Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Tanzania kinara wa elimu Kusini

Muktasari:

Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (Unesco) limetoa ripoti inayoonyesha Tanzania imefanya vizuri katika kutekeleza malengo ya Elimu kwa Wote

Katika miaka ya hivi karibuni Watanzania wamekuwa wakishuhudia wanafunzi wengi wakifanya vibaya katika mitihani ya mwisho, jambo ambalo limekuwa likiwatia shaka wananchi kuhusu mustakabali wa elimu.

Wakati wananchi wakiendelea kutafakari kinachoendelea, Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Elimu, Sayansi na Utamaduni (Unesco) kupitia ripoti yake ya Elimu kwa Wote (Efa), limetoa matokeo ya kushangaza.

Akisoma nafasi ya Tanzania katika ripoti hiyo, ofisa mipango na mwakilishi wa Unesco nchini, Zulmira Rodrigues, anasema tangu kuwekwa kwa malengo sita ya Efa mwaka 2000, Tanzania imepiga hatua kubwa na kuzipiku nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara.

Anasema matokeo ya Efa ya mwaka 2012, yanaonyesha kuwa Tanzania ilishafikia na kupita kigezo kilichokuwa kimewekwa cha asilimia 57.1 kwa kupata asilimia 72.2 ikiwa imepanda juu kwa pointi 14.6 dhidi ya pointi 17.8 za nchi zilizo kusini mwa Jangwa la Sahara.

“Mafanikio haya ni kutokana na kufanikisha wanafunzi kumaliza masomo. Mwaka 2012 asilimia 87.5 walimaliza, tofauti na asilimia 62.9 ya mwaka 2011,” anaeleza.

Anasema mafaniko hayo ya juu barani Afrika yamechangiwa zaidi na uamuzi wa Serikali kuanzisha sera ya kutoa elimu bure kwa wanafunzi wa shule za msingi mwaka 2002 na kufuta mtihani wa darasa la nne uliokuwa ukiwakwamisha wanafunzi wengi.

“Kwa mwendo huu, Tanzania ipo katika njia sahihi ya kufanikisha haraka lengo namba mbili la kutoa bure elimu ya msingi kwa wote. Lengo namba tano la usawa wa kijinsia kwa shule za msingi limeshafikiwa kwa asilimia 100 ya wasichana kwenda shule dhidi ya asilimia 96 ya wavulana,” anasema.

Pia matokeo hayo yanaonyesha kuwa Tanzania imefanya vizuri katika lengo namba nne la kupunguza idadi ya watu wasiojua kusoma kuanzia miaka 15 kwa kufikisha asilimia 73.2 mwaka 2012 kutoka asilimia 69.4 ya mwaka 2002, ambayo ni juu zaidi ya malengo yaliyowekwa ya asilimia 67.6.

Vilevile, Tanzania imefanikiwa kutimiza lengo namba moja la kusomesha watoto wa awali kwa asilimia 40 kiwango ambacho ni mara mbili zaidi ya kilichowekwa chini ya Jangwa la Sahara. Wakati kiwango cha wanafunzi wanaomaliza sekondari ni asilimia 35, mwaka 2011 Tanzania ilikwishafikisha asilimia 43.

Kuhusu idadi ya wanafunzi wanaoandikishwa shuleni katika ngazi zote, ripoti inaonyesha ongezeko kubwa la wanafunzi. Idadi ya wanafunzi wanaoingia sekondari imeongezeka kutoka asilimia 18 hadi asilimia 52.

“Mafanikio haya yamefikiwa kutokana na mipango endelevu iliyowekwa shule za awali. Pia idadi ya wanafunzi katika jamii imeongezeka hadi kufikia 374 kati ya watu 100,000 mwaka 2012, sawa na mara tano zaidi ikilinganishwa na ilivyokuwa mwaka 2001,” inasema ripoti hiyo.

Hata hivyo, ripoti inabainisha kuwa Tanzania haijafanya vizuri katika kipengele hicho, ikilinganishwa na malengo yaliyowekwa Kusini mwa Jangwa la Sahara la kuwa na wanafunzi 632 kati ya 100,000.

Mfumo wa elimu unapendelea watoto wa matajiri

Matokeo ya utafiti huo yamefichua kuwa watoto wa matajiri ndiyo wenye fursa zaidi ya kumaliza shule ikilinganishwa na maskini. Wakati asilimia 98 ya watoto wa matajiri wanaandikishwa shule ya msingi, asilimia 86 ndiyo wanamaliza elimu hiyo, watoto wa maskini asilimia 91 walioandikishwa idadi yao inateremka haki kufikia asilimia 55 tu.

Asilimia 41 ya watoto wa matajiri wanaingia sekondari (hadi kidato cha nne) dhidi ya asilimia 19 ya watoto wa maskini. Pia imebainika kuwa asilimia 70 ya watoto wa wenye ‘nacho’ ndiyo huingia kidato cha tano na sita huku asilimia 44 ya wenzano ambao hupata fursa hiyo.

Hata hivyo, ikilinganishwa matokeo yanaonyesha kuwa asilimia 106 ya wasichana huingia darasa la kwanza dhidi ya asilimia 105 ya wavulana. Hali hiyo inaonekana kubadilika wakati wanafunzi hao wanapoingia sekondari, kwani asilimia 60 ya wavulana ndiyo hufaulu kuvuka kikwazo hicho dhidi ya asilimia 45 ya wasichana.

Idadi ya wanafunzi wavulana hushuka hadi kufikia asillimia 12 wanapofika kidato cha tano, huku wasichana wakiwa asilimia saba.

Akizungumzia hali hiyo, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa anakiri kutokuwa na ulingano kati ya wavulana na wasichana pia kati ya watoto wa matajiri na maskini.

“Jambo hilo tumeanza kulifanyia kazi, juhudi unazoziona zinaendelea ni sehemu yake, mwaka jana Shule ya Sekondari ya Kata ya Igowole iliongoza kitaifa, lakini kuna shule nyingi za binafsi za gharama kubwa mbona hazikuongoza?

Hii ina maana Serikali inahakikisha tuna walimu wa kutosha, madarasa mazuri lakini sasa tumeanza kushambulia maabara ili wanaojifunza sayansi wafanye elimu kwa vitendo,” anasema.

Kuthibitisha kuwa hatua zinachukuliwa anatoa mfano: “Nilipokuwa Ngorongoro katika shule ya Kata ya Malambo, msichana mmoja wa Kimasai kidato cha kwanza akanionyesha experiment (jaribio) nilipokwenda kuzindua maabara, akanionyesha akapiga kizungu pale kwa kweli nilihisi raha sana.

“Nilihisi raha, nikaona kumbe kuwa Waziri wa Elimu ni kitu kitamu sana. Huko Ngorongoro msichana mdogo wa Kimasai anaonyesha namna ya kufanya kazi na nilipotaka kumwambia sivyo alikuwa mkali, akajiona yeye anajua kuliko waziri.”

Hata hivyo, pamoja na sifa zote kwa Tanzania, ripoti hiyo inasema Serikali inapaswa kuongeza kiwango cha ubora wa elimu, kwa kuwa ongezeko la idadi ya wanafunzi haliendani na ubora.

Hiki kimekuwa kilio cha wadau wengi wa elimu ambao mara kwa mara wanasema shule zina wanafunzi wengi, lakini ama hawafundishwi au wanachofundishwa hakina ubora.