Mtanzania Dk Mwapinga achaguliwa Katibu Mkuu FP-ICGLR

Luanda, Angola. Kuimarika kwa diplomasia ya Tanzania na ushirikiano wa kikanda, Mtanzania Dk Deo Mwapinga ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu mpya wa Jukwaa la Mabunge ya Nchi Wanachama wa Mkutano wa Kimataifa wa Kanda ya Maziwa Makuu (FP-ICGLR).
Uteuzi wake umefanyika baada ya kuungwa mkono kwa kauli moja na Maspika wa Mabunge ya Kitaifa ya nchi wanachama wa ICGLR.
Uteuzi wa Dk Mwapinga umefanyika leo Ijumaa Aprili 25, 2025 katika Mkutano Mkuu wa FP-ICGLR unaofanyika jijini Luanda, Angola, ambapo wajumbe kutoka mabunge ya nchi za Kanda ya Maziwa Makuu walikutana kujadili masuala ya amani, usalama na utawala wa kidemokrasia, ikiwa ni pamoja na kuidhinisha uamuzi wa maspika juu ya uchaguzi wa Katibu Mkuu mpya wa FP-ICGLR.
Katika hotuba yake ya kukubali uteuzi huo, Dk Mwapinga amewashukuru wajumbe wa nchi wanachama kwa heshima hiyo waliyompa, akiahidi kufuata maadili ya FP-ICGLR na kuimarisha ushirikiano wa kibunge katika ukanda huo.
“Hii siyo tu heshima binafsi, bali ni kutambua dhamira ya Tanzania ya kuendeleza amani, utulivu na ushiriki wa kikanda. Nakubali jukumu hili nikiwa na ufahamu kamili ya kazi muhimu iliyo mbele yetu: kutetea amani na usalama, kuimarisha diplomasia ya kibunge, kuimarisha ushirikiano wa kikanda na kuendeleza demokrasia na utawala bora katika ukanda wetu,” amesema.

FP-ICGLR linajumuisha mabunge kutoka nchi 12 wanachama wa ICGLR kwa lengo la kusaidia kutekeleza itifaki kuhusu demokrasia, utawala bora na haki za binadamu.
Akiwa Katibu Mkuu, Dk Mwapinga atawajibika kuratibu programu na shughuli za jukwaa hili ambazo hufanyika jijini Kinshasa, DRC, zikiwamo kuimarisha mazungumzo baina ya mabunge na kusaidia kuratibu malengo ya maendeleo ya ukanda huo.
Dk Mwapinga aliungwa mkono kwa kiasi kikubwa kutoka kwa Maspika wa Mabunge ya Kitaifa ya nchi wanachama wa ICGLR, jambo linalodhihirisha imani kubwa waliyonayo kwa uongozi wa Tanzania.
Nafasi hiyo ya Katibu Mkuu iligombewa na nchi tatu za Burundi, Kenya na Tanzania ambapo Maspika walikubaliana kwamba Tanzania inastahili kuongoza ajenda ya ICGLR kwa kipindi cha miaka mitatu ijayo, huku ikiruhusiwa kuhuishwa kwa kipindi kingine kimoja, hali iliyosababisha Kenya na Burundi kujiondoa katika kinyang’anyiro hicho.
Serikali ya Tanzania imepokea uteuzi huu kwa fahari, ambapo Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mussa Azzan Zungu, aliyeongoza ujumbe wa Tanzania nchini Angola, ameuelezea kama: “Wakati wa kujivunia kwa nchi yetu, ishara ya mafanikio ya diplomasia imara katika Kanda ya Maziwa Makuu na ushuhuda wa uongozi wetu chini ya Rais Dk Samia Suluhu Hassan.”
Dk Mwapinga anachukua nafasi ya Balozi Onyango Kakoba wa Uganda, ambaye alihudumu kama Katibu Mkuu wa jukwaa hilo tangu Machi 2018. Kakoba ni Mbunge wa zamani wa Buikwe Kaskazini nchini Uganda na aliteuliwa pia kwa kauli moja na Mkutano wa Maspika hadi Oktoba 2024.
Uteuzi huu unafungua ukurasa mpya katika historia si tu kwa Tanzania bali pia kwa FP-ICGLR kwa ujumla, ukiwa mwanzo wa enzi mpya ya uongozi na ushirikiano.
Akizungumza baada ya ushindi huo, Mbunge wa Singida Magharibi, Elibariki Kingu ambaye aliongoza mazungumzo ya pande mbili na wakuu wa ujumbe kutoka mabunge ya nchi wanachama nchini Angola kutafuta kuungwa mkono, amesema: “Huu si ushindi binafsi wa mgombea aliyechaguliwa tu, bali ni mafanikio ya kimkakati kwa Tanzania kwa ujumla. Unaiweka nchi yetu katikati ya uamuzi katika moja ya maeneo yenye umuhimu mkubwa kijiografia barani Afrika.”
Kingu, ambaye ni mbunge mwenye uzoefu mkubwa katika mazungumzo ya pande mbili na mabunge ya nchi nyingine, aliteuliwa na Spika wa Bunge la Tanzania, Dk Tulia Ackson kwa ajili ya kuunga mkono kampeni ya Tanzania katika kumsaidia Dk Mwapinga kushinda nafasi hiyo.