwaka huu.
RPC Kuzaga amesema taarifa za awali zimeeleza kabla ya umauti kumkuta Happyness uliibuka ugomvi kati ya wanandoa hao waliokuwa wakiishi kitongoji cha Masista Kijiji cha Lusese wilayani Mbarali.
Kuzaga amesema baada ya ugomvi huo kudumu kwa dakika kadhaa ndani ya nyumba wanaoishi, ndipo mtuhumiwa alichukua kisu na kumkata mke wake shingoni na kumsababishia umauti .
Imeleezwa kuwa uchunguzi wa awali umebaini chanzo cha tukio hilo ni wivu wa kimapenzi baada ya mtuhumiwa kumhisi na kumtuhumu mke wake kuwa na uhusiano wa kimapenzi na wanaume wengine.
Kamanda Kuzaga ametoa wito kwa jamii hususan wanandoa kuwa wawazi inapojitokeza migogoro ya kiuhusiano, ili kuepuka na matukio ya kuchukua sheria mikononi kwa kufanya mauaji na kuacha familia zikihangaika.
“Viko vituo vya Polisi na madawati ya kijinsia ambapo mnaweza kupeleka malalamiko yakatolewa maamuzi ikiwa ni pamoja na kupewa ushauri, kufanya mauaji sio suluhisho,”amesema.
Hata hivyo baadhi ya wananchi wamesema matukio hayo yameshika kasi na kuomba Jeshi la Polisi kufanya kazi ya ziada kutoa elimu maeneo mbalimbali ili kusaidia kupunguza matukio ya mauaji.