Mrema afunga ndoa, mkewe anena
Muktasari:
- Hatimaye mwanasiasa mkongwe, Augustino Mrema amefunga ndoa na Doreen Kimbi baada ya taarifa ya ndoa hiyo kuwa gumzo kwa takribani siku tatu katika mitandao ya kijamii
Marangu. Hatimaye mwanasiasa mkongwe, Augustino Mrema amefunga ndoa na Doreen Kimbi baada ya taarifa ya ndoa hiyo kuwa gumzo kwa takribani siku tatu katika mitandao ya kijamii
Wawili hao walifunga ndoa hiyo jana katika Parokia ya Uwomboni, Jimbo Katoliki la Moshi wakipishana umri kwa miaka 38, huku mke wa Mrema akisema umri wa mwenza wake ni namba tu.
Mke huyo pia alisisitiza kuwa hakufuata mali kwa Mrema, mwenye umri wa miaka 77 bali ni upendo wake wa dhati alionao kwa mwenza wake.
Ndoa ya Mrema na Doreen imekuwa gumzo katika mitandao ya kijamii kuanzia Twitter, Instagram, Facebook na makundi ya Whatsapp na jana ilihitimisha upotoshaji wa picha ya mkewe, ambayo ni tofauti na waliotajwa mitandaoni.
Mrema, ambaye Septemba 16, 2021 alipata pigo la kifo cha mkewe, Rose Mrema, jana alionekana mwenye bashasha kubwa. Aliwasili na mkewe kanisani saa 3:47 asubuhi wakiwa katika gari aina ya Toyota Harrier nyeusi namba T407 DUA wakisindikizwa na majirani wachache na kundi la waandishi wa habari.
Ndoa ya Mrema haikuwa na shamrashara nyingi kama ilivyo kwa harusi nyingine, kwa kile ambacho kimeelezwa kuwa ni kutokana na Wakristo kuwa katika kipindi cha Kwaresma hivyo ilipaswa kufungwa kimya kimya bila shamrashamra.
Tangu taarifa za Mrema kufunga ndoa kuanza kusambaa wiki hii, picha ya mkewe haikuwahi kuvuja mitandaoni na Mrema mwenyewe alizuia mkewe kuonekana hadharani kwa kile alichosema alitaka kuishangaza dunia na mpenzi wake huyo.
Hiyo pengine ndiyo ilisababisha mkewe kutoka nyumbani akiwa amejifunika sura hadi alipoingia kanisani bado alikuwa kajifunika na kitenge hadi usoni, lakini dakika chache kabla ya ibada kuanza alitoka nje na aliporudi hakuwa amejifunika.
Ilipotimu saa 5.49 asubuhi ibada ya ndoa ilianza na ilikuwa ikiongozwa na Padri Adelaidi Amani na kumalizika saa 6.52 mchana, kisha msafara kuondoka kuelekea nyumbani kwa Mrema kwa ajili ya ibada takatifu nyumbani kwake.
Mbali na ibada hiyo, pia kumezinduliwa sanamu ya Mtakatifu Agustino iliyotengenezwa na Mrema kama njia ya kuutumia uzee wake katika kumtumikia Mungu na kuzindua nyumba yake aliyoifanyia ukarabati.
Msafara huo ukitoka kanisani ulisindikizwa na kundi kubwa la watu wakiimba nyimbo mbalimbali za kushangilia, ikiwemo nyimbo za Kichaga na wakati msafara huo ukiingia nyumbani Mrema na mkewe walipokelewa na wazee wa Kichaga.
Mke wa Mrema afunguka
Akizungumza na wanahabari kwa mara ya kwanza, Doreen alisema kuwa suala la yeye kuolewa na Mrema limesukumwa na upendo wake wa dhati na kwamba, umri ni namba tu na kwamba yeye amempenda kwa dhati mzee huyo.
“Mimi nina miaka 39, lakini mume wangu anaenda miaka 77 na zamani nilikuwa namuona ni mtu mkubwa sana kwangu, sikuwahi kumtamani wala kuwaza kuolewa naye hapo nyuma,” alisema.
Akizungumzia habari za watoto wa Mrema, Doreen alisema amejipanga vizuri kuilea familia hiyo kwa upendo uliotukuka.
“Nitakaa na familia hii kwa upendo, kwani ni watu tunafahamiana na wengine tuko na umri sawa na wengine wamenizidi umri, lakini tunaishi kama ndugu na huwa wamekuwa wakiniona kama dada, wengine tumelingana na wengine kunizidi.
“Katika kipindi ambacho nimeanza uchumba na mzee Mrema nimekuwa nikijitahidi kudumisha upendo na hata nilipoona pana shida nilijitahidi kutengeneza ili kuhakikisha familia inakuwa na amani,” alisema Doreen.
Akanusha kufuata mali
Akizungumzia madai ya yeye kufuata fedha, alisema kuwa yeye ni mwanamke anayejitegemea, anayefanya kazi na kwamba ana biashara zaidi ya tano ambazo zinamuingizia fedha, ikiwemo kampuni ya ulinzi na kampuni ya utalii.
“Tafuteni historia yangu nadhani mtaipata. Mimi ni mwanamke mpambanaji. Mimi sio mwanamke wa kupewa lakini mimi ni mwanamke niliyesimama, na nina msimamo wangu hata mali pia ninazo,” alisema.
Alichokisema Mrema
Awali akizungumza na waandishi wa habari, Mrema alisema ameamua kuoa mke mwingine kwa lengo la kumsaidia kutokana na afya yake ili aendele kumhudumia katika kumalizia uzee wake.
Alisema amemlipia mahari mke wake huyo Sh1 milioni na kwamba wazee walipoenda kujadili suala la mahari, jumla ya gharama zote za mahari zilikuwa ni Sh4.2 milioni.
Mrema aliwaacha hoi vijana alipowauliza “vijana mnakwama wapi”, kauli iliiyobua shangwe kutoka kwa watu waliokuwepo,
Taarifa ya nyongeza na Janet Joseph.