Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ahukumiwa kunyongwa kwa mauaji gesti

Muktasari:

  • Kwenye kitabu cha wageni gesti mshtakiwa Elia Wekwe alijitambulisha kwa jina la Juma Jackson ili kutimiza nia yake ovu.

Arusha. Elia Wekwe ametiwa hatiani na Mahakama na kuhukumiwa kunyongwa hadi kufa kwa kumuua Kulwa James katika nyumba ya kulala wageni.

Mauaji hayo yalifanyika Desemba 28, 2023 katika eneo la Unyanyembe, wilayani Maswa, Mkoa wa Simiyu.

Kwa mujibu wa ushahidi uliowasilishwa mahakamani, Elia aliwasiliana na Kulwa (marehemu) wakakubaliana kwenda kufanya mapenzi na kwamba atampa Sh50, 000, hivyo wakakutana kwenye nyumba ya kulala wageni iitwayo Siha.

Kwenye kitabu cha wageni imeelezwa Elia alijitambulisha kwa jina la Juma Jackson.

Kumbukumbu za ushahidi mahakamani zinaeleza Elia na dada yake, Konzela Wekwe walishtakiwa kwa kesi hiyo ya mauaji iliyosikilizwa na Mahakama Kuu Shinyanga, mbele ya Jaji Ruth Massam.

Jaji Massam alitoa hukumu ya kesi hiyo Aprili 8, 2025 baada ya kuridhika Elia alitenda kosa hilo na imemuachia huru Konzela.


Ilivyokuwa

Ilidaiwa mahakamani kuwa Desemba mosi, 2023 Elia alisafiri kutoka Kijiji cha Maliwanda wilayani Bunda mkoani Mara kwenda kumtembelea dada yake (Konzela) na wakapanga njama ya kumuua Kulwa.

Ushahidi unaeleza mshtakiwa alifika nyumba ya kulala wageni ya Kibo akajitambulisha kwa jina la Juma Jackson. Alikaa katika nyumba hiyo kwa siku tano hadi Desemba 28, 2023.

Ilidaiwa siku ya tukio alihamia nyumba ya kulala wageni ya Siha, akajiandikisha kwa jina la Juma Jackson. Akiwa hapo aliwasiliana na Kulwa wakakubaliana kufanya mapenzi kuwa atampatia Sh50, 000.

Ushahidi unaeleza Elia na Kulwa walikutana katika chumba namba nne na baada ya kitendo hicho, Kulwa alidai apatiwe fedha ndipo Elia alimuua kwa kumnyonga na kuuficha mwili uvunguni mwa kitanda, kisha akarudi Bunda.

Desemba 29, 2023 wakati mhudumu akifanya usafi aliona mwili huo akamjulisha mfanyakazi mwenzake aliyempigia simu kiongozi wa eneo hilo ambaye aliwajulisha polisi.

Askari kutoka Kituo cha Polisi Maswa walifika wakauchukua mwili wa marehemu na baada ya uchunguzi ilibainika chanzo cha kifo ni kukosa hewa baada ya kunyongwa shingo.

Katika upelelezi washtakiwa wawili walikamatwa kwa nyakati tofauti na kuhojiwa na Elia alikiri kula njama na dada yake kumuua mke mwenzake Kulwa, kwa madai alikuwa chanzo cha kutoelewana kati ya Konzela na mume wao.

Wakati wa usikilizwaji wa kesi, upande wa mashtaka ulikuwa na mashahidi saba na vielelezo sita.

Shahidi wa kwanza, Venance Magorio, mume wa marehemu alidai mwaka 2023 alikuwa akiishi na Kulwa (marehemu) baada ya kuachana na mkewe wa kwanza (Konzela) kwa sababu alikuwa mzee.

Alidai siku ya tukio alitoka nyumbani kwenda kutafuta dawa na alimuacha mkewe na watoto lakini aliporudi hakumkuta. Alipowauliza watoto walisema mama yao amekwenda kununua mahindi.

Alieleza baada ya saa kadhaa kupita alimpigia simu lakini haikupatikana kwa kuwa ilikuwa imezimwa. Siku iliyofuata alikwenda kuuliza kwa dada yake, ambaye alisema hajamuona.

Akiwa njiani kurudi nyumbani, alikutana na mwanamke aliyemuarifu aliwaona polisi wakiwa wamebeba mwili wa mkewe aliyefariki dunia kutoka nyumba ya wageni ya Siha.

Alidai aliwasiliana na shemeji yake wakaenda Kituo cha Polisi Maswa, kisha mochwari kuutambua mwili.

Alidai Januari mosi, 2024, ulifanyika uchunguzi wa mwili wa marehemu baadaye akapewa kibali cha kwenda kuzika. Alidai Kulwa na Konzela hawakuwa na mzozo.

Shahidi wa pili, mhudumu wa nyumba ya kulala wageni ya Siha, Allen William alisema siku ya tukio akiwa kazini alimpokea mgeni, Juma Jackson aliyempatia chumba namba nne na akalipwa Sh5,000.

Alidai mgeni huyo alimuuliza iwapo kuna mlango wa nyuma naye akamjibu hakuna, kisha akaendelea na shughuli zake.

Shahidi alidai Desemba 29, 2023 akiwa kazini, mfanyakazi mwenzake, Mary alimjulisha kuwa alipokuwa akifanya usafi alikuta mwili wa mtu uvunguni, hivyo alitoa taarifa polisi wakafika kuuchukua.

Januari 8, 2024 alipigiwa simu na polisi akitakiwa Kituo cha Polisi Bariadi kwenye gwaride la kumtambua mtuhumiwa, ambako alimtambua Elia.

Shahidi wa tatu, Dk Bwire Robert aliyeufanyia uchunguzi mwili wa Kulwa alisema alibaini shingo ilikuwa na alama, jicho la kulia lilikuwa na damu iliyoganda. Chanzo cha kifo alisema ni kukosa hewa kwa sababu ya kunyongwa.

Shahidi wa nne, Inspekta Mahoho aliieleza mahakama Januari 9, 2024 aliendesha gwaride na utambulisho likihusisha watu tisa na kwamba, shahidi wa kwanza alimtambua Elia aliyekuwa wa tatu kutoka kulia. Shahidi wa pili pia alimtambua katika gwaride hilo.

Shahidi wa tano, Sajenti Enock alidai mtuhumiwa alipohojiwa alikiri kumuua Kulwa ambaye alijulikana kwa jina lingine la Rebeca James.

Alidai mshtakiwa aliwapeleka polisi eneo la tukio ambako alijiandikisha kwa jina la Juma Jackson, sawa na kwenye nyumba ya Kibo.

Alidai walichukua vitabu hivyo na pia walifanya ufuatiliaji wa mawasiliano ya simu ikabainika Desemba 28, 2023 mshitakiwa wa pili aliwasiliana na Kulwa. Mshtakiwa wa kwanza baada ya kuhojiwa alikiri kuhusika na mauaji hayo.

Konzela katika utetezi wake alisema alikuwa mke wa Venance Magorio, mume wa Kulwa lakini uhusiano wao uliisha mwaka 2019 baada ya  mume kuwa mlevi na kumpiga.

Alisema alikamatwa Januari 5, 2024 kwa tuhuma za mauaji na kutakiwa awapeleka askari kwa Juma Jackson ambaye hakumfahamu.

Alipoulizwa ana kaka wangapi, alijibu wanne na kati yao watatu wako nchini Kenya na mmoja Tanzania.

Aliambiwa awapeleke kwa anayeishi Maliwanda, Bunda, ambaye ilifahamika ni Elia Wekwe, ambako aliwapeleka.

Elia Wekwe yeye alisema Januari 6,2024 saa 4:00 asubuhi alikamatwa huko Maliwanda na askari wawili na wakiwa njiani walipitia kwa mwenyekiti wa kitongoji na kumjulisha kuwa wanataka kufanya upekuzi nyumbani kwake, na katika upekuzi huo hawakukuta kitu chochote, lakini walikamata simu yake.

Alifikishwa mahakamani Februari 7, 2024 akikabiliwa na kesi ya mauaji ya Kulwa aliyedai hakuwahi kumfahamu na hahusiki na kifo chake.


Uamuzi Jaji

Jaji Massam katika hukumu amesema anakubaliana na utetezi wa mshitakiwa wa kwanza – Konzela kwamba hakufanya kosa na hajui lolote kuhusu kifo cha Kulwa na upande wa mashtaka umeshindwa kumhusisha na kifo hicho.

Hata hivyo, amesema mshtakiwa wa pili amehusika na kifo hicho, hivy amemwachia huru Konzela na kumhukumu Elia adhabu ya kunyongwa hadi kufa.