Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Msongamano wa wanafunzi kikwazo cha ubora wa elimu shule za msingi Temeke-1

Dar es Salaam. Kilomita zaidi ya 27, mwendo wa zaidi ya saa tatu kutoka ofisi ya Mwananchi Communications Limited (MCL) Tabata, nafika Shule ya Msingi Mbande.

Muda huu wa saa tatu asubuhi wanafunzi wakiwa darasani kabla ya mapumziko, wengine waliendelea kucheza nje wakizunguka huku na kule kiasi cha kunifanya nianze kutafakari kutokana na wingi wao.

Sehemu ambayo tulisimamisha gari tulipakana na mlango wa moja ya madarasa ambalo mwalimu alikuwa akiendelea kufundisha, lakini kitu kilichonishangaza, baadhi ya wanafunzi walikuwa wamekaa chini, karibu kabisa katika miguu yake.

Mwalimu huyu wa kike aliyevalia nguo ndefu kuvuka magoti ufundishaji wake haukuwa ule wa kumfanya awe huru kuzunguka ndani ya darasa, ili kuhakikisha kila mwanafunzi anamsikia na kumuelewa na badala yake aligeuka mbele na nyuma na kupiga hatua chache kulia na kushoto ili kuhakikisha anaeleweka.

Watoto waliokuwa chini si kwamba walikuwa wakifanya jambo dogo na pindi watakapomaliza watarudi katika madawati yao, la hasha, hiyo ndiyo sehemu yao ya kudumu kwa siku husika kutokana na uchache wa madawati uliopo shuleni hapo.

Shule hiyo iliyopo wilayani Temeke ina wanafunzi 6,373, ndiyo inayoshika namba moja kwa kuwa na idadi kubwa ya wanafunzi nchini kwa mujibu wa takwimu za Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi).

Mbali na shule hiyo, Wilaya ya Temeke pia inaingiza shule nyingine tano katika orodha ya shule 10 zinazoongoza kwa kuwa na wanafunzi wengi Tanzania, jambo ambalo linaweka shaka ya ubora wa elimu.

Hiyo ni kutokana na idadi ya wanafunzi waliopo katika shule hizo kutoendana na wingi wa madarasa na madawati yanayopatikana, jambo ambalo linafanya wanafunzi wengine kukaa chini au kupokezana madarasa.

“Siku ikiwa zamu yako ya kukaa chini unapata tabu, huwezi kuandika mwandiko mzuri kutokana na jinsi ulivyokaa, unachafuka bila kujali ni siku gani,” anasema mmoja wa wanafunzi.

Kukaa chini wakati wa kujifunza kunatajwa kuwa na athari, hasa kwa wanafunzi wa madarasa ya chini.

Kwa mujibu wa Kassana Maganga, ambaye ni mwalimu mstaafu wa madarasa ya awali na la kwanza, moja ya vitu vinavyoweza kumfanya mwanafunzi kuwa na uwezo wa kuumba herufi vizuri ni kukaa sehemu inayompa uhuru.

“Wakati nikiwa mwalimu nilikuwa nikiwaweka wanafunzi nje waandike herufi katika mchanga, ili iwe rahisi kwao kuandika katika daftari, lakini wakikaa chini muda wote haiwapi huo uhuru,” anasema.

Anasema kukaa katika dawati pia huwa kuna uelekeo wa aina moja, hivyo kuweka ugumu kwa wanafunzi kutingishana, tofauti na wanapokuwa chini.

“Wakikaa chini huwezi hata kuwaweka katika mstari na kila mtu anapotaka kuandika lazima atainama kwa aina yake, wakati mwingine miguu ya mtu inaweza kufika katika daftari la mwingine,” anasema Kassana.

Mbali na wanafunzi kukaa chini ndani ya madarasa, shule hiyo na ile ya Majimatitu zina mbao za nje ambazo wakati mwingine mwalimu badala ya kuhama mkondo mmoja kwenda mwingine, hulazimika kukusanya wanafunzi wa mikondo yote na kuwaweka sehemu moja ili aweze kuwafundisha kirahisi.

Hali iliyopo katika shule hiyo, pia imeshuhudiwa katika Shule ya Msingi Majimatitu, yenye wanafunzi 4,824 na Shule ya Msingi Chamazi iliyo na wanafunzi 5,230, ambazo pia zimeelemewa na idadi ya wanafunzi.


Hali ilivyo

Shule hizo tatu za Mbande, Majimatitu na Chamazi kwa ujumla kabla wanafunzi wa darasa la saba hawajamaliza Septemba mwaka huu zilikuwa na wanafunzi 17,158, kwa mujibu wa ripoti ya Tamisemi ya mwaka 2024.

Idadi ya wanafunzi wanaopatikana katika shule hizo ni zaidi ya waliopo ndani ya wilaya nzima ya Korogwe, mkoani Tanga na shule 35 zilizopo, kwani zina jumla ya wanafunzi 16,742.

Pia idadi hiyo ni zaidi ya wanafunzi wote wanaopatikana katika shule 33 za Wilaya ya Madaba iliyo na jumla ya wanafunzi 11,530.

Uchambuzi zaidi wa kina unaonyesha kuwa shule ya Mbande yenye wanafunzi 6,373 ina madarasa 37, Chamazi yenye wanafunzi 5,957 ina madarasa 29 na shule ya msingi Majimatitu yenye wanafunzi 4,828 ina madarasa 44.

Hiyo ikiwa na maana kuwa shule ya msingi Mbande ilikuwa inahitaji vyumba vya madarasa 142, Chamazi ilihitaji vyumba 132 na Majimatitu ilihitaji madarasa 107, ili kuweka uwiano sawa wa wanafunzi kwa darasa ili kuendana na idadi ya wastani wa wanafunzi 45 ndani ya darasa kwa shule za msingi.

Hali hii inafanya sasa wanafunzi katika shule ya Mbande kuwa na wastani wa wanafunzi 172 kwa darasa, Chamazi ikiwa na wastani wa wanafunzi 205 kwa darasa na Majimatitu ikiwa na wastani wa wanafunzi 110 kwa darasa.

Uchache wa madarasa unaosababisha jambo hilo unatokana na upuuzaji wa Mwongozo wa Uanzishaji na Usajili wa Shule wa mwaka 2020, kifungu cha 3 unaotaka idadi ya wanafunzi darasani kwa shule za msingi wasizidi 45.

Jambo hilo pia linachangiwa na usimamizi mbovu wa majukumu ya bodi na kamati za shule kama inavyoelekezwa katika Kanuni za Elimu za Mwaka 2002 Kanuni ya 3(b) inayotoa wajibu kwa bodi ya shule kuhakikisha madarasa yana uwiano unaofaa wa wanafunzi kwa mwalimu ili kutoa elimu bora.


Hali ilivyo kitaifa

Mbali na shule hizo, ripoti ya Tanzania in Figures iliyotolewa na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), inaonyesha kuwa hadi mwaka 2021 uwiano wa wanafunzi kwa darasa kitaifa ulikuwa 81.

Hiyo ni baada ya shule za msingi zilizokuwapo kipindi hicho kusajili wanafunzi 10,687,593 ambao walitumia madarasa 132,389 yaliyokuwapo kwa wakati huo.

Madarasa hayo ni sawa na asilimia 55.74 pekee ya madarasa yote yaliyokuwa yakihitajika ili kuweza kufanya wanafunzi kukaa kwa wastani unaohitajika kwa darasa.

Hiyo ikiwa na maana kuwa shule nyingi zilikuwa zinakabiliwa na mrundikano wa wanafunzi, huku mikoa miwili pekee ya Njombe na Kilimanjaro ikiwa na uwiano mzuri kwa wanafunzi kwa darasa, ikiwa na wastani wa 43 na 38.

Ripoti ya mwaka 2021 ambayo ndiyo ya mwisho kutolewa na Serikali ikionyesha mchanganuo wa wanafunzi dhidi ya madarasa yaliyopo, inaonyesha kuwa mikoa mingi ilikuwa na wanafunzi wengi ndani ya darasa moja, huku Dar es Salaam, Geita, Katavi na Mwanza ikiwa zaidi.

Mikoa hiyo ilikuwa na wastani wa wanafunzi 106, 124, 130 na Mwanza 106. Mikoa mingine iliyokuwa taabani ni Tabora (99), Simiyu (94) na Mara (91).


Shule binafsi kibano

Wakati hali ikiwa hivyo kwa shule za Serikali, uzingatiwaji wa idadi ya wanafunzi kwa darasa umekuwa ukiwekewa mkazo zaidi kwa shule binafsi kuliko zile za Serikali.

Hali hiyo imefanya shule nyingi za binafsi wanafunzi darasani kuwa wasiozidi 45, hali ambayo imetajwa kuwa moja ya sababu za wao kufanya vizuri katika mitihani mbalimbali ya kitaifa, kwani walimu wanakuwa na uwezo wa kumfikia mwanafunzi mmoja mmoja.

Mmoja wa wamiliki wa shule binafsi, Leonard Mao anasema mara nyingi madarasa yao yanakuwa na kati ya wanafunzi 30 hadi 40 na katika baadhi ya shule madarasa hayana watoto.

“Ikitokea ni muujiza, sisi tuna madarasa mengi kuliko idadi ya wanafunzi. Serikali inajaza wanafunzi wengi kwa darasa kutokana na uhaba wa majengo na uhaba wa walimu, ndiyo maana wanasongamanishwa,” anasema Mao.

Anasema wathibiti ubora wamekuwa wakali hasa kwa kuangalia idadi ya wanafunzi kwa choo, kitabu kwa mwanafunzi, idadi ya walimu kwa mwanafunzi.

“Katika eneo hili wamekuwa wakali sana na shule zetu zimejitahidi kuzingatia miongozo yote tuliyopewa na Serikali katika utoaji wa huduma kwa wanafunzi,” anasema Mao.


Wazazi walia

Kuzidi kwa idadi ya wanafunzi ndani ya darasa kunaweka ugumu katika ujifunzaji, jambo ambalo linaweza kufanya kuwapo kwa matokeo mabaya katika mitihani ya majaribio, ya muhula na hata ya kitaifa.

“Mwanangu alikuwa anasoma Mbande kabla sijamhamisha, mwaka mzima wa darasa la awali hakujua kusoma, nilipokuja kubaini nilimhamishia shule za mitaani za kulipia, miezi mitatu alijua kusoma hadi kuhesabu moja hadi 100 kwa Kiingereza,” anasema Naifath Mapunda, mkazi wa Mbande.

Naifath, ambaye ni fundi wa kusuka anasema hali hiyo ilimfanya kuweka nadhiri ya kuhakikisha mwanaye anasoma shule ya kulipia kupitia kipato chake kidogo anachokipata.

Mbali na kujua kusoma, Naifath bado ana kumbukumbu ya mwanaye kurudi mchafu kila alipotoka shuleni kutokana na kukaa chini anapokuwa darasani kutokana na uhaba wa madawati.

Kumbukumbu hiyo pia anayo Mariam Issa, ambaye pia mwanaye anasoma shuleni hapo hadi sasa anatamani kuona changamoto kama za upungufu wa madawati zinafika mwisho.

“Watoto wanahangaika, ukiwakuta chini wanavyojikunja ni tatizo, hawawezi kuwa na mwandiko mzuri kwa hali ile kwa kweli, sisi kama wazazi tuko tayari kuchanga lakini madawati yatakaa wapi?” anahoji Mariam.

Kukosekana kwa vyumba vingi vya madarasa nayo ni moja ya changamoto ambayo inaweza kufanya jitihada za kuhakikisha madawati yanakuwa toshelevu zikagonga mwamba.

Hiyo ni kutokana na madarasa kuwa na uwezo wa kubeba madawati machache, hivyo hata madawati yakichongeshwa mengi yatashindwa kuwekwa sehemu inayotakiwa.


Diwani

Hata hivyo, wakati mwingine madarasa yamekuwa machache kiasi cha kulazimika madawati kutolewa nje. Diwani wa kata ya Mbagala, Michael Kamwega anasema idadi kubwa ya wanafunzi katika eneo lake umekuwa ukilazimisha baadhi ya vyumba vya madarasa kutowekwa madawati ili wanafunzi waenee katika mkondo mmoja wakiwa chini.

Anasema wastani wa wanafunzi kwa mkondo ni hadi 170, jambo ambalo linaweka ugumu kuweka madawati yanayoweza kuwatosha wanafunzi wote.

Kwa mujibu wa uchambuzi wa idadi hiyo ya wanafunzi, ikiwa kila dawati moja litakaliwa na wanafunzi watatu, basi darasa hilo litahitaji madawati 57 na ikiwa watakaa wanne, madawati 43 yatahitajika.

“Sasa tunachofanya ni kuangalia namna gani tunaweza kutumia nafasi iliyopo kujenga madarasa kwenda juu ili kupunguza msongamano ndani ya madarasa,” anasema Kamwega.


Serikali

Hata hivyo, katika kupunguza msongamano katika baadhi ya shule, Wilaya ya Temeke ilijenga shule mpya tisa katika maeneo tofauti kati ya mwaka 2021/2022 na 2023/2024 zikiwa na madarasa 241, vyoo 225 na majengo ya utawala 7.

“Ujenzi wake uligharimu Sh9.688 bilioni ambazo ni fedha za mapato ya ndani pamoja na ruzuku ya Serikali kuu (EP4R na BOOST),” anasema Shafi Kipande, Ofisa wa Mipango ofisi ya Mkurugenzi Temeke.

Akizitaja shule hizo kuwa ni Ushirika, Mkondogwa, Vikunai, Kiponza, Ponde, Mikwambe, Mbande Kisewe, Goroka na Dovya.

Mbande Kambayo ni miongoni mwa shule zilizojengwa, ilizaliwa kutoka Shule ya Msingi Mbande ambayo awali ilikuwa na wanafunzi wengi kuliko waliopo sasa.

Hali hiyo imeifanya Temeke sasa kuangalia namna ya kurekebisha madarasa yaliyopo na kuongeza mengine kwenda juu.

Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Sixtus Mapunda anasema ili kumaliza tatizo hilo unahitajika mpango wa muda mrefu kwa sababu mara zote idadi ya wanafunzi wanaojiunga masomo hawatabiriki ikilinganishwa na wanaomaliza shule.

“Jambo hilo linakwenda sambamba na kutafuta fedha kwa ajili ya kuongeza miundombinu ya madarasa ili kupunguza msongamano wa wanafunzi madarasani,” anasema Mapunda.


Kama una maoni kuhusu habari hii, tuandikie ujumbe kupitia WhatsApp: 0765864917.