Mshtakiwa mpya aunganishwa kesi ya ‘vigogo’ NIC

Muktasari:
- Mshtakiwa Eshimendi Uronu ameunganishwa katika kesi inayomkabili aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Bima la Taifa (NIC), Sam Kamanga na wenzake, wakikabiliwa na mashtaka 390, likiwemo la kuchepusha fedha na kuisabishia hasara ya zaidi ya Sh 1.8 bilioni.
Dar es Salaam. Mshtakiwa Eshimendi Uronu ameunganishwa katika kesi inayomkabili aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Bima la Taifa (NIC), Sam Kamanga na wenzake, wakikabiliwa na mashtaka 390, likiwemo la kuchepusha fedha na kuisabishia hasara ya zaidi ya Sh 1.8 bilioni.
Wengine ni Tabu Kingu ambaye alikuwa Kaimu Mhasibu Mkuu wa NIC, Victor Mleleu na Peter Nzunda ambaye ni walikuwa ni whasibu wa shirika hilo, huku Kenan Mpalanguro, Lusubilo Sambo na Mafworo Ngereji wakiwa watumishi wa kawaida wa shirika hilo.
Wakili wa Takukuru, Ipyana Mwakatobe amemsomea Uronu mashtaka yanayomkabili yakiwemo ya kughushi nyaraka mbalimbali, kutakatisha fedha, kuongoza genge la uhalifu, kuchepusha fedha, kuwasilisha nyaraka za uongo na kulisababishia hasara shirika hilo.
Wakili Mwakatobe akisoma hati ya mashtaka mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Evodia Kyaruzi amedai katika shtaka la kuongoza genge la uhalifu linalowakabili washtakiwa wote, inadaiwa washtakiwa hao walitenda kosa hilo kati ya Januari Mosi 2013 na Desemba 31, 2018 katika maeneo tofauti tofauti jijini Dar es Salaam, mkoani Rukwa, Kilimanjaro, Arusha, Mbeya, Morogoro na Kigoma.
Inadaiwa katika kipindi hicho washtakiwa kwa makusudi waliongoza genge la uhalifu ili kujipatia Sh 1,863,017,400.76 kwa njia ya ulaghai kutoka shirika hlo.
Katika shtaka la kughushi, linalomkabili Kingu na Nzunda, Oronu inadaiwa Mwaka 2013 katika Wilaya ya Ilala, washtakiwa hao wakiwa wahasibu, walighushi hundi yenye thamani ya Sh50 milioni wakionyesha kuwa ni halali na imetolewa na NIC.
Anadai katika mashtaka ya utakatishaji washtakiwa Maleleu, Nzunda, Mparanguro, Sambo na Oronu walijihusisha kununua mashamba na magari maeneo tofauti tofauti jijini Dar es Salaam, Rukwa, Kilimanjaro, Arusha, Mbeya, Morogoro na Kigoma huku wakijua fedha hizo ni mazalia ya makosa ya jinai.
"Upelelezi umekamilka na ameiomba mahakama hiyo ipange tarehe yingine,"Mwakatobe
Baada ya maelezo hayo Hakimu Kyaruzi aliahisha shauri hilo hadi Julai 17, 2023 kwa ajili ya kuwasomewa idadi ya mashahidi na vielelezo.
Washtakiwa Maleleu, Nzunda, Mparanguro, Sambo na Uronu wana makosa ya utakatishaji wa fedha hivyo hawana dhamana.
Lakini kwa upande wa washtakiwa Kamanga, Kingu na Ngereji mashtaka wanaokabiliwa nayo yanadhaminika hivyo wapo nje kwa dhamana