Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Muliro: Ulinzi sio polisi kuwa wengi mitaani

Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna Msaidizi Jumanne Muliro, akizungumza na waandishi wa Mwananchi, alipofanya ziara katika ofisi za Kampuni ya Mwananchi communications (Ltd ) juzi Tabata jijini Dar es Salaam.

Muktasari:

Wakati Jiji la Dar es Salaam likielezwa kuwa na changamoto ya uhalifu, Jeshi la Polisi limesema kila mwananchi ana jukumu la kulinda usalama katika eneo lake.


Dar es Salaam. Wakati Jiji la Dar es Salaam likielezwa kuwa na changamoto ya uhalifu, Jeshi la Polisi limesema kila mwananchi ana jukumu la kulinda usalama katika eneo lake.

Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro alitoa kauli hiyo juzi alipotembelea ofisi za Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL)jijini hapa.

Akiwa katika mahojiano yake na Gazeti la Mwananchi Muliro aliulizwa kwamba, kutokana na ukubwa wa Jiji la Dar es Salaam, inaonekana Jeshi la Polisi linashindwa kufika kila mahali kutoa huduma kutokana na uchache wa askari wake, je linafanyaje?

Muliro: Kwanza polisi tunataka tutoke huko kwamba polisi wawepo popote. Kitu tunachotaka watu wafuate sheria, suala sio kujaza polisi.

Sio kila unapokwenda uone polisi, ni dalili mbaya za nchi, watu wake kutofuata sheria, wala sio dalili nzuri kwa polisi kwamba wamefanya kazi kubwa.

Hata wale tunaowakalisha muda wa kazi mwingi tunaangalia muda gani kuna magari mengi ni mchana, usiku yanapungua, vinginevyo tutasema polisi walale barabarani, ambao ni mtazamo mchafu kabisa.Tunataka watu wafuate sheria ili polisi wapungue barabarani.

Nenda kaangalie Sheria ya Serikali za Mitaa, inakwambia, Mwenyekiti wa Serikali za Mitaa ndio mwenyekiti wa ulinzi na usalama wa mtaa ule.

Maana yake wewe ni mtu mkubwa, unaratibu masuala ya kuzuia vitendo vya kihalifiu, matishio ya usalama kwenye eneo lako. Ukiratibu vizuri Polisi Kata anakuletea timu mara moja, unamaliza kazi yako. Mitaa inayofuata mifumo wa usalama chini ya mifumo ya Serikali za Mitaa, wahalifu hawataingia.

Mwandishi: Katika utendaji wako kwa jijini Dar es Salaam, ni changamoto gani kubwa unazokumbana nazo?

Muliro: Tuna changamoto ya Jiji la Dar es Salaam, kama sehemu ya jiji la kibiashara. Changamoto kubwa ilikuwa ni uhalifu wa kuwania mali na kutaka pesa ya moja kwa moja mkononi.

Changamoto ni jinsi ya kushughulika na uhalifu wa kijinai. Sheria zimeweka wazi jinsi ya kushughulika na uhalifu wa kijinai, pia zimeweka wazi muda wa kumshikilia mtuhumiwa huyo.

Lakini ukiangalia miundombinu ya kushughulikia naye, kuanzia kwenye ufuatiliaji, upelelezi na ule utayari wa wananchi kukubaliana na sheria hiyo, ule mgongano wa kifikra na mgongano wa kisheria, hiyo ndiyo changamoto ninayopata.

Kwa mfano X anaibiwa TV yake, ufuatiliaji unafanyika, Y anapatikana ndiyo mtuhumiwa. Kwa mifumo ya kisheria, pamoja na wizi uliofanyika na kuvunja nyumba yako, huyo bado ni mtuhumiwa na dhamana ni haki yake.

Kwa hiyo wakati wa utekelezaji wa jukumu hilo la kisheria, ndipo hapo makundi mengine ambao ndiyo waathirika, hawakubaliani na sheria na hawakubaliani na usimamizi ule wa sheria kutoka kwa polisi.

Ndipo zinapokuja zile fikra polisi wanashirikiana na mhalifu. Mtuhumiwa anakamatwa asubuhi anaachiliwa jioni kwa sababu ya pesa au mtuhumiwa akikamatwa leo, kesho unamkuta nje.

Kwa hiyo mgongano wa fikra za watu wengi dhidi ya mtuhumiwa ndiyo changamoto kubwa.

Watu wengi waliopata matatizo ya kijinai, huwa hawataki mtuhumiwa arudi, pamoja na Katiba kueleza, huyu mtu hana hatia mpaka itakapothibitishwa. Wanaokubaliana na sheria ni ndugu na marafiki wanaotaka sheria itekelezwe.

Hapo ndipo kuchafuka kwa Jeshi la Polisi inapokuja anakamatwa asubuhi, jioni anaachiwa hata vitu vyangu havijapatikana. Ukiangalia Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA) inavyosema, fanya uchunguzi kwamba ndipo ukamate, lakini wananchi wanakuletea taarifa aliyeniibia ni X. Kwa hiyo pamoja na sheria hiyo anakuendesha kwamba umkamate yule aliyemwibia vitu vyake na unaposita anasema unakula na yule mtu.

Mwandishi: Kuhusu miundombinu napo kuna changamoto gani?

Muliro: Ipo dhana ambayo mimi naona sheria zetu tunaziiga bila kuenendana na mazingira yetu.

Mazingira ya Sweden kwa mfano au maeneo ya India ambako sheria za ushahidi nyingi zimechukuliwa, au Ulaya zinaruhusu kutekelezeka kwa sheria zile.

Kwa sababu ukiangalia mifumo ya kimaisha na maeneo mengi yamefungwa mifumo ya kiusalama yaani CCTV.

Kwa hiyo ukifanya uchunguzi wa maeneo yenye mifumo ya kiusalama, jambo likitokea ni rahisi. Hata huna haja ya kukamata mtu halafu upeleleze, kwa sababu ni rahisi unapelekeza halafu unakamata. Kwa sababu kila kitu unakiona, unakaa naye kwa nini? Kwa hiyo hata kubambikiza kesi haiwezekani, kwa sababu ya mifumo ya miundombinu ya yanayofanyika katika miundombinu ya kiuchumi ya kisiasa na kiusalama.

Mwandishi: Kwa hiyo unapendekeza nini kifanyike katika masuala ya sheria ili kukabiliana na changamoto hizi?

Muliro: Kwanza ukitaka kupata kitu bora ambacho kipo kwenye misingi mizuri ya kisheria, lazima utengeneze miundombinu. Kama maboresho yanayofanyika kwenye Mahakama na hata Jeshi la Polisi linafanya maboresho na hata jamii pia.

Kwa mfano haya masuala ya kupora simu au kukwapua, kama barabara zina CCTV, hivi unafikiri utaweka askari wa kuwa wanahangaika namna hiyo?

Kwa sababu wakipora, polisi si wanakuja wanahangaika na CCTV? Au tunakuweka kwenye vyombo vya habari, kwamba huyu tunamtafuta ndiye mporaji wa matukio ya Selander bridge.

Kwa hiyo tunajua tunamtafuta nani na ushahidi upo, lakini pia inasaidia kuzuia. Kama watu wanakujua na wamekutangaza, utarudia? Watu wanasema sijui Ulaya, sio kwamba wale ni watakatifu, ni kwa sababu miundombinu imewafanya wasifanye matukio. Mifumo inaweza kuzuia matukio ya kihalifu na hata ya kitolea upelelezi wake unakuwa rahisi.

Mwandishi: Kwa hiyo kwa sababu ya changamoto hizo za miundombinu, huwa mnalazimika kubambika watu kesi?

Muliro: Sitaki kukiri hivyo. Ninachotaka kusema maboresho yanayokuja ni makubwa sana katika shughuli za kiupelelezi.

Ninachosema ni kwamba kuna mitizamo ya migongano ya kifikra wakati wa utekelezaji wa sheria, tunagundua kwamba huyu ni mtuhumiwa hatutaki kukaa naye, lakini jamii haitaki, halafu unaandika rushwa imejaa vituoni.

Mwandishi: Kumekuwa na matukio ya mauaji ya nyumbani, haya mnachukua hatua gani kudhibiti?

Muliro: Nimefurahishwa jinsi unavyofuatilia kwa karibu kwamba mauaji yanayoripitiwa ni vurugu za nyumbani. Ni mivutano, kutoelewana katika uhusiano, halafu anakupiga kisu au ukapigwa panga, lakini siyo jambazi. Au mtu akakukaba kwa mtandio, sio ujambazi, lakini ni mauaji.

Ukiangalia aina hiyo ya uhalifu, huwezi kudhibiti kwa polisi kuja kwa silaha kama bunduki au bastola. Yanadhibitiwa kwa malezi au masuala ya dini. Ni suala linalohitaji taasisi nyingi zikiwamo za kidini na watu wasali usikie hofu ya Mungu.

Ufundishwe uvumilivu kati ya mume na mke, boyfriend na girlfriend, kwamba usishangae mwanamke ukamkuta na mume mwingine au mwanaume ukamkuta na mwanamke mwingine, bila kutahadharishwa unaweza kumpiga mtu kisu au panga. Ila huwezi kudhibiti kwa kufanya doria.