Prime
Mume aliyefumwa ‘akichat‘ usiku wa manane alivyomuua mkewe kwa kumlipua kwa mafuta ya taa

Dar es Salaam. Ni simulizi inayoweza kukutoa machozi kutokana na namna mume aliyefumwa na mkewe ‘akichat’ usiku wa manane, alivyomuua mkewe kwa kumwagia mafuta ya taa kisha kumlipua ambapo mwili uliungua kwa asilimia 62.
Mahakama Kuu, masjala ndogo ya Dar es Salaam, imemuhukumu Yusuph Omary Seleman, kunyongwa hadi kufa baada ya kumtia hatiani kwa kosa la kumuua kwa kukusudia, mkewe Judith Patrick Kiza kwa kumwagia mafuta ya taa na kumchoma.
Tukio hilo lililotokea Aprili 16, 2023 huko eneo la Kidubwa Vikindu, wilaya ya Mkuranga mkoa wa Pwani, baada ya kuibuka ugomvi baina ya wanandoa hao. Ugomvi huo ulitokea baada ya mke kumfuma mumewe ‘akichat’ kwa simu usiku wa manane.
Katika hukumu yake aliyoitoa Aprili 11, 2025 na kupakiwa katika tovuti ya mahakama leo Jumatatu Aprili 14, 2025, Jaji Awamu Mbagwa alisema ushahidi wa mazingira wa Jamhuri, unamlenga mshtakiwa kuliko mtu mwingine yeyote.
Jaji Mbagwa alisema utetezi wa mshtakiwa kuwa mkewe alijilipua mwenyewe kwa kujimwagia mafuta ya taa kutokana na wivu wa mapenzi ulikuwa ni dhaifu, na Mahakama imethibitisha ni mshtakiwa aliyesababisha kifo hicho kwa nia ovu.
Lakini Jaji alisema hata matendo ya mshtakiwa baada ya tendo hilo kwa kushindwa kwenda kumuona mkewe akiwa amelazwa hospitali akipigania uhai, yanathibitisha kuwa alikuwa akijishtukia kuwa ni mwenye hatia.
Tukio lilivyotokea
Mshtakiwa na marehemu walifunga ndoa mwaka 2018 na kubarikiwa kupata mtoto mmoja, Nasra Yusuph.
Kupitia ushahidi wa shahidi wa sita wa Jamhuri, WP 8639 Koplo Margaret na maelezo ya marehemu aliyoyatoa akiwa hospitalini Aprili 16, 2023, unaeleza kuwa siku hiyo saa 7:00 usiku alimka na kumkuta mumewe ‘anachat’ kwenye simu.
Kulingana na ushahidi huo, marehemu alimshuku mumewe alikuwa ‘akichat’ na mchepuko wake na hivyo akamtaka mumewe amweleze alikuwa akiwasiliana na nani usiku huo, kitendo ambacho hakikumpendeza mumewe na ugomvi ukaibuka.
Usiku huo ndani ya nyumba yao, walikuwa wametembelewa na mama wa mshtakiwa aitwaye Zainabu Abdalah Kilungu na akiwa amelala kitandani kwake, mama huyo alisikia kelele za kugombana kati ya marehemu na mshtakiwa.
Mama huyo alimka na kwenda katika chumba cha mwanaye lakini hakuweza kutoa msaada wowote na kutokana na kukerwa na tuhuma hizo za usaliti, mshtakiwa alianza kumpiga vibaya mkewe na baadaye kummwagia mafuta ya taa na kumuunguza.
Marehemu alianza kuungua huku akipiga mayowe ya kuomba msaada na akimwita jirani yake aitwaye Nimaka Salim, ambaye katika ushahidi wake alieleza kusikia akiitwa lakini alishindwa kutoka akiamini wamevamiwa na majambazi.
Baadaye Nimaka aliyekuwa shahidi wa saba, alisikia sauti ya mshtakiwa akifungua geti na hapo ndio alipata ujasiri wa kwenda kwenye nyumba ya mshtakiwa akiwa na majirani wengine na kushuhudia majeraha ya moto kwa marehemu.
Wakati huo marehemu alikuwa katika hali mbaya kutokana na majeraha ya moto kiasi kwamba hawakupata nafasi hata ya kuuliza kiini cha kuungua vile, kwani dhamira yao ilikuwa ni kumuwahisha haraka hospitali iliyo jirani.
Mshtakiwa aliwasha gari lake na kumbeba mkewe na kusindikizwa na majirani wawili, mama wa mshtakiwa na mtoto wa marehemu aitwaye Nasra ambapo walimwahisha hospitali ya Saint Vicent ambako alipokelewa na kulazwa.
Mshtakiwa alivyodanganya Polisi
Baada ya marehemu kupokelewa hospitalini hapo, daktari aliyempokea mgonjwa alimshauri mshtakiwa akachukue fomu namba tatu ya Polisi (PF3) kwa ajili ya mkewe ili waweze kuendelea na matibabu, kwani takwa la PF3 ni la kisheria.
Msitakiwa akamwacha mkewe hospitali akiendelea na matibabu na kwenda kituo cha Polisi Vikindu ambapo aliwaeleza shahidi wa nne na nane kuwa mkewe alipata ajali kwa kuungua na maji ya moto wakati akipika daku.
Mashahidi hao, Sajenti Paschal na Koplo Emmanuel walimpa fomu hiyo lakini baadaye machale yaliwacheza (walishuku jambo) wakaamua kufutilia tukio hilo, ambapo walifika hadi hospitali ya Saint Vincent alikolazwa marehemu.
Huko walifanikiwa kufanya mahojiano na daktari aliyemuhudumia mgonjwa pamoja na mgonjwa mwenyewe, ambapo marehemu akafunguka mwanzo mwisho kuhusu nini kilitokea na kuwa ni mumewe ndiye aliyemuunguza kwa mafuta ya taa.
Halikadhalika daktari aliyekuwa amemuhudumia mwanamke huyo alimweleza Sajenti Paschal kwamba majeraha hayo ya moto yalitokana na moto na sio maji ya moto kama ilivyodaiwa na mume wa marehemu alipowaeleza.
Kutokana na maelezo hayo, mshtakiwa alikamatwa na usiku huohuo Polisi walikwenda kupekua nyumbani ambapo walifanikiwa kupata kipande cha nguo kilichoungua, chupa iliyokuwa na mafuta ya taa na kiberiti kilichotumika.
Mshtakiwa alifikishwa mahakamani kwa kosa la kujaribu kumuua mkewe ambaye wakati huo bado alikuwa akiendelea kupata matibabu, hadi Mei 15,2023 alipofariki dunia na hapo shitaka likabadilika kutoka kujaribu kuua hadi mauaji ya kukusudia.
Alivyojitetea mahakamani
Katika utetezi wake, alikiri kuwepo kwa ugomvi baina yake na marehemu siku hiyo ya tukio, lakini akakanusha kusababisha kifo cha marehemu na kudai kuwa badala yake marehemu alijilipua mwenyewe kutokana na wivu wa mapenzi.
Shahidi wake wa pili, Zainabu ambaye ni mama yake mzazi, alieleza siku hiyo usiku alimuona marehemu akitokea chumbani akiwa na hasira na baada ya kwenda stoo alichukua mafuta ya taa na kujimwagia.
Kisha akachukua kiberiti na kujilipua mafuta ya taa na kujiwasha kwa kiberiti na baada ya kujiwasha, aliendelea kumshikilia mtoto wake wa kike, Nasra akitamka maneno kuwa alikuwa anataka wafe pamoja.
Shahidi wa tatu, Yasin Ally ambaye ni mdogo wa mshtakiwa, alielezea namna alivyojulishwa juu ya tukio hilo na baada kuungana na mshtakiwa Hospitali ya Saint Vincent na kuthibitisha kuwa ndugu yake alikamatwa hospitalini hapo.
Hukumu ya Jaji
Katika hukumu yake, Jaji Mbagwa alisema ingawa utetezi katika wasilisho lao la mwisho wanapinga sababu ya kifo, shahidi wa kwanza na wa pili wa utetezi, walikubaliana na Jamhuri kuwa marehemu alikuwa na majeraha ya moto.
“Kwa msingi huo, hoja muhimu ya kuifanyia maamuzi ni kwamba je, ni mshtakiwa ndiye aliyesababisha kifo cha marehemu kwa kumuunguza kwa moto kama ambavyo upande wa mashitaka unadai?” alieleza Jaji Mbagwa.
“Nikiri kwamba upande wa mashitaka hauna ushahidi wa moja kwa moja katika kesi hii kwa maana kuwa hakuna shahidi wao hata mmoja aliyeshuhudia mshtakiwa akimuwasha kwa moto marehemu,”alieleza Jaji na kuongeza:-
“Ushahidi wao wote uliegemea katika ushahidi wa mazingira. Ni msimamo wa sheria kwamba hata ushahidi wa mazingira unakubalika mahakamani na unaweza kusababisha mshtakiwa au washtakiwa kutiwa hatiani kwa kosa la jinai”
Jaji alisema hakuna ubishi kuwa siku ya tukio, ndani ya nyumba ya mshtakiwa lilipotokea tukio kulikuwa na watu wanne, ambao ni mshtakiwa, marehemu, mama wa mshtakiwa pamoja na mtoto wa wana ndoa hao aitwaye Nasra.
“Swali la kujiuliza ni kuwa kama mshtakiwa sio aliyemuunguza marehemu, kwa nini alichukua muda mrefu kutoa msaada huku akishuhudia mkewe akiungua vibaya vile? Mama yake alisema marehemu alijiwasha mwenyewe”.
“Hata hivyo kwa haraka lazima niseme nimeuchukulia ushahidi huo kwa mashaka makubwa na niliupa uzito mdogo. Hii ni kwa sababu wakati anadodoswa ilibainika alikuwepo kwenye chumba cha mahakama shahidi wa sita akitoa ushahidi”
“Mbali na hivyo lakini mwonekano wake (demeanour) wakati akitoa ushahidi unaibua maswali. Wakati anaulizwa maswali ya dodoso (cross examination) alikuwa anapata wakati mgumu kujibu maswali ya kawaida kabisa”
Jaji alisema katika kuamua kesi hiyo, mahakama pia imeangalia matendo ya mshtakiwa ambapo mashahidi namba 4 na 8 walisema aliripoti kuwa mkewe ameungua na maji ya moto wakati akiandaa chakula aina ya daku.
“Ingawa mshtakiwa aliukataa ushahidi huu, lakini ninalazimika kuamini ushahidi huu wa upande wa mashitaka kwa vile hakuna ushahidi mwingine ulioletwa kuishawishi mahakama kwamba mashahidi hao walikuwa wanadanganya”
“Kama mshtakiwa hakuwa muhusika kama anavyotaka mahakama iamini, kwa nini walidanganya polisi kuhusu kiini cha majeraha ya moto? Hata matendo ya mshtakiwa baada ya kupewa dhamana yanaongea mambo mengi.”
“Katika ushahidi wake mwenyewe, alieleza mahakama kuwa baada ya kupewa dhamana hakuenda hospitali kumtembelea mkewe aliyekuwa mahututi kwa kuwaogopa ndugu zake kwa vile wanaamini yeye ndio muhusika”
Jaji alisema hiyo peke yake inaonyesha alifahamu ana hatia ya tukio hilo baya na alijua marehemu alikuwa amewaeleza ndugu zake nini kilichomtokea, na ndio maana akawa anajishuku na kuogopa kwenda hospitali.
Mbali na hilo, lakini Jaji alihoji sababu za marehemu kuomba msaada kutoka kwa jirani yao aitwaye Nimaka au Zuwena na kuhoji “Sasa kama kweli alijilipua mwenyewe, kwa nini hakuomba msaada kwa mshtakiwa pamoja na mama yake,”
Jaji alisema kama mshtakiwa angekuwa hana dhamira ovu ya kumuua marehemu angetoa msaada wakati anamuita jirani yake amsaidie na kama angefanya hayo, wala mkewe asingeungua vibaya.
“Kwa hiyo Mahakama inaona alikuwa ni nia ovu ya kutenda kosa hilo la mauaji”, alisema Jaji na kusema anamtia hatiani mshtakiwa na kumuhukumu adhabu ya kifo kwa kuwa kisheria, adhabu kwa kosa la kuua ni moja tu nayo ni adhabu ya kifo.