Mtendaji wa kata ashikwa ‘kigugumizi’ kujibu tuhuma mbele ya Makonda

Mtendaji wa Kata ya Bwawani, Simon Kaaya akiwa chini ya ulinzi wa Jeshi la Polisi kwa amri ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha,Paul Makonda kwa tuhuma za kusababisha migogoro ya ardhi ikiwemo kuuza ardhi ya bila kufuata utaratibu
Muktasari:
- Hayo yamejiri leo Mei 28, 2024 kwenye ziara ya Makonda ikiwa ni siku ya nne kati ya sita anazotembelea halmashauri sita za Mkoa wa Arusha.
Arusha. Mtendaji wa Kata ya Bwawani, Simon Kaaya leo amejikuta akihaha kutoa majibu mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda baada ya kutuhumiwa na wananchi kuuza eneo la kijiji.
Hayo yamejiri leo Jumanne Mei 28, 2024 wakati wa mwendelezo wa ziara ya mkuu huyo wa mkoa yenye lengo la kusikiliza kero za wananchi na kuzitafutia ufumbuzi.
Baada ya kukagua mradi wa Zahanati ya Bwawani, akajitokeza Lucas Samweli na kumweleza konda kuwa Januari 2002 aliuziwa shamba ndani ya ofisi ya Kijiji cha Bwawani na mtu aliyekuja na mwenyekiti wake, lakini hadi sasa hajakabidhiwa shamba hilo.
"Siku hiyo kuna mtu alikuja na mwenyekiti wangu wa kijiji akasema kuna shamba linauzwa Sh2 milioni nikanunue, nilienda kuangalia nikakubali lakini kwa sababu sikuwa na hela nikaenda kukopa kwenye kikundi nikalipa," amesema Samwel.
Hata hivyo, anasema baada ya siku kadhaa kupita, alianza kuliandaa shamba lake hilo alilouziwa kwa kufyeka msitu.
Anasema wakati anaendelea na kazi hiyo, alifuatwa na ofisa mtendaji aliyemweleza kuwa fedha aliyoitoa haitoshi anatakiwa aongeze Sh2 milioni nyingine.
“Nikamwambia sina, akaniambia nitoe angalau Shilingi milioni moja na nusu, bado nikamwambia sina,” amesema Samwel.
Anasema kwa kuwa shamba alilihitaji, ikabidi auze ng'ombe zake sita ili alipe fedha hizo. Anasema licha ya kulipa fedha hizo, kwa sasa hana haki ya kuligusa shamba hilo kwa kuwa aliambiwa kuna mtu mwingine anadai shamba hilo ni lake.
“Nilimfuata mtendaji kumlalamikia lakini akanihakikishia eneo hilo ni langu na hata kama huyo mtu kalima maharage niyafyeke,” amesema mwananchi huyo.
Anasema licha ya kuambiwa hivyo, hakuona busara kuyafyeka aliyaacha akaamu kushtaki ngazi mbalimbali za kata na wilaya lakini mpaka sasa hajapata msaada.
Amedai baada ya Kaaya kusikia kuna ziara ya Makonda katani hapo, alimuita ofisini kwake akitaka amrudishie fedha zake alizolipa kwa ajili ya kununua shamba hilo, lakini alimkatalia kwa madai alishaingia hasara ya kuuza ng’ombe wake ilia pate ardhi.
Hata hivyo, anasema katika kipindi cha vuta nikuvute ya mgogoro huo, waligundua kuwa eneo alilouziwa na mtendaji huyo ni mali ya Serikali ya kijiji na linatumika kutapeli watu wengi.
Anasema eneo hilo upande mwingine tena alishauziwa pia kijana mwingine aliyemtaja kwa jina la Julias Alex naye haruhusiwi kulifanyia chochote.
Baada ya maelezo hayo, Makonda alimuita Mwenyekiti wa Kijiji hicho cha Bwawani, Abduli Nkindi kujibu tuhuma hizo naye alikiri kumfahamu mwanachi wake.
"Ndio namfahamu huyu mwananchi na aliuziana eneo na mtu, lakini kuna kipande kilizidi ndio mtendaji akamwambia aongeze hela kama anataka lote kwa ajili ya ujenzi wa ofisi ya kijiji chetu na kituo cha afya,” amesema Nkindi.
Hata hivyo, Kaaya alipoulizwa amesema eneo alilouziwa Lucas siyo hilo bali alivuka mpaka ndiyo akatakiwa kuongeza fedha.
"Aliongeza hela ili aongezewe eneo lakini sijui mgogoro mwingine unatokea wapi maana mimi simjui hata huyo mtu,” alisema Mtendaji huyo.
Alipoulizwa na Makonda amepata wapi dhamana ya kuuza eneo la kijiji, alishindwa kujibu na kupata kigugumizi hali iliyoamsha kelele kwa wananchi za akamatwe, akamatwe.
Baada ya kelele hizo, ndipo mkuu huyo wa mkoa akamtaka Mkuu wa Polisi Wilaya (OCD) Wilaya ya Arumeru na Mkuu wa Takukuru kumkamata Kaaya na wafanye upelezi juu ya tuhuma hizo haraka.
"Nataka ndani ya wiki moja nipate taarifa ya majibu ya upelelezi huu imekuwaje. Sina tabia ya kulea wezi, wala rushwa, wala wazembe kwenye uongozi wangu, yaani nitawapiga spana hadi mnyooke," amesisitiza Makonda.
Hivyo Kaaya alikamatwa na askari waliokuwa kwenye msafara huu na kumpandisha kwenye gari lao na kuondoka naye.